Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Cecil David Mwambe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE K.n.y. MHE. MWANTUM M. ZODO aliuliza:- Kada ya Elimu inakadiriwa kuwa na upungufu wa walimu takribani 60,000. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kukabiliana na changamoto hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali haioni umuhimu sasa wa kupeleka majina ya waajiriwa moja kwa moja kwa Wakurugenzi ili Wakurugenzi wawapangie vituo vya kufanya kazi badala ya kupangwa moja kwa moja kutoka TAMISEMI?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wakurugenzi ndio wanaofahamu idadi ya upungufu wa walimu, ukiangalia Jimbo la Ndanda Wilaya ya Masasi kwa mfano, sasa je, Serikali haioni haja ya kuwapa nafasi Wakurugenzi kupendekeza nafasi za ajira kutokana na watu wanaostaafu au kufariki kwenye maeneo yao? (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa tumekuwa na taratibu tofauti hususani kwa walimu ambao wamekuwa wakiajiriwa kuwapeleka katika maeneo yao husika na moja utaratibu ni kwamba sisi tumekuwa tukiwatuma katika halmashauri husika katika vituo ambavyo wao wenyewe wamekuwa wakiomba. Kwa hiyo, wao wanaoomba zile ajira huwa wanaainisha maeneo gani wanataka kwenda kufanyia kazi na sisi tumekuwa tukitekeleza kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili kuwapa mamlaka Wakurugenzi ni taratibu za kiutumishi na Serikali inafanya kazi baada ya kupata kibali kutoka Ofisi ya Rais (Utumishi) ambao wanatuletea namna, vigezo na sababu mbalimbali za mtu kuajiriwa. Kwa hiyo, kama kuna mapendekezo hayo ya kutaka kubadilisha ni Bunge lako Tukufu ndio lenye mamlaka hiyo, ahsante sana.
Name
Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Longido
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE K.n.y. MHE. MWANTUM M. ZODO aliuliza:- Kada ya Elimu inakadiriwa kuwa na upungufu wa walimu takribani 60,000. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kukabiliana na changamoto hiyo?
Supplementary Question 2
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna uhaba mkubwa wa walimu nchini na Serikali imekuwa inawaajiri kwa awamu kidogo kidogo na bado pengo ni kubwa, imebidi shule nyingi zitumie walimu wa kujitolea na ajira zinapotangazwa unakuta mwalimu aliyejitolea amepangiwa kwenda shule mbali na ile aliyojitolea.
Je, Serikali haioni sasa ni muhimu wale walimu wote waliojitolea na walimu wale wakuu wamewapendekeza kwamba ikitokea ajira waajiriwe palepale walipojitolea?
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kiruswa, Mbunge wa Longido kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tungetamani walimu wote ambao wanajitolea katika maeneo yao husika wapangiwe maeneo hayo lakini bahati mbaya inatokana na ule uhaba ambao unatokana. Kwa mfano kama sasa hivi tuliomba taarifa za walimu wote wanaojitolea mashuleni tukaletewa nafasi walimu wanaojitolea 70,000 na nafasi ambazo zimetangazwa na Serikali ni 6,000 kwa hiyo nafikiri unaweza kuona ni changamoto kiasi gani tunapitia katika kukabiliana na janga hili.
Mheshimiwa Spika, Serikali bado ina nia njema kuhakikisha kwamba itaendelea kuajiri walimu kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha na bajeti ambayo tutakuwa tunajipangia na kila mwaka tutakuwa tunaendelea kufanya hivyo walau kuhakikisha kwamba tuna accommodate hili ambalo Mheshimiwa Mbunge amelieleza. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Kiruswa kwa swali lake la nyongeza kwa nini tusiajiri walimu ambao wanajitolea. Ni kweli kigezo kikubwa ambacho tutakitumia katika kuangalia wenye vigezo ni wale ambao wanajitolea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka kukiri sasa hivi yapo malalamiko hata hao wanaojitolea kuna wengine wameleta barua za fake za kusema kwamba wanajitolea wakati hawajitolei. Kwa hiyo, jana tumepokea pia maelekezo yako suala hili ni tete, nafasi ni 6,949 mpaka juzi walioomba wameshafika 89,958. Kwa hiyo, suala hili naomba utuamini Serikali tutatenda haki; hata hao wanaojitolea tutawachambua kama ni kweli wanajitolea.
Mheshimiwa Spika, pia kuna walimu wamemaliza 2012, 2013, 2014, 2015 hawajaajiriwa kwa hiyo upo pia mtazamo ