Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kunti Yusuph Majala

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. KUNTI Y. MAJALA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua changamoto kubwa ya maji inayowakabili wananchi wa Mji wa Chemba?

Supplementary Question 1

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; suala la mradi huu wa Dola za Kimarekani milioni 500 ni mradi ambao umekuwa wa kila siku tunaendelea kusimuliwa, kuandikiwa kwenye vitabu, lakini utekelezaji wake hauleti tija kwa Watanzania. Kama Waziri alivyosema kwamba mradi huu ndio ulitarajiwa kwenda kukidhi maji kwa wananchi wa Wilaya ya Chemba ukiwemo Mji wa Chemba. Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya visima viwili ambavyo vimechimbwa mwaka 2017 lakini mpaka leo visima vile havijafungwa pump wala miundombinu yoyote haijaweza kutekelezwa? Lini Serikali itatoa fedha ili kwenda kukamilisha huo mradi wa visima hivyo viwili ambavyo vimechimbwa mwaka 2017 na mpaka sasa ni miaka minne? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Wilaya ya Chemba tunatarajia kupata maji ya kutosha kutokana na mradi mkubwa wa Bwawa la Farkwa, lakini bwawa hilo si tu kwa Wilaya ya Chemba bali litasaidia pia kupunguza adha ya maji kwenye Jiji la Dodoma, Wilaya ya Bahi na Wilaya ya Chamwino. Natamani kusikia kauli ya Serikali, ni lini mradi huu utakwenda kuanza rasmi kwa sababu hata kwenye bajeti ya maji hakujatengwa fedha za kwenda kuanzisha huu mradi badala yake tunasubiri fedha za wafadhili. Kwa hiyo nataka nijue Serikali ni lini inaenda kuanza Mradi wa Farkwa? Ahsante. (Makofi)

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kunti Majala, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipende kumpongeza Mheshimiwa Kunti, amekuwa ni mfuatiliaji mzuri pamoja na kwamba ni mjumbe katika Kamati yetu ya Maji, amekuwa na mchango mkubwa, lakini vilevile nipende pia kumpongeza kwa sababu ana mahusiano mazuri na Mbunge wa Jimbo, wamekuwa wakifuatilia kwa pamoja masuala haya. Sisi kama Wizara tumesema kwamba Chemba maji lazima yaje. Pamoja na kwamba kuna visima hivi viwili vilichimbwa mwaka 2017, lakini mwezi Machi, 2021 tumeongeza kuchimba visima vinne, ili visima vile vinne vya mwaka huu tunakuja sasa kutengeneza mtandao wa usambazaji maji kuelekea kwenye vituo vya uchotaji maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anaongelea Bwawa la Farkwa. Hili bwawa ni juzi tu Mheshimiwa Waziri ametoka kuliongelea kama moja ya mikakati ya kuhakikisha maji Chemba yanafika. Pamoja na hilo tuna Mradi mkubwa wa Ziwa Victoria ambao pia Chemba utafika. Kwa hiyo bwawa hili litakwenda sambamba na mradi huu mkakati wa Ziwa Victoria. Tuendelea kuvuta subira, tumetoka mbali tunakokwenda ni karibu, maji Chemba yanakuja bombani.

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. KUNTI Y. MAJALA aliuliza:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua changamoto kubwa ya maji inayowakabili wananchi wa Mji wa Chemba?

Supplementary Question 2

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza niipongeza Wizara ya Maji kwa kazi wanayoifanya, lakini naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Kutokana na ongezeko la watu kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Makete, hasa hasa Makete Mjini tuna uhitaji mkubwa wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Mradi wa Maji wa kutoka Kitulo, Isapulano kwenda Iwawa Makete Mjini ili kuongeza upatikanaji wa maji kutokana na kwamba tayari kama halmashauri tulishawasilisha andiko letu la mradi wa bilioni 3.1 kwenye Wizara? Ahsante.

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Festo Sanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli andiko hili tumeshalipokea pale Wizarani na mipango ya kuona namna gani ya utekelezaji itaweza kufanyika tayari pia tunashughulikia. Pia nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Festo Sanga amekuwa ni mfualitiaji mzuri wa miradi hii yote, yeye mwenyewe amefuatilia na sasa hivi tumeshampelekea Mradi wa Maji wa Lupila milioni 100, lakini vile vile tumempelekea Mradi wa Maji wa Bulongwa milioni 100. Yote haya ni matunda ya yeye kuwasemea vyema wananchi wake. Hivyo sisi kama Wizara hatutakuwa kikwazo kwa Mheshimiwa Sanga na kwa wote anaowawakilisha, tutahakikisha na mradi huu wa bilioni 3.0 nao tunakuja katika utekelezaji. (Makofi)