Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Felista Deogratius Njau
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FELISTA D. NJAU K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:- Je, nini kimepelekea mkwamo wa mkakati wa ujenzi wa Mji mpya wa Kawe kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na lini mradi huo utaendelea?
Supplementary Question 1
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Shirika la Nyumba la Taifa lengo lake kisheria ni kujenga nyumba za kupangisha na kuuza kwa wananchi wa kima cha chini na hii inasababisha wananchi wale kununua kwa bei rahisi. Hata hivyo, Shirika linashindwa kutekeleza jukumu hili kutokana na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo inakuwa kwenye vifaa vya ujenzi. Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuondoa hii kodi katika vifaa vya ujenzi kwa shirika la nyumba la Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, katika Ripoti ya CAG ya 2019/2020 ilionesha kwamba mradi huu usipokamilika mapema basi Serikali itaingia hasara kwa kulipa Shirika la Nyumba shilingi bilioni 100 na mpaka sasa wakandarasi wanalipwa. Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutekeleza mradi huu ili kuepuka hasara hii ya Taifa ambayo inaenda kuingia?
Mheshimiwa Spika, lakini pili, kuweza…
SPIKA: Aahaa, tayari maswali mawili. (Kicheko)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa sababu muda hautoshi, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge kwa sababu sheria ilipitishwa Bungeni humu aangalie malengo mazima ya uanzishwaji wa Shirika la Nyumba. Mbali na hilo alilolisema, lakini kwa sasa Shirika la Nyumba halipati ruzuku yoyote kutoka Serikalini na hivyo ni shirika linalojiendesha kibiashara. Kwa hiyo, katika miradi linayofanya kuna kujenga zile nyumba za gharama nafuu ambazo watu wananunua na wengine wanapanga, lakini pia linakuwa na miradi ya kibiashara ambayo inaliongezea pato Shirika ili kuweza kupanua miradi na kuweza kuongeza wigo wa kupata pesa kwa ajili ya kuendelea kujenga. Kama sasa hivi hapa Dodoma wana mradi wa nyumba 1,000 ambao wanaendelea kujenga nazo ziko katika viwango tofautitofauti.
Mheshimiwa Spika, ameongelea suala la kuondolewa kwa VAT kwa Shirika la Nyumba. Naomba niseme tu, katika suala zima la ujenzi ni mashirika mengi ambayo yanafanya kazi hizi za ujenzi ikiwemo Watumishi Housing. Kwa hiyo, unapozungumzia suala la kuondoa VAT, Watumishi Housing nao wanajenga nyumba kwa ajili ya wafanyakazi, sasa huwezi ukasema unaondoa VAT wakati haya mashirika yote yanafanya huduma ileile ya ujenzi wa nyumba kwa ajili ya kuboresha makazi kwa watu wetu. Kwa hiyo, hili kama linaonekana kwamba ni tatizo basi nadhani ni jambo la kuangaliwa upya, lakini kwa sasa bado VAT itaendelea kutozwa kama ambavyo inaendelea, japokuwa kama Wizara tulikuwa na mpango awali wa kuangalia namna bora ya kuweza kuliwezesha Shirika kwa kuangalia pia katika suala hilo la VAT, lakini bado mchakato haujafikia mwisho wake kwa sababu ya hali halisi ya ushindani na mashirika yanavyofanya kazi kama hiyo.
Mheshimiwa Spika, anaongelea suala la utekelezaji wa mradi ule kwamba unapata hasara na CAG ameonesha. Kwenye jibu langu la msingi nimesema ya kwamba kwa sasa tumepanga mradi huo utaendelea na ujenzi katika mwaka wa fedha huu 2020/2021 kwa sababu kubwa tu kwamba mradi wa Morocco Square ambao unaendelea mpaka sasa na tayari umefikia kwenye asilimia 92 ukikamilika ule tayari unaongeza vyanzo vya pesa kwa ajili ya ku-subsidize matumizi katika ujenzi ule. Pia tunayo Victoria Palace ambayo ina unit 88 lakini pale tayari 86 zimeshanunuliwa. Kwa maana hiyo ni pesa inayoingia kuliwezesha Shirika mbali na kutegemea mikopo basi pia kutoka katika vyanzo vya ndani vya miradi yake ya uwekezaji vitaenda kusaidia kuweza kukamilisha mradi ule ili kuweza kuboresha mji ule ambao uko katika eneo ambalo ni very prime.
Name
Dr. Josephat Mathias Gwajima
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kawe
Primary Question
MHE. FELISTA D. NJAU K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza:- Je, nini kimepelekea mkwamo wa mkakati wa ujenzi wa Mji mpya wa Kawe kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na lini mradi huo utaendelea?
Supplementary Question 2
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninalo swali kidogo la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, kukamilika kwa Mji Mpya wa Kawe utaongeza shughuli za kijamii kwa wananchi wanaokaa kwenye eneo la Kawe, hasa Mzimuni, Ukwamani na maeneo mengine. Kukamilika kwa Mji Mpya wa Kawe ni kiashiria cha Kawe yetu ijayo kuwa wilaya. Je, ni lini hasa Mji Mpya wa Kawe utakamilika? (Makofi)
Name
Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ilemela
Answer
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kumjibu Mheshimiwa Askofu Gwajima swali lake la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze kwa sababu baada ya kuingia tu Bungeni amekuwa akifuatilia sana mradi ule ili kuweza kuona unakamilika lini ili uweze kupendezesha maeneo yale. Azma ya Serikali hata ilipohamishia Makao Makuu hapa Mji wa Dar es Salaam ulibaki kama mji wa kibiashara. Kwa hiyo, lengo letu kama Serikali pia ni kuhakikisha kwamba mradi ule unakamilika ili ile maana halisi ya kufanya Dar-es-Salaam kuwa mji wa kibiashara na Kawe kuonekana kama satellite town ambayo tumekusudia kuifanya hivyo tumesema mwaka wa fedha unaokuja mradi ule utakwenda kukamilishwa. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi Mheshimiwa Wizara iko makini katika hilo. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved