Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Daniel Awack Tlemai
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Karatu
Primary Question
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua mgogoro wa Wananchi wa Bugeli na Hifadhi ya Manyara pamoja na mauaji ya Wananchi yanayotokea mara kwa mara?
Supplementary Question 1
MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na kwamba sijaridhika na majibu ya Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mauaji yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika Hifadhi ya Lake Manyara; imetokea mwaka 2005, ikatokea mwaka 2015 na ikatokea tarehe 28/10/2020 ng’ombe wapatao zaidi ya 10 walipigwa risasi wakikutwa kijijini wakidai kwamba wamefuata nyayo. Askari wa Game Reserve wakaenda mpaka nyumba ya mtu huko kijijini na ng’ombe kumi kupigwa risasi.
Vilevile tarehe 28 mwezi wa Novemba, walipigwa risasi watu wanne kule msituni na kuchomwa moto. Nami ni shahidi, nikaenda msituni kule kuwatafuta wananchi hawa na kupata mabaki na mabaki yale yakapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali:-
Je, ni lini wananchi wale watapata majibu ya Mkemia Mkuu wa Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kwa kuwa, Hifadhi ile ya Lake Manyara ikihamishwa mipaka mara kwa mara kila mwaka kutoka Hifadhi ya Lake Manyara:-
Je, Waziri yuko tayari kufuatana nami kwenda kujionea mpaka jinsi unavyohamishwa katika Lake Manyara National Park?
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza niendelee kutoa pole kwa wananchi wa Karatu kwa kadhia hii ambayo waliipata. Niwakumbushe tu kwamba, wananchi kwa asilimia kubwa wanatumia nguvu ikiwemo kutotii sheria za uhifadhi na hivyo kusababisha hawa Askari sasa kujichukulia sheria ambazo kimsingi wananchi wangetii kusingetokea vurugu yoyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, tuendelee kushirikiana kuelimisha hawa wananchi. Hili suala la tarehe 28/11/2020 naomba tu waendelee kuwa subira kwa sababu ni taarifa za kiuchunguzi na Askari tayari walishachukua sample na wakapeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali. Hivyo, majibu yatatolewa na Jeshi la Polisi baada ya kufanyika uchunguzi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili. Niko tayari kuongozana naye kwenda kuangalia maeneo haya na kuonesha mipaka halisi kama ambavyo ameomba. Ahsante.
Name
Robert Chacha Maboto
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda Mjini
Primary Question
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua mgogoro wa Wananchi wa Bugeli na Hifadhi ya Manyara pamoja na mauaji ya Wananchi yanayotokea mara kwa mara?
Supplementary Question 2
MHE. ROBERT C. MABOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Bunda ina Kata 14 na wakulima wake mazao yao yameathirika sana na wanyamapori, hasa tembo; Kata ya Nyatwali, Bunda Store, Mcharo na Sazila:-
Je, ni lini Waziri atatembelea Halmashauri hii ili aweze kujionea uharibifu huo?
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nianze kwanza kwa kuwapongeza Wabunge wote ambao wanazungukwa maeneo ya uhifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sheria ambayo tulishapitisha kwamba wananchi wanapokutana na kadhia hii ya tembo na wanyama wengine tunatoa kifuta machozi. Nampongeza Mheshimiwa Robert Chacha kwamba ameendelea kulizungumzia suala hili la wananchi wake kuhakikisha wanapata kifuta machozi, lakini pia nimwahidi kwamba, nitafika kwenye eneo hilo ili tuweze kuzungumza na wananchi. Ahsante.
Name
Dr. Charles Stephen Kimei
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Primary Question
MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua mgogoro wa Wananchi wa Bugeli na Hifadhi ya Manyara pamoja na mauaji ya Wananchi yanayotokea mara kwa mara?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ubarikiwe sana. Kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inawajali sana wananchi wake wakiwemo wale wanaoishi kwenye Vijiji vya Kata ya Kirua Vunjo, Kilema, Marangu, Mamba na Mwika na wanaoishi kwenye vijiji vinavyozunguka msitu wa Mlima Kilimanjaro:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutathmini upya msimamo wake na kuwaruhusu wanavijiji hawa kutumia eneo la nusu maili ambalo limeainishwa kwenye mipaka? (Makofi)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nitoe rai tu kwa Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo ambayo tayari yanakuwa yameshatangazwa kuwa Hifadhi ya Taifa haturuhusiwi kufanya kitu chochote. Isipokuwa kama ana maombi ambayo anahitaji ifanyike tathmini, basi naomba kupitia Serikali ya Wilaya na Vijiji walete maombi kwenye Wizara, halafu tutaangalia tathmini kama itawezekana; na pale ambapo haiwezekani pia, tutawapa majibu. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved