Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Mussa Ramadhani Sima
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Primary Question
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanya Lugha ya Kiswahili kuwa bidhaa ya kimataifa ili kuendeleza na kukuza utamaduni wetu Duniani?
Supplementary Question 1
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa nchi nyingi sana kama alivyoeleza zimeamua kwa dhati kuwa na mtaala wa Kiswahili na ukizingatia pia tunao vijana wengi wabobezi kwenye eneo hili la Kiswahili. Serikali inaweka mkakati gani kuhakikisha vijana hawa wanapata ajira kwenye maeneo hayo ili tusije kuzidiwa na nchi zingine za Jirani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kumekuwa na ongezeko kubwa sana la misamiati ambayo inatokana na matukio mbalimbali na misamiati hii inaweza kuathiri lugha yetu ya Kiswahili. Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na ongezeko la misamiati hii? Ahsante sana. (Makofi)
Name
Pauline Philipo Gekul
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Babati Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Mbunge amehitaji kufahamu Serikali inajipanga vipi kuwasaidia vijana wetu wapate ajira kupitia lugha hii ya Kiswahili.
Mheshimiwa Spika, katika majibu yangu ya awali nilieleza kwamba Serikali ilishaanza mazungumza na Balozi zetu kupitia Wizara ya Mambo ya Nje kuhakikisha kwamba hawa wataalam ambao wamezamishwa, wameeleweshwa lugha ya Kiswahili na namna gani wafundishe wageni waweze kushirikiana katika Balozi zetu na madawati hayo yaanzishwe.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia BAKITA tunalifahamu jambo hili na nimesema kwamba tuna wataalam zaidi ya 1318 ambao wapo tayari na tumekuwa tukiwasaidia na wamekuwa wakiwasiliana na BAKITA kwa karibu waweze kupata ajira hizo.
Mheshimiwa Spika, swali la pili Mheshimiwa Mbunge alitaka kufahamu ni kwa kiasi gani Serikali inaangalia misamiati inapokuwa imezalishwa ni kwa kiasi gani tunafuatilia kama kuna mabadiliko ya mazingira. Mheshimiwa Mbunge nikuhakikishie kwamba Serikali kupitia BAKITA tumekuwa makini sana. Panapotokea mabadiliko yoyote ya kimazingira, ya kieneo au mazingira ya matukio yoyote BAKITA wamekuwa wakitafuta misamiati mbalimbali na kuhakikisha kwamba tunasanifisha misamiati hiyo lakini pia tunachapisha.
Mheshimiwa Spika, mfano, hivi karibuni nchi yetu imekumbwa na ugonjwa wa Covid lakini BAKITA tumejidhatiti na tumeshasanifisha covid – 19 inaitwaje kwa Kiswahili ambayo inaitwa UVIKO – 19. Nitoe rai kwa Watanzania kwasababu tunapenda lugha yetu tuhakikishe tunatumia lugha hii ya Kiswahili badala ya kusema covid – 19 tunaweza tukasema UVIKO – 19. Naomba kuwasilisha.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved