Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Leah Jeremiah Komanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Meatu

Primary Question

MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Kata za Mwamalole, Mbushi, Mwamanongu, Imalaseko, Mwamanimba, Mwabuzo na Kimali ili wananchi waweze kufaidika na huduma hiyo na kuchochea maendeleo katika Kata hizo?

Supplementary Question 1

MHE. LEAH J. KOMANYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuongeza vijiji tisa ambavyo viliachwa katika mzunguko wa pili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Mzunguko wa Pili wa REA Awamu ya Tatu, Serikali imetenga wigo mdogo wa kusambaza umeme katika vijiji ambao ni kilometa moja.

Je, Serikali haioni namna ya kuongeza wigo kutokana na mtawanyiko wa jinsi vijiji vyetu vilivyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kukatika katika kwa umeme katika Jimbo la Meatu na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla kumeathiri utekelezaji wa shughuli za maendeleo za wananchi: Je, ni lini kituo cha kupoozea umeme kitakamilika katika Mkoa wa Simiyu?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba katika upelekaji wa umeme kwenye maeneo yetu hatuwezi kufika katika maeneo yote kwa wakati mmoja. Ni kweli kwamba wigo uliopo hautoshelezi mahitaji tuliyokuwa nayo kwa sababu mahitaji ni makubwa kuzidi uwezo tuliokuwa nao.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba mara kwa mara tumekuwa tukiongeza wigo kwa maana ya kupanua scope ya kazi ambayo tunakuwa tumempa mkandarasi kulingana na mahitaji ya eneo husika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Leah, ambaye amekuwa mfuatiliaji mzuri sana wa masuala ya umeme ya Jimbo lake, kwamba tutakapokwenda katika utekelezaji, tutaongeza wigo kama ambavyo tayari tumeongeza wigo wa vijiji tisa ambavyo Mheshimiwa Waziri amevitaja hapo kuhakikisha kwamba tunawafikia wananchi wote kuwapelekea umeme.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili; ni kweli Mkoa wa Simiyu unapokea umeme kutoka maeneo matatu; Mwanza, Shinyanga (Ibadakuli) na Bunda. Umeme huo unakuwa siyo wa uhakika kwa sababu unasafiri umbali mrefu. Hivyo Serikali imechukuwa jitihada za kuamua kujenga kituo cha kupooza umeme pale Imalilo katika Mkoa wa Simiyu ambacho kitagharimu takribani shilingi bilioni 75 na ujenzi wa transmission line ya kilometa 109 kutoka Ibadakuli (Shinyanga) mpaka pale Imalilo.

Mheshimiwa Spika, kituo hiki tayari kilizinduliwa na Mheshimiwa Waziri. Ujenzi wake ulizinduliwa tarehe 3 Machi, kwa kuweka jiwe la msingi na tunatarajia kwamba mwezi Julai tutakuwa tayari tumekamilisha taratibu za manunuzi na kufikia mwishoni mwa mwaka ujao Desemba, kituo hicho kitakuwa kimekamilika chenye kuweza kusafirisha msongo wa kilovoti 220.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mkoa wa Simiyu utakuwa una uhakika wa umeme kwa sababu umeme mkubwa utakuwa unapoozwa pale na kusambazwa katika maeneo yote ya Mkoa wa Simiyu na hivyo tatizo la kukatika katika kwa umeme litakwisha. (Makofi)