Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Tumaini Bryceson Magessa
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busanda
Primary Question
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza:- Je, ni lini Serikali italipatia Jimbo la Busanda Vituo vya Afya hususan Tarafa ya Butundu na Tarafa ya Busanda?
Supplementary Question 1
MHE. TUMAINI B. MAGESSA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, majibu haya yaliyotoka ni ya Wilaya ya Geita, nami maswali yangu yalikuwa yanaelekea Jimbo la Busanda. Kwa hiyo, nilipokee tu kwa sababu Jimbo la Busanda liko ndani ya Wilaya ya Geita, lakini mgawanyo wake inawezekana Wilaya ya Geita usiwe ule ambao tunautarajia kuupata kule Busanda.
Swali langu la kwanza la nyongeza: Je, Serikali ina mpango gani; kwa sababu sasa hivi kuna ramani mpya ya vituo vya afya na vituo vingi vinavyotajwa vina ramani ya zamani ikionekana wazi kwamba kuna upungufu mkubwa wa wodi za wanaume na wodi za wanawake: Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya hivi vituo vya afya vijengwe kwa ramani hii mpya ya sasa? (Makofi)
Swali la pili; pamoja na vituo vilivyotajwa, kuna upungufu mkubwa sana wa uimarishaji wa upatikanaji wa dawa kwenye vituo hivyo: Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba vituo hivi sasa vinaweza kuwahudumia wananchi na upatikanaji wa dawa ukawa kama uliokuwa unapatikana awali; kwa sababu, kwa miaka miwili sasa wananchi wana vituo vya afya lakini hawapati dawa kwa ajili ya kuwahudumia? (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Swali la kwanza Mheshimiwa Mbunge alilokuwa anahitaji kufahamu ni juu ya ramani ambazo zimekuwa zikitolewa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye ujenzi wa vituo vya afya kwamba, wakati mwingine haziendani na mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kikubwa ambacho naweza nikamwambia Mheshimiwa Mbunge, zile ramani zilizoletwa katika maeneo husika ni minimum standards. Maboresho yanaweza yakafanyika kulingana na maeneo husikwa. Kwa hiyo, endapo kutakuwa na hitaji fulani, watu wa eneo husika wanaweza kufanya maboresho pamoja ikiwemo kuijulisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI, nasi tutawapa ruhusa hiyo ili kuhakikisha hivyo vituo vinajengwa kulingana na mahitaji husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili amezungumzia kwamba, tumekuwa na vituo lakini bado mahitaji ya dawa hayapatikani vya kutosha. Jambo hili nafikiri karibu Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto tumekuwa tukilijadili hili kila wakati na tumekuwa tukilitolea ufafanuzi. Kikubwa, wote tunafahamu kwamba, mahitaji kama bima za afya, fedha ambazo wananchi wanatoa pale pale, lakini kwa hivi karibuni Serikali imeongeza bajeti kubwa kwenye madawa na usimamizi wake mzuri. Kwa hiyo, tutaendelea kuongeza dawa katika vituo vyetu na tutaongeza vile vile usimamizi ili ziweze kuwafikia walengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Name
Anne Kilango Malecela
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Same Mashariki
Primary Question
MHE. TUMAINI B. MAGESSA aliuliza:- Je, ni lini Serikali italipatia Jimbo la Busanda Vituo vya Afya hususan Tarafa ya Butundu na Tarafa ya Busanda?
Supplementary Question 2
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii. Kwa kuwa, Mkoa wa Kilimanjaro asilimia 40 ni Wilaya ya Same; na kwa kuwa Wilaya ya Same ina majimbo mawili; na Wilaya nzima ina Hospitali ya Wilaya moja: Je, Serikali haioni kwamba lile eneo ni kubwa sana, sasa upande wa Mashariki nao wapate japo Hospitali ya Wilaya moja? (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, sera yetu ya sasa ni kwamba kila Halmashauri ya Wilaya ipate hospitali yenye hadhi ya wilaya na ndio maana kwenye bajeti hata ya mwaka huu ambayo tumeipitisha mwaka 2021/2022 Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuhakikisha hata zile Halmashauri ambazo hazikuwa na hospitali za Halmashauri tutazijenga mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili alilolileta hapa ni wazo kwamba angalau jimbo kwa imbo liweze kupata lakini tutaendelea kuzingatia kuleta huduma bora za afya katika maeneo yote ikiwemo kujenga vituo vya afya na zahanati kuhakikisha huduma zinawafikia walengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lengo la kwanza ni kuhakikisha kwamba tunamaliza kwanza Halmashauri zote halafu maombi mengine tutakuja kuyazingatia kulingana na mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved