Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Primary Question

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mradi wa Maji wa Kiburubutu katika Jimbo la Kilombero?

Supplementary Question 1

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kilombero, napenda kushukuru kwa majibu mazuri ya Wizara na tunaombea kweli huu mkopo upatikane na mradi huu ufanyike.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kutembelea Jimbo la Kilombero ili apite angalau kuzungumza na wananchi wa Zinginai, Magombera, Kanyenja, Mpanga na Muhelule ambao wana shida kubwa ya maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kutokana na hali ya udharura wakati tukisubiri mradi huu wa maji tayari Serikali ilishachimba kisima kikubwa katika Kata ya Lumemo ambapo kinatoa lita 30,000 kwa saa. Changamoto ni tenki la kuhifadhi maji yale kuwasambazia wananchi. Katika hali hii ya udharura, je, Serikali haiwezi kutujengea tenki wakati tunasubiri mradi wa maji wa Kiburubutu - Ifakara? (Makofi)

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la kwenda Kilombero ni moja ya majukumu yangu. Mheshimiwa Mbunge mara baada ya Bunge hili tutaweka utaratibu mzuri ili niweze kufika hapo. Naamini mpaka mwisho wa Bunge hili hata mradi huu utekelezaji utakuwa umeanza, kwa hiyo, nitakuja nikiwa na bashasha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ujenzi wa tenki kwa kisima kile ambacho tumekichimba, nia na dhamira kabisa ya Wizara ni kuona wananchi wanapata maji kwa umbali mfupi. Tumeshaweza kutoa fedha ya kuchimba kisima ni dhahiri lazima tutoe fedha ya ujenzi wa tenki. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge, kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha, ujenzi wa tenki utaanza kufanyika. (Makofi)