Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Primary Question
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA (K.n.y. MHE. CATHERINE V. MAGIGE) aliuliza:- Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kuongeza bajeti ya TARURA Wilayani Ngorongoro ili kukabiliana na uharibifu wa barabara uliotokana na mvua kubwa zilizonyesha msimu wa mwaka 2019 na 2020?
Supplementary Question 1
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza, lakini pia nitumie fursa hii kuishauri Serikali kwamba, kwa kuwa barabara zetu za vijijini haziachi kuharibiwa na mvua kila wakati, nashauri kila Wilaya ambayo haina mtambo wa kutengeneza barabara, wapewe mtambo ili kuweza kunusuru barabara hizi badala ya kungojea makandarasi wapatikane ndipo barabara zifanyiwe repair? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza. Kuna mkandarasi anaitwa Balcon Construction Tanzania Ltd. ambaye amepewa contract ya shilingi 115,357,520/= kutengeneza barabara ya kwenda Kitongoji cha Esokonem mlimani Gelai kwenye Kata ya Gelailumbwa, ambaye ametelekeza barabara, baada ya kuiharibu barabara hiyo ambayo imetengenezwa kwa nguvu ya wananchi na kutifua mawe makubwa kiasi kwamba haipitiki tena. Tangu mwezi wa Kumi na Moja mwaka 2020 barabara hiyo imesimama, haipitiki. Naomba Serikali iseme neno kuhusu hilo: Je. Serikali itamchukulia hatua gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kuna barabara za mitaa ya Mji Mdogo wa Longido na ambazo zilikuwa ni sehemu ya ahadi ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, kutoka pale kwa DC kwenda Makao Makuu ya wakazi wa Halmashauri ya Longido, ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami na tangu mwezi wa Kumi na Moja mwaka 2020 kazi imesimama kwa sababu mkandarasi hajalipwa certificate ambayo amewasilisha; je, Serikali itatimiza lini takwa lake la kumlipa mkandarasi huyo ili kazi imalizike? (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Mbunge wa Longido, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amejaribu kuitaka Serikali tueleze ni hatua gani tutachukua kwa Mkandarasi ambaye ameitelekeza barabara aliyoitaja iliyopo jimboni kwake. Kwa kuwa taarifa hizi ndio nazipata hapa, naomba niiagize TARURA Makao Makuu kwa kushirikiana na Mkoa wa Arusha waweze kutuletea taarifa haraka iwezekanavyo ili sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tujue ni hatua gani tutachukua. Endapo itabainika kwamba Mkandarasi huyo ametelekeza barabara basi tutamnyang’anya hiyo contract na tutatangaza upya ili tupate mkandarasi mwingine atakayemalizia hiyo barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ahadi ambayo ilitolewa na Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli ya barabara kutoka DC kwenda Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Longido eneo hilo ambalo ametaja Mheshimiwa Mbunge, kazi hiyo imesimama na amesema sababu ya kusimama ni yule Mkandarasi kutokulipwa fedha. Naomba hili nilifuatilie ili tuone ni hatua gani ambazo ofisi zetu zimekuwa zinachukua kwa sababu mpaka Mkandarasi labda hajalipwa maana yake kutakuwa labda wana-process zile certificates ambazo amekuwa amezileta katika Ofisi ya Rais TAMISEMI. Kwa hiyo naomba nilifuatilie ili tuweze kui-fast truck na kuirahisisha ili waweze kulipwa na hiyo barabara iweze kukamilika. Ahsante sana.
Name
Justin Lazaro Nyamoga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Primary Question
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA (K.n.y. MHE. CATHERINE V. MAGIGE) aliuliza:- Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kuongeza bajeti ya TARURA Wilayani Ngorongoro ili kukabiliana na uharibifu wa barabara uliotokana na mvua kubwa zilizonyesha msimu wa mwaka 2019 na 2020?
Supplementary Question 2
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kata ya Udekwa, Kata ya Ukwega, Kata ya Kimara na Kata ya Idete hazina mawasiliano kabisa kutokana na mvua ambazo zimeharibu kabisa barabara.
Je, Serikali ipo tayari kutoa fedha za dharura kwa ajili ya barabara ya kata hizi ambazo zina mazao mengi ili ziweze kutengenezwa na wananchi waweze kuendelea na shughuli zao?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ameomba fedha za dharura katika barabara ambazo ameziainisha hapa. Nimwambie tu moja ya kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na TARURA katika kipindi hiki ni pamoja na kupeleka fedha za dharura katika maeneo yote ambayo yalikuwa yemeathirika sana na mvua kubwa ambazo zilikuwa zimenyesha. Pamoja na fedha ndogo ambayo tunayo kwa sababu katika fedha za dharura ambayo tunayo kwa mwaka huu ambayo unakwisha ni kama bilioni 12 ambazo tulikwenda kuziainisha katika yale maeneo ambayo yana uhitaji mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ameainisha maeneo hayo, niseme tu kabisa Ofisi ya Rais, TAMISEMI itapitia hayo maeneo na ione kama kuna udharura wa haraka kabisa ili tuweze kupeleka fedha na hizo barabara ziweze kupitika. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved