Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Jumaa Hamidu Aweso
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Pangani
Primary Question
MHE. JUMAA H. AWESO aliuliza:- Jimbo la Pangani linakabiliwa na tatizo sugu la maji hususan katika Kata za Mkalamo, Masaika, Mikunguni, Mkaja, Mwera na Bushiri. Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hili ambalo limesababisha kuzorotesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa kata hizo?
Supplementary Question 1
pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini pamoja na changamoto kubwa ya maji katika kata nilizoainisha lakini tumekuwa na tatizo sugu katika suala la maji katika Mji wetu Mkuu wa Pangani, na mpaka sasa nioneshe masikitiko yangu kutokana na changamoto hii ya maji, fedha zilizokuwa zimeidhinishwa katika bajeti iliyopita kiasi cha shilingi milioni 200 mpaka sasa nazungumza hazijafika.
Je, ni nini commitment ya Waziri kuhakikisha kwamba fedha zile zilizoainishwa kwa ajili ya kwenda kutatua tatizo la maji mjini, na ni lini zinapelekwa na wakati bajeti inafikia ukingoni? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili; Wilaya yetu ya Pangani imejaliwa kuwa na Mto Pangani ambao unatiririsha maji baharini. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba inautumia mto huu kwa kuanzisha mradi mkubwa wa maji ambao utaweza kutatua suala zima la maji kwa Wilaya yetu ya Pangani na Wilaya za jirani kwa maana ya Muheza na Tanga Mjini?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kilio cha Mheshimiwa Mbunge ni kweli kilio sahihi, kwa reference ni kwamba miaka miwili iliyopita nilienda na nililala mpaka katika ule Mji wa Mwera pale. Nimeweza kubaini tatizo la maji katika Mji wa Pangani, lakini kama hiyo haitoshi nikaenda mpaka Redio Pangani nikawa nina kipindi cha moja kwa moja cha kuongea na maswali ya wananchi pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru wananchi wa Pangani wengi walipiga simu kusikia Mbunge wa Pangani yuko eneo lile na miongoni mwa shida ambayo waliizungumza ilikuwa ni shida ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ni kweli, ule Mradi wa Pangani nadhani ulianzishwa takribani pale Pangani Mjini kati ya mwaka 1963 au 1973, miundombinu yake kweli kwa idadi ya watu waliokuwa wanahudumiwa kipindi hicho kwanza imechakaa, lakini population kipindi hicho ilikuwa ni ndogo. Ndio maana katika Ofisi ya Mheshimiwa Mbunge harakati zilizofanyika ni kwamba Ofisi ya Mkurugenzi walipeleka maombi maalum katika Wizara ya Maji, walitaka shilingi milioni 400 ikiwezekana kwamba waweze kupata bajeti ya kukarabati miundombinu ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, walipata awamu ya kwanza shilingi milioni 200 kutoka Wizara ya Maji, lakini hata hivyo wanasubiria kwamba kwa sababu ule mradi wa milioni 200 umepelekwa pale Pangani Mashariki, lakini kuna maeneo mengine bado ukarabati haujafanyika ikiwemo sambamba na ukarabati wa tenki. Kwa hiyo, ni kwamba Serikali imesikia hiki kilio na inalifanyia kazi ndio maana nimezungumza haya yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo ni program kubwa ni kweli, haiwezekani hata kidogo eneo la Pangani ambalo Mto Pangani ni mkubwa unapoteza maji baharini, halafu wananchi wa Pangani hawapati maji! Na hili ndio maana leo hii niliongea na Mkurugenzi wa Pangani pale na ameniambia sasahivi yuko Mahakamani kuna kesi za uchaguzi zinazoendelea; nikamwambia, nini programu yake anayotaka kuhakikisha Mto Pangani unatumika?
