Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Aloyce Andrew Kwezi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kaliua

Primary Question

MHE. ALOYCE A. KWEZI - K.n.y. MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza:- Je, Serikali imechukua hatua gani kukabiliana na upungufu wa walimu na madawati hasa baada ya elimu ya msingi na sekondari kuwa bure?

Supplementary Question 1

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kuwa matatizo yaliyopo katika Jimbo la Tabora Mjini ya walimu na madawati yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Jimbo langu la Kaliua nilikuwa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja; Kaliua katika shule zetu za Usenye, Usinge, Ufukuto na maeneo mengine tuna upungufu wa walimu wa msingi na sekondari wapatao 873.

Je, Serikali ni lini itatupatia walimu hao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Kaliua tuna upungufu wa takribani madawati 4009. Je, Serikali ni lini itatupatia madawati hayo au fedha kwa ajili ya kukamilisha? (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE.DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aloyce Kwezi, Mbunge wa Kaliua kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kwanza la Mheshimiwa Mbunge alikuwa anazungumzia kwamba katika Jimbo lake kuna upungufu wa walimu 873 na akataka kufahamu ni lini Serikali tutapeleka walimu hao? Mimi nimuahidi tu kabisa kwamba katika mgawanyo ambao tutakwenda kuajiri wale walimu 6000 basi sehemu ya walimu wale baadhi tutapeleka katika Halmashauri yake na Jimbo lake la Kaliua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili kuhusu madawati, changamoto ya madawati kama tulivyoahidi na tumetenga katika bajeti yetu ambayo Waheshimiwa Wabunge mliipitisha kwamba katika yale madawati 710,000 sehemu ya hayo madawati tutapeleka katika jimbo lako. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge usiwe na wasiwasi na hilo. Ahsante. (Makofi)