Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Cecilia Daniel Paresso
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:- Wananchi wanaoishi jirani na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Wilayani Karatu kwa muda mrefu wamekuwa wakipata adha kubwa ya wanyama kuingia na kuvamia mashamba yao na wakati mwingine kujeruhi wananchi:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo hilo?
Supplementary Question 1
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa katika majibu ya Serikali wanaonesha kabisa kwamba mbadala wa wanyama hawa kutokuingia kwenye maeneo ya wananchi ni kutumia mbinu zilizoainishwa hapa, lakini mbinu hizi zinahitaji wananchi waelimishwe na wawezeshwe kwa sababu unapomwambia afuge nyuki na kadhalika, mwananchi huyu hana huo uwezo. Sasa je, Serikali inafanya nini kuwawezesha wananchi hawa kama kweli wana uhakika hili ndiyo litakuwa suluhisho ya kuondoa kero hii ya muda mrefu ya wanyama kuingia kwenye maeneo ya wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wananchi wanapoingia kwenye maeneo wakaribu mazao, fidia inayolipwa hailingani na uharibifu uliotokea, lakini hata fidia hiyo inayolipwa inachukua miaka na miaka mwananchi kupata fidia hiyo. Je, ni lini sasa Serikali italeta sheria hapa Bungeni tuifanyie marekebisho ili wananchi waweze kupata haki yao kwa jinsi ambavyo wanastahili? (Makofi)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecilia, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali imekiri kwamba kumekuwa na changamoto ya hawa wanyama wakali wakiwemo tembo kuendelea kuvamia mashamba ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii tumeendelea kuiongelea hata katika Bunge lako hili Tukufu kwamba kwa kuwa wananchi wameendelea kusogea kwenye maeneo ya hifadhi na asilimia kubwa ya maeneo ambayo shughuli za kilimo zinafanyika ni ushoroba wa wanyama.
Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwa ni changamoto kwa sababu wanyama hao sasa badala ya kupita yale maeneo wakaenda kwenye shughuli zao zingine zikiwemo pamoja na kutafuta madini pamoja na dawa asili wanazotumia ambazo sisi wanadamu hatuwezi kuzitambua, lakini wao kama nilivyokuwa nikiendelea kusema, wana Serikali yao, basi yale maeneo sasa wanapokutana na mazao wanafanya vurugu ambayo sio ya kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee kuhamasisha wananchi kama wataweza waachane na mazao yanayohamasisha tembo kupita katika maeneo ya mashamba yao. Kama itashindikana sana basi kwenye jibu langu lile la msingi nimeelezea mbinu mbadala ya kuweza kusaidia ili angalau kuepuka hili tatizo linaloendelea kujitokeza kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kutoa elimu kwenye maeneo husika na kupitia vyombo vya habari na hata hapa naendelea kutoa rai kwa wananchi kwenye maeneo ambayo mashamba yao yanavamiwa na tembo, wafuate haya tunayoelekeza ili wasaidie. Wapande pilipili, waweke hiyo mizinga ya nyuki, lakini pia waendelee kutoa taarifa kwa Serikali kwa sababu Serikali iko kwa ajili yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu fidia. Lengo la Serikali si ku-compensate mpaka mwananchi afurahi. Tukisema kila mwananchi apate kile ambacho anakusudia, basi hii Wizara haina haja ya kuwepo kazini kwa sababu uhifadhi ni gharama kubwa sana, lakini pia hata tunapotekeleza tunahakikisha kwamba tunahifadhi ili kuendelea kuiongezea Serikali mapato kupitia utalii, lakini kwa wakati huo huo tunaendelea ku-compensate wananchi wanaoathirika na hao wanyama. Kwa hiyo niombe rai kwa wananchi…
NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge, ameelewa.
Name
Dr. Charles Stephen Kimei
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Primary Question
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:- Wananchi wanaoishi jirani na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Wilayani Karatu kwa muda mrefu wamekuwa wakipata adha kubwa ya wanyama kuingia na kuvamia mashamba yao na wakati mwingine kujeruhi wananchi:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo hilo?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa fursa hii. Niseme kwamba kutokana na jitihada za wananchi wetu kule Vunjo kupanda miti na kuitunza kwenye mashamba yao ya kahawa na ndizi, ngedere na tumbili wameongezeka sana mpaka wamekuwa tishio kwa maisha ya watoto wachanga wanaoachwa nyumbani na ni vigumu sana kupambana na ngedere na tumbili kwa vile wana akili kama binadamu. Sasa nataka nijue, je Serikali ina suluhisho gani kuhusiana na ongezeko hili kuwaondoa hawa ngedere na tumbili? Ahsante. (Makofi)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI, MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kimei kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli changamoto hii ipo katika Mkoa wa Kilimanjaro na wiki iliyopita tu tulienda kuangalia changamoto hii katika Wilaya ya Rombo na kukawa kuna changamoto ya nyani pamoja na hao ngedere. Wizara ya Maliasili na Utalii ilitoa tamko kwamba tutaenda kuwahamisha hao nyani pamoja na ngedere, tuwapeleke kwenye maeneo ya hifadhi ambako kutafaa zaidi. Ahsante. (Makofi)
Name
Tecla Mohamedi Ungele
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:- Wananchi wanaoishi jirani na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Wilayani Karatu kwa muda mrefu wamekuwa wakipata adha kubwa ya wanyama kuingia na kuvamia mashamba yao na wakati mwingine kujeruhi wananchi:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo hilo?
Supplementary Question 3
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kadhia inayowapata wananchi wa Karatu ndiyo hiyo inayowapata wananchi wa Mkoa wa Lindi Wilaya ya Kilwa, Liwale, Lindi Vijijini, Nachingwea. Hata hivi juzi tu Wilaya ya Liwale, Kata ya Mbaya kuna mwananchi kule ameuawa na tembo. Pia wanaharibu mashamba ya vyakula na mazao kiasi kwamba wananchi wanaendelea…
NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.
MHE. TECLA M. UNGELE: Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo hili la wanyama kule Nachingwea, Liwale na Kilwa ili wananchi wa huko nao wawe na maisha mazuri? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Lindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekwishakuelezea kwenye jibu langu la msingi nimetoa rai kwa wananchi kupanda mazao ambayo yanaweza yakaepusha hawa wanyama. Hata hivyo, tukumbuke kwamba tunaishi kwenye maeneo ambayo yalikuwa ni njia za wanyama na tukumbuke kwamba hawa wanyama walikuwepo kabla hata ya sisi kuwepo.
Kwa hiyo, wanyama siku zote wanaenda kwenye maeneo yao ya siku zote ambayo sisi ndiyo tumefanya mashamba. Niwaombe wananchi tena kwamba waendelee kupanda mazao haya ambayo tunahamasisha, lakini ikishindikana basi wasilime kwenye maeneo ambayo yako kandokando ya hifadhi. Ahsante.