Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maimuna Salum Mtanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Newala Vijijini

Primary Question

MHE. MAIMUNA S. MTANDA aliuliza:- (a) Je, ni lini Serikali itaimarisha na kuboresha miundombinu ya maji ya Mamlaka ya Maji Makonde ili Wananchi waweze kupata maji ya uhakika? (b) Je, Serikali inachukua hatua gani za dharura kuboresha upatikanaji wa maji Newala Vijijini ambapo kwa sasa uzalishaji ni ujazo wa lita 6,700 tu kwa siku badala ya lita 23,741?

Supplementary Question 1

MHE. MAIMUNA S. MTANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante. Naomba kuiuliza wizara maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Tatizo la maji kwenye Jimbo la Newala Vijijini limekuwa ni sugu, wananchi wa Newala Vijijini wanakunywa maji ya kuokota ambayo wanaokota kipindi cha mvua, maji ambayo huwa yanaoza na yanatoa harufu. Lakini tunacho chanzo kikubwa cha Bonde la Mitema ambalo Serikali ikiwekeza kwa kiasi kikubwa bonde lile litatua kabisa changamoto za maji kwa sababu maji yaliyopo katika bonde lile yana mita za ujazo zipatazo 31,200 lakini mahitaji ya wananchi wa Newala, Tandahimba pamoja na Nanyamba kwa siku ni mita za ujazo 23,441.

Je Serikali imejipangaje kuhakikisha inaweka fedha za kutosha katika bonde la Mitema ili tatizo la maji liweze kukoma na wananchi waweze kupata maji ya kutosha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika kituo cha Mto Ngwele kulikuwa na tatizo la pump house pamoja na transformer. Lakini bahati nzuri Januari mwaka huu pump house imerekebishwa na TANESCO wameshapelekwa pale transformer iko pale haijafungwa hadi leo hii ikaweza kusukuma maji. Nini kauli ya Serikali kwasababu wananchi wanaendelea kutaabika kupata maji wakati transformer iko pale wanashindwa kuifunga. (Makofi)

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge kwanza nakupongeza sana wewe ni Mbunge wa Jimbo, mwana mama Hodari na umekuwa ukifuatilia kwa uchungu sana masuala la maji ili kuokoa kina mama wenzako kuhakikisha wanatuliwa ndoo kichwani kama ambavyo wizara tunakesha, tunafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kwamba kina mama lazima tuwatue ndoo kichwani na maji yapatikane umbali mfupi kutoka kwenye makazi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake namba moja anauliza fedha za kutosha kuwezesha bonde la Mitema. Hii ni moja ya kazi ambazo tumeagiza RUWASA waweze kushughulikia, hii itafanyika ndani ya mwaka wa fedha ujao na kuona kwamba tuanze kuuona usanifu unakamilika na kila kitu kinakwenda vizuri ili maji yaweze kupatikana kwenye chanzo cha uhakika. Wakati tuna hitimisha bajeti yetu nimeongelea suala la Newala hata mimi ni mwana mama nisingependa kuona watu wanaendelea kutumia maji ya kuokota kwa karne hii na tumshukuru Mungu tumempata Rais mwana mama ambaye kiu yake kubwa ni kuona kina mama wanatuliwa ndoo kichwani. Mheshimiwa Mbunge Maimuna hili tutashirikiana kwa pamaja kuona kwamba tunakamilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusiana na transformer ambayo ipo pale. Sisi kwa upande wa wizara yetu tuliweza kushughulika na pump house na imeshakamilika. Kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Nishati kuona kwamba sasa ile transformer inakwenda kufungwa haraka iwezekanavyo ili matumizi ya umeme kwenye kusukuma maji yakaweze kufanyika na watu wakanufaike na mradi ambao umeshakamilika.