Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Primary Question

MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji Ruduga – Mawindi ili kuwatua ndoo kichwani akina mama wa Mbarali?

Supplementary Question 1

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri. Naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali ilitenga fedha kujenga visima nane vya maji katika Wilaya ya Chunya katika Kata za Sangambi, Shoga, Matunda, Skambikatoto, Rualaje, Nkung’ungu na Soweto mpaka Itumbi, lakini mpaka sasa hivi fedha hizo hazijatoka.

Je, ni lini fedha hizi zitatoka ikiwa imebakia takribani siku 40 mwaka huu wa fedha uishe?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwenye chanzo cha maji cha Chunya Mjini kuna takribani visima nane vilichimbwa, lakini visima viwili pekee ndivyo vinavyofanya kazi.

Je, ni kwa nini visima hivi vingine, takribani sita, havifanyi kazi?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Mbarali kuwa miongoni mwa Wabunge ambao wamepitisha bajeti yetu na kutupatia fedha zaidi ya shilingi bilioni 680. Kwa hiyo, jukumu letu sisi kama Wizara ni kuhakikisha tunakwenda kutatua tatizo la maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu fedha ambazo kwa ajili ya uchimbaji wa hivyo visima; nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya Saa 07:00 naomba tukutane ili tuweke commitment ya Wizara tuweze kuku-support kuhakikisha wananchi wako wanapata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusu suala zima la visima pale katika eneo la Chunya Mjini, kuna visima nane, viwili vinafanya kazi. Nimetoa maelekezo mahususi. Wizara ya Maji inafanya mageuzi makubwa katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma ya maji safi na salama kama Mheshimiwa Rais maelekezo yake ametupatia sisi Wizara ya Maji. (Makofi)

Kwa hiyo, maelekezo ambayo tumeyatoa kwamba, kwa wataalam wetu wote kusimamia na kufuatilia, hususan aidha visima ama miradi ya maji, kuhakikisha vyote vinafanya kazi na wananchi waende kupata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Oscar Ishengoma Kikoyo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Primary Question

MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji Ruduga – Mawindi ili kuwatua ndoo kichwani akina mama wa Mbarali?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipatia nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Muleba iko pembezoni mwa Ziwa Victoria, lakini inalo tatizo kubwa la uhaba wa maji na tunao mradi mkubwa ambao usanifu na upembuzi yakinifu umekamilika.

Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwa ajili ya kata sita za Wilaya ya Muleba; Kata ya Gwanseri, Kata ya Muleba Mjini, Kata ya Magata Karutanga, Kikuku, Kagoma na Buleza?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Muleba kwa namna bora na nzuri ambayo kwa kufuatilia wananchi wake waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa ambalo sisi kama Wizara na Bunge lako tukufu, sisi kama Wizara ya Maji tumesema hatuna sababu tena ya Watanzania kulalamika suala la maji. Mwenyezi Mungu ametupa rasilimali toshelevu, tuna rasilimali ya maji mita za ujazo zaidi ya bilioni 126. Tuna mita za ujazo bilioni 105 juu ya ardhi ikiwemo mito pamoja na mabonde na bilioni 21 ambayo iliyokuwa chini ya ardhi.

Kwa hiyo, mkakati ambao tumeuweka sisi kama Wizara na katika bajeti yetu kutumia maziwa, rasilimali toshelevu, kuhakikisha kwamba tunatatua tatizo la maji na moja ya maeneo ambayo ya kipaumbele ni vijiji ambavyo vipo kandokando ya mito ama maziwa. Nataka nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi ni Wizara ya Maji si Wizara ya ukame. Tunakwenda kutatua tatizo la maji kwa wananchi wako, ahsante sana. (Makofi)

Name

Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji Ruduga – Mawindi ili kuwatua ndoo kichwani akina mama wa Mbarali?

Supplementary Question 3

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mradi wa chujio wa Maswa, Kata ya Zanzui, umeshakamilika na mradi ule unategemewa kusambaza maji katika vijiji kumi, Maswa Mashariki vijiji vitano na Maswa Magharibi vijiji vitano.

Ni lini sasa maji yale yatasambazwa ili wananchi wa Maswa na akinamama wa Maswa wapumzike na adha ya maji? (Makofi)

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli anatosha mpaka chenji inabaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa namna nyingine ambayo nataka kusema wananchi wa Maswa changamoto kubwa sana lilikuwa ni chujio kwamba wanapata maji, lakini sio safi na salama na yenye ubora. Kwa hiyo, tumepata fedha, chujio lile tumelikamilisha kazi iliyobaki na ninatoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa pale na tumekwishamthibitisha, kipimo chake cha kwanza ni kuhakikisha maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaeleza kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara tutampatia fedha kuhakikisha kwamba anatimiza majukumu yake na wananchi wanapata huduma ya maji. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Primary Question

MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Mradi wa Maji Ruduga – Mawindi ili kuwatua ndoo kichwani akina mama wa Mbarali?

Supplementary Question 4

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; kwa kuwa Jimbo la Kibamba sasa changamoto yake kubwa ni usambazaji wa mabomba tu katika maeneo mbalimbali. Je, Serikali sasa iko tayari kutoa kauli au maelekezo ya utoaji wa mabomba yale ili wananchi wa maeneo mengi wapate maji safi na salama?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kidhati ya moyo nikupongeze sana kaka yangu Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu Mtemvu. Moja katika bajeti yako umeonesha masikitiko yako eneo ambalo halina maji na tumekwishakubaliana na commitment yangu mimi baada ya Bunge tunakwenda Kibamba tunakwenda kumaliza kabisa tatizo la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na tumeshatoa maelekezo mahususi kwa DAWASA, wamefanikiwa maeneo mengi sana, walipe kipaumbele Jimbo la Kibamba katika kuhakikisha kwamba, tunaenda kumaliza kabisa tatizo la maji. Ahsante sana. (Makofi)