Mheshimiwa Naibu Spika, amekiri kwamba, sasahivi wanafanya utafiti na inaonekena gharama ya shilingi bilioni 10 nadhani itahitajika kwenye mradi ule, lakini bado iko katika suala zima la tathmini, lakini hili niseme ni nini! Ni kwamba Wizara ya Maji nayo ilisema kwamba sasa wataenda kutumia kama Serikali tutaenda kutumia vyanzo vyote vinavyowezesha kutumia maji. Imani yangu ni kwamba Mto Pangani tunaweza kuutumia katika sekta ya maji hasa Programu ya Awamu ya Pili ya Maji ambayo tunaenda kuibua suala zima la kutatua tatizo la maji kwa wananchi wetu wa Tanzania.
Name
Stephen Hillary Ngonyani
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Primary Question
MHE. JUMAA H. AWESO aliuliza:- Jimbo la Pangani linakabiliwa na tatizo sugu la maji hususan katika Kata za Mkalamo, Masaika, Mikunguni, Mkaja, Mwera na Bushiri. Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hili ambalo limesababisha kuzorotesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa kata hizo?
Supplementary Question 2
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Katika Jimbo la Korogwe Vijijini kulitokea kampuni ambayo sio mali ya Serikali, UNDP, ilinipa milioni 243 nikachimba visima tisa. Baada ya kuchimba visima hivyo walikuja wataalamu wa Serikali wakasema sehemu hizi tukichimba tutapata maji safi, lakini cha kusikitisha baada ya kuchimbwa maji yale yalivyokwenda Serikalini kuleta majibu nikaambiwa maji yale hayafai kutumika kwa binadamu na hela tayari zimeshatumika shilingi milioni 243.
Je, hii hasara ambayo wameipata wananchi wa Jimbo la Korogwe Vijijini italipwa na nani?
Name
Dr. Selemani Said Jafo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kisarawe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani Naibu Waziri Wizara ya Maji siku ile kama mtaalam wa maji, amezungumza hapa kwamba, mara nyingi sana taaluma zetu hizi za maji wakati mwingine unaweza kufanya survey, lakini hujui kiwango gani cha maji utakipata! Lakini sio kiwango cha maji, hata ule ubora wa maji wa kiasi gani!
Mheshimiwa Naibu Spika, na ndio maana ukiangalia, kwa mfano katikati tulikuwa na mradi kutoka China, tulipata visima kwa Wilaya ya Kilosa na Wilaya ya Kisarawe. Katika visima vilivyochimbwa ikaonekana kwamba kiwango cha madini ya chuma yako mengi zaidi ya madini ya aina mbalimbali maji yale hayafai kunywa! Halikadhalika katika eneo lako, kwanza nikupongeze kwa sababu umefanya initiative ya kupata watu ambao wanakusaidia kuchimba maji, maji yamechimbwa, lakini ubora wa maji bado hauko sawasawa! Naomba nikwambie itakuwa ni jambo la ajabu kusema kwamba gharama ile italipwa na nani!
Mheshimiwa Naibu Spika, itakuwa ni jambo la ajabu ni kwa sababu, maji yamepatikana, lakini mtaalamu wa maji hata anavyofanya survey hawezi kusema maji haya nikiyatoa hapa yatakuwa matamu au ya chumvi! Jambo hilo bado ni gumu na wataalam wote wanakiri hivyo. Kwa hiyo, nini cha kufanya; cha kufanya ni kwamba kwa sababu visima vile maji hayajawa na ubora uliokusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la Serikali sasa tuweke mipango mipana jinsi gani tutawasaida wananchi wa Jimbo lako waweze kupata huduma huduma ya maji kama sera ya maji inavyoelekeza hivi sasa kwamba wananchi waweze kupata maji. Mbunge nakujua kama ni mpiganaji na hili litawezekana katika maeneo yetu.
Name
Dr. Joseph Kizito Mhagama
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Madaba
Primary Question
MHE. JUMAA H. AWESO aliuliza:- Jimbo la Pangani linakabiliwa na tatizo sugu la maji hususan katika Kata za Mkalamo, Masaika, Mikunguni, Mkaja, Mwera na Bushiri. Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hili ambalo limesababisha kuzorotesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa kata hizo?
Supplementary Question 3
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa vile suala hili la maji ni suala la kisera; na kwa vile miraji mingi ya maji inayotekelezwa kwa kupitia Halmashauri za Wilaya inakwama; na kwa vile ni Wizara inayohusika na maji ndiyo inayopeleka miradi hii isimamiwe na Halmashauri za Wilaya; na Halmashauri za Wilaya hizi hazitekelezi majukumu yake vizuri na kukwamisha Wizara kufikia yale malengo waliyojiwekea. Na kwa vile Wilaya ya Songea katika kijiji cha Maweso na Lilondo, miradi hiyo imekwama kwa sababu tu certificate za wakandarasi hazijafikia Wizara mpaka leo;
Ni hatua gani Wizara ya TAMISEMI inachukua pale ambapo miradi inakwamishwa na Halmashauri, ni miradi ambayo kimsingi inatoka kwenye Wizara zingine? Ahsante.
Name
Eng. Gerson Hosea Lwenge
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa kujibu vizuri sana maswali aliyoulizwa ya nyongeza kwenye sekta ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu spika, tumetoa maelekezo kwenye Halmshauri wakiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu ya Sekta ya Maji kwamba kwa sasa hivi tunapeleka fedha baada ya kuletwa certificate. Sasa Mheshimiwa Mbunge kama unayo certificate ya kazi ambayo imeshafanyika naomba uniletee hata leo, tutakwenda kulipa. Kwa sababu wanasema certificate zipo lakini tumeangalia uhalisia kule Wizarani certificate hazipo, sasa kama ipo certificate na kazi imefanyika tunakwenda kulipa ili kusudi wakandarasi warudi wafanye kazi miradi ya maji iweze kukamilika.
Name
George Malima Lubeleje
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpwapwa
Primary Question
MHE. JUMAA H. AWESO aliuliza:- Jimbo la Pangani linakabiliwa na tatizo sugu la maji hususan katika Kata za Mkalamo, Masaika, Mikunguni, Mkaja, Mwera na Bushiri. Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hili ambalo limesababisha kuzorotesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa kata hizo?
Supplementary Question 4
MHE. GEORGE M. LUBELEJE:Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali moja la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ya Maji.
Kwa kuwa tatizo la maji ni kubwa sana karibu nchi nzima na Majimbo matatu haya ya Kibakwe, Mpwapwa na Kongwa ni tatizo kubwa. Kuna visima ambavyo vilianzishwa kuchimbwa vya Benki ya Dunia mpaka sasa havijakamilika. Mpaka sasa hivi Mjini Kongwa, dumu moja la maji wananchi wananunua shilingi 1,000;
Je, Mheshimiwa Waziri, utakuwa tayari kutembelea maeneo hayo kuhakikisha kwamba miradi hii ya Benki ya Dunia ambayo haijakamika sasa ikamilishwe?
Name
Eng. Gerson Hosea Lwenge
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo maeneo ambayo tunayo hii miradi ya vijiji kumi ambayo haijakamilika na tumesema tu katika Awamu hii ya Pili kwanza tunakaribisha miradi ambayo imeshaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo suala la kutembelea kuangalia hiyo miradi ambayo inasuasua, kwa sababu kusuasua inawezekana ikawa tatizo ni mkandarasi ambaye amewekwa. Sasa kama itaonekana ni tatizo la mkandarasi tutachukua hatua kulingana na mkataba wenyewe.
Kwa hiyo, kama tatizo ni fedha nimeshasema fedha sasa hivi Awamu ya Tano imeshajipanga vizuri, fedha zipo za kuweza kukamilisha miradi hii ambayo tayari iweze kupata huduma ya maji kwa wananchi wetu.