Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abeid Ighondo Ramadhani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Kaskazini
Primary Question
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa maboma ya vituo vya afya yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika Kata za Makuro na Ngimu?
Supplementary Question 1
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naipongeza Serikali kwa juhudi hizi za kuboresha huduma za afya katika Jimbo la Singida Kaskazini ikiwemo maendeleo yanayofanyika kwenye hii Hospitali ya Wilaya pamoja na vifaa tiba na upanuzi wa wodi.
Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Halmashauri ya Wilaya ya Singida inakabiliwa na upungufu mkubwa sana wa watumishi wa Idara ya Afya, hasa wauguzi pamoja na madaktari: Je, Serikali ina mpango au mkakati gani wa kuhakikisha inaleta watumishi wa kada hii katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana ipasavyo?
Mheshimiwa Spika, pili, Serikali ilijenga Kituo cha Afya cha Mgori pale ambapo hata wewe ulifika siku ile ulipokuja kuniombea kura; lakini hospitali hii hadi sasa haijaanza kufanya kazi pamoja na kwamba kituo hiki kimekamilika kwa asilimia 100 kwa maana ya majengo; hapana vifaa tiba wala gari la kubebea wagonjwa.
Mheshimiwa Spika, napenda kujua Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inapeleka fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba pamoja na ununuzi wa ambulance kwa ajili ya kubebea wagonjwa? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani kwa ufuatiliaji wa karibu sana katika miradi ya maendeleo katika Jimbo lake hili la Singida Kaskazini ikiwepo miradi hii ya afya. Kimsingi ni kweli tunafahamu baada ya kazi kubwa sana iliyofanywa na Serikali ya kujenga miundombinu ya huduma za afya kwa maana ya Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali mpya za Halmashauri, automatically tumekuwa na uhitaji mkubwa pia wa watumishi wakiwemo Waganga, Madaktari pamoja na Wauguzi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuweka mipango ya kuendelea kuajiri watumishi hawa ili sasa vituo hivi ambavyo vimejengwa na kukamilika vianze kutoa huduma; na katika mwaka ujao wa fedha, Serikali imeomba vibali vya ajira kwa ajili ya wataalam hawa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Ighondo kwamba pamoja na maeneo mengine kote nchini, Serikali itahakikisha inawapangia watumishi katika Halmashauri ya Singida likiwemo Jimbo hili la Singida Kaskazini ili vituo vya afya viendelee kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, pili, ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Mgori kimekamilika muda mrefu na sasa kinahitaji kupata watumishi kama ambavyo nimeongea kwenye swali langu la msingi, pia gari la wagonjwa na vifaa tiba. Katika mwaka ujao wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa tiba kwa ajili ya Vituo vya Afya na Hospitali za Halmashauri mpya ambazo zinaendelea kukamilishwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakipa kipaumbele sana Kituo cha Afya cha Mgori ili na chenyewe kipate vifaa tiba na kuhakikisha kwamba kinaanza kutoa huduma.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na magari ya wagonjwa, utaratibu wa Serikali tunaendelea kuandaa mipango ya kupata magari ya wagonjwa katika Vituo vya Afya na Hospitali za Halmashauri kwa awamu kwa kadri ambavyo tutapata fedha. Hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hicho pia ni kipaumbele na Serikali itakwenda kukitimiza.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved