Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:- Je, ni gharama kiasi gani na taratibu gani hutumika ili kupata huduma za ulinzi za SUMA JKT?

Supplementary Question 1

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza; kwa kuwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alitoa maagizo, taasisi na kampuni za Serikali kutumia Kampuni ya Ulinzi ya SUMA JKT. Je, hadi sasa ni makampuni mangapi au Taasisi ngapi za umma au Serikali zinazotumia Ulinzi wa SUMA JKT? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je ni fedha kiasi gani hadi sasa Kampuni ya SUMA JKT inadai kwa wateja wake? Ahsante. (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza la Mheshimiwa Angelina Malembeka kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze na kumshukuru sana Mheshimiwa Malembeka kwa namna ambavyo anafuatilia maelekezo ya viongozi wakuu, lakini pia kufuatilia maendeleo hususan ya SUMA JKT. Kwa kujibu maswali yake niseme tu baada ya maelekezo ya Amiri Jeshi Mkuu Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kuyatoa juhudi zimefanyika mpaka sasa idadi ya malindo 443 tunayo, ikiwemo malindo 259 ya Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma na malindo 184 ya watu binafsi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, ni kweli kwamba baada ya maelekezo yale tumefanya ufuatiliaji kama Wizara kulikuwa na rekodi ya madeni ya shilingi bilioni kama kumi na mbili na milioni mia tano (12,500,000,000) hivi, lakini baada ya uhakiki, deni hilo lilikuwa kwenye bilioni kumi na mbili na milioni tisini na sita (12,096,000,000), lakini kwa juhudi zilizofanyika asilimia 70 ya madeni yale ya kama bilioni nane na milioni mia tano (8,500,000,000) hivi zimeshalipwa. Bado tunalo deni kama la bilioni tatu nukta tano (3,500,000,000). Kwa hiyo, niendelee kuwashukuru wateja wetu kwa kutupa kazi, lakini niwashukuru pia kwa kuendelea kufanya malipo.

Mheshimiwa Spika, pia niwaombe wateja wetu waendelee kufanya malipo ya madeni haya kwani yapo manufaa makubwa kwamba tunapokusanya fedha hizi tunaendelea kuongeza ajira mbalimbali kwa vijana wetu lakini pia kadri tunavyoongeza huduma hizi za ulinzi, usalama kwenye mitaa unaongezeka kwa sababu pale ambapo tuna walinzi wetu wa SUMA JKT, ni msaada mkubwa kwa maeneo pia ya jirani na malindo yao. Kwa hiyo tunaendelea kupata manufaa makubwa, lakini kubwa zaidi pia tunaongeza uchumi katika nchi yetu. Ahsante sana. (Makofi)