Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Primary Question

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE aliuliza:- Visiwa vilivyopo katika Ziwa Victoria, Wilayani Muleba havina usafiri salama na wa uhakika, na vilevile Bandari Ndogo ya Kyamkwikwi haina miundombinu stahili. (a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kupeleka kivuko ili kurahisisha usafiri kati ya Visiwa vilivyopo Ziwa Victoria na Miji ya Mwambao ya Ziwa hilo Wilayani Muleba? (b) Je, ni lini Serikali itajenga miundombinu muhimu ikiwemo maghala ya kuhifadhia bidhaa katika Bandari Ndogo ya Kyamkwikwi ili kuwavutia wafanyabiashara kutumia bandari hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuwa umekamilisha kumlipa mtu fidia unapoweka pesa kwenye akaunti yake. Kwa nini sasa Serikali isiwalipe wananchi wa Kyamkwikwi kwa kuhakikisha pesa zinaingia kwenye akaunti zao kabla ya mwisho wa mwezi huu ili jibu la Mheshimiwa Waziri liweze kuwa sahihi? Hawa watu hawajalipwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tunapozungumza Bandari ya Kyamkwikwi tunamaanisha huduma kwa Visiwa vya Bumbile, Makibwa, Nyaburo, Kerebe na Gooziba. Sasa kwa nini Serikali isichukue maoni ya wananchi waliyoyatoa kwa Kepteni Mwita wa MV Clarias juu ya chombo muafaka cha kuweza kwenda katika hivyo visiwa nilivyovirejea? Kwa sababu unapozungumzia MV Chato, MV Chato haiwezi kupita kwenye mkondo wa Makibwa kuelekea Kerebe.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI(MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Charles Mwijage, Mbunge wa Muleba Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuelekeze Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi atumie wataalam wake atueleze status ya fidia ya wananchi hawa, itakapofika Bunge la jioni Mheshimiwa Mbunge atapewa majibu sahihi ni lini wananchi wake watalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Mheshimiwa Mbunge anasema ni kwa nini tusichukue maoni ya wananchi waliyotoa kwa Kepteni Mwita kama alivyotaja, ili yaweze kufanyiwa kazi kwa lengo kubwa la kuboresha huduma ya usafiri katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tuyapokee maoni haya tuyafanyie kazi, yapitiwe na wataalam wetu tupate ushauri sanifu ili tuweze kutekeleza kama ambavyo tunapaswa kukidhi mahitaji ya wananchi. Kwa sababu lengo la Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi ni kuhudumia wananchi, tena wananchi wale ambao wana uhitaji mkubwa hasa wa pale Muleba Kusini na Kaskazini.