Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:- Je, Serikali ipo tayari kuanzisha Wilaya ya TANESCO kwa ajili ya kuhudumia viwanda na wananchi katika Mji wa Mafinga ili kuendana na kasi ya uchumi wa viwanda?

Supplementary Question 1

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwanza kabisa, nakupongeza kwa kurudi kwenye hicho kiti, tuliku-miss sana Mzee wa Jaza Ujazwe. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali lakini nina maswali mawili ya nyongeza na msingi wa maswali haya ya nyongeza la kwanza, asilimia thelathini ya muda wa kufanya kazi katika Mji wa Mafinga na maeneo yanayozunguka unapotea kutokana na kukatikakatika kwa umeme. Hii maana yake ni nini? Saa za kufanyakazi katika nchi yetu wastani kwa mujibu wa sheria ni saa nane. Kwa hiyo, kwa siku tunapoteza wastani wa saa mbili au dakika 144, kwa wiki tunapoteza wastani wa saa 16 au dakika 1008, kwa mwezi tunapoteza saa ya kufanya kazi 40 au dakika 2,400. Maana yake ni kwamba tunapoteza kwanza mapato kwa TANESCO yenyewe lakini pia mapato kwa wananchi na kwa Serikali. Swali langu linakuja, kama tuna viwanda vikubwa 80 kwa nini tusiwe na Wilaya ya TANESCO katika Mji wa Mafinga kama ambavyo katika Wilaya ya Ilala, Wilaya ya Temeke, Wilaya ya Kinondoni wana Wilaya za TANESCO zaidi ya moja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, toka asubuhi nimepokea simu na meseji nyingi sana kutoka kwa wananchi wakiuliza kwamba wanashindwa kununua LUKU leo siku ya pili jambo ambalo linakosesha TANESCO mapato lakini pia shughuli za uzalishaji kwa wananchi kukosa umeme zinakuwa zimesimama. Nini kauli ya Serikali kuhusiana na jambo hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chumi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la kwanza Mafinga ni mojawapo ya maeneo ambayo TANESCO inafanikiwa kwa asilimia kubwa kupeleka umeme wa uhakika, kwa sababu inayo sub-station ambayo ipo jirani kilometa kama 80 kutoka kwenye huo mji wenyewe eneo la Igowolo na umeme huo unatokea Iringa.

Pia tunayo line nyingine ndogo inayotoka Iringa moja kwa moja kupeleka umeme Mafinga. Kwa hiyo, Mji wa Mafinga unalishwa na line mbili za umeme, ikitoka moja inaunganishwa nyingine, ikitoka nyingine inaunganishwa hiyo moja. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Chumi aendelee kutuvumilia katika maboresho tunayoendelea kuyafanya kuhakikisha umeme unakuwa wa uhakika na kama ambavyo tumeshasema mara kwa mara eneo la Iringa, Mafinga, Mbeya na Bukoba tunaathari sana za kupatwa na radi kwa hiyo tunaendelea kurekebisha mifumo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali la pili la LUKU, nikiri kwamba kwa siku mbili na leo itakuwa ni ya tatu tumekuwa tuna tatizo na tumepata shida kubwa sana kwenye mfumo wa kidigitali wa kununua na kuuza LUKU. Tunawahakikishia kwamba tunalishughulikia, tunazo system mbili; system moja imekufa, ilipata hitilafu kidogo na tayari tumeshapata itengenezwe na hiyo system nyingine iliyobakia inabeba mzigo mkubwa sana na hivyo inashindwa kuhudumia wateja wote kwa wakati. Tunaahidiwa na wataalamu wetu kwamba kabla ya siku ya leo haijaisha tatizo hilo litakuwa limekwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge na kupitia forum hii, naomba niwaambie Watanzania wote kwamba ukifika katika ofisi za TANESCO unaweza ukanunua umeme. Shida tunayo kwenye ile data base au mfumo unaouza kupitia kwenye mifumo ya kibenki na mifumo ya simu, ile ndiyo imepata shida kidogo lakini ukifika Ofisi ya TANESCO unaweza ukanunua umeme. Naomba radhi kwa niaba ya wenzangu lakini tunawahakikishia kwamba leo kabla siku haijaisha tutajitahidi kuhakikisha huduma hiyo inarejea ili Watanzania waendelee kupata huduma ya LUKU kama kawaida.

Name

Lucy Thomas Mayenga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:- Je, Serikali ipo tayari kuanzisha Wilaya ya TANESCO kwa ajili ya kuhudumia viwanda na wananchi katika Mji wa Mafinga ili kuendana na kasi ya uchumi wa viwanda?

Supplementary Question 2

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa usambazaji wa umeme kwa kutumia REA umekuwa ukitumia transfoma za KV 50 lakini Serikali kwa ujumla na kama Taifa tumekuwa tukihamasisha sana shughuli za uzalishaji. Je, Serikali haioni kwamba kwa kuendelea kutumia umeme huu wa KV 50 wakati idadi ya watu na shughuli za uzalishaji zinaongezeka baadaye kuonekana kwamba umeme huu hautoshi. Kwa nini Serikali isianze sasa kubadilisha badala ya kuweka KV 50 ianze kwa maeneo kidogo kidogo kuweka KV 100? Ahsante.

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Lucy, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa tunapeleka umeme tunaangalia na kuzingatia mahitaji ya wananchi walio katika maeneo hayo. Transformer ya KV 50 ni transformer kubwa inaweza kuhudumia wateja zaidi ya 200 katika eneo moja. Kwa hiyo, kadri wateja wanavyoongezeka na sisi tutazidi kuboresha na kuongeza ukubwa wa transformer tunazoziweka katika maeneo husika.