Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Aloyce John Kamamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Primary Question

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA K.n.y. MHE. AUGUSTINE V. HOLLE aliuliza:- Kumekuwa na mgogoro wa ardhi wa muda mrefu baina ya Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu na Kata ya Makere:- Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro huo?

Supplementary Question 1

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Kutokana na kuwepo kwa mgogoro huo kwa muda mrefu, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kwenda eneo lenyewe la mgogoro ili aweze kujionea hali halisi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, ikidhihirika kwamba katika utaratibu huo wa kugawa mipaka kuna makosa ambayo yatakuwa yamejitokeza wakati huo: Serikali iko tayari kuchukua hatua kwa wale ambao watakuwa wamekiuka taratibu za utoaji mipaka?

Name

Khamis Hamza Khamis

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Uzini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Kamamba ni: Je, nipo tayari kwenda katika eneo hilo ili nikajionee mwenyewe huo mgogoro? Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, ndani ya kipindi hiki cha Bunge la Bajeti nikipata nafasi ambayo itaniruhusu kuweza kwenda kwa sababu ni sehemu ya wajibu wangu kuyajua, kuyaona na kusikiliza changamoto za wananchi, nimhakikishie tu kwamba naenda kupanga ratiba na nitajitahidi nimjulishe tuweko pamoja ili kwa kushirikiana na maafisa kutoka hiyo Idara ya Wakimbizi, tuone namna ambavyo tunaenda kutatua hiyo changamoto ambayo kwa sasa wananchi inawakabili. Kwa hiyo, kwa ufupi ni kwamba, nipo tayari kufuatana naye kwenda katika eneo.

Mheshimiwa Spika, swali lingine ni: Je, ikidhihirika kama kuna makosa kuna watu wamefanya mambo mengine, mengine, Serikali ipo tayari kuchukua hatua? Serikali ipo kwa ajili ya kuwatetea, kuwasemea na kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi. Tumegundua kuna baadhi ya mambo yanafanywa na baadhi ya maafisa au baadhi ya watu ambayo yanavunja utaratibu na sheria katika maeneo haya. Kama Serikali tuko tayari kuchukua hatua ili kuhakikisha kwamba wengine wawe ni funzo na wasiendelee kufanya makosa hayo.

Mheshimiwa Spika, kikubwa nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba wakimbizi hawa tuliamua kuwapokea kwa sababu ya Mkataba wa Kimataifa ambao tuliukubali sisi wenyewe, kwamba ikitokea machafuko katika nchi fulani, basi kama wakija na tuki-prove kwamba kweli kuna tatizo, sisi tunawapokea.

Mheshimiwa Spika, pia tulikubaliana kwamba migogoro ikimalizika katika maeneo yao, sisi tupo tayari kuwarejesha katika maeneo yao kwa kushirikiana na mashirika na kwa kushirikiana na nchi zao.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimwambie tu kwamba eneo hili ikitokea wakimbizi hawa wameondoka na ikawa hakuna machafuko, maana yake ni kwamba eneo hili tutalirejesha kwa Serikali, halafu Serikali itaona namna ya kufanya. Unless ikitokea fujo nyingine huko kwenye nchi za wenzetu ikawafanya wakimbizi waje, tutawapokea na kuwahifadhi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.