Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Primary Question

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itafuta hati ya mashamba yaliyotelekezwa kwa zaidi ya miaka 20 Wilayani Mkinga hususan shamba la Kwamtili ili ardhi hiyo igawiwe kwa wananchi?

Supplementary Question 1

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naishukuru Wizara kwa majibu haya. Swali la kwanza; kwa kuwa taratibu hizi za Ilani zimekwisha kukamilika na kwamba mmiliki huyu anatumia ardhi isivyo stahili. Je. Waziri anatuambia nini kwa kuwa taratibu hizi zimekamilika ni lini sasa hati ya mashamba haya zitafutwa baada ya kupelekwa kwa mamlaka ya Mheshimiwa Rais? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa barua ya mapendekezo ya kufuta hati ya shamba hili yalizungumzia vile vile Shamba la Mwele ambalo, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja kutembelea Mkinga alitoa maagizo kwamba, ardhi ile imegwe kutoka kwenye shamba la Serikali kwa sababu, limetelekezwa kwa zaidi ya miaka 20. Je. Waziri yupo tayari kufuatilia jambo hili ndani ya Serikali ili agizo lile la Waziri Mkuu liweze kufanyiwa kazi? (Makofi)

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza amezungumzia kwamba taratibu zile zinazotakiwa kufuatwa katika ubatilishwaji zilishakamilika. Naomba kukiri ni kweli kwasababu barua ya ubatilisho ilitoka tarehe 10 Machi, 2020 maana yake kufikia Juni, 2020 tayari utaratibu ule ulikuwa umekwisha. Lakini wakati huo huo mmiliki huyu alileta utetezi wake akitetea kwamba asiweze kunyang’anywa kwasababu alizokuwa amezilieleza. Lakini baada ya kuangalia pia ilionekana kwamba miliki ile ilikuwa imewekezwa kama dhamana kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini hiyo pia haituzuii kama wizara tumetoa maelekezo kwenye halmashauri kwasababu ile hati imeshawekwa dhamana katika Benki, na Benki yenyewe ni Benki ya Nje kwa hiyo tumeshaelekeza na tayari wamekwisha toa ilani kwa ajili ya kubatilisha tena wamempelekea na yule mmiliki wa Benki ili ajue kwamba dhamana aliyonayo kisheria kwa sheria za Tanzania sasa haitakiwi iwe kule kama ambavyo inapaswa.

Kwa hiyo, tunasubiri hizi siku zikiisha basi tutaweza kufanya kile ambacho kinatakiwa kufanywa kisheria na watu wa Halmashauri ya Mkinga wataweza kufaidika na lile shamba. Namuomba tu Mheshimiwa Mbunge basi awe na subira katika hilo kwasababu tayari taratibu zinafanyika na ilani imekwishatumwa kwenye ile Benki ya Nje pamoja na kwa mmiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Swali lake la pili anaongelea suala Mweru ambalo lilikuwa na maelekezo pia ya Waziri Mkuu. Kwanza nichukue fursa hii pia kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Dunstan Kitandula kwasababu amekuwa akifuatilia sana. Nakumbuka hata mwaka jana, mwaka juzi kuna shamba la MOA alilipigia kelele taratatibu zilifuatwa likabatilishwa na wakaweza kupewa na sasa wananchi wanalitumia kwa mujibu wa waliyoelekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika hili naomba nimuhakikishie kwamba, tutachukua speed isiyo ya kawaida tunahakikisha kwamba tunafanya ufuatiliaji na kama umemsikia pia Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita amesema hana mzaha na wale ambao wana hodhi ardhi bila ya kuzitumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Na sisi kwa kasi ile ile tutaendelea mbali na hilo shamba la Mweru tutaangalia pia na mashamba mengine katika maeneo mengine ambayo wameyahodhi ili tuweze kuchukua hatua stahiki na yaweze kutumika kwa matumizi ambayo yataleta faida kwa wananchi lakini kwa Taifa kwa ujumla. Ahsante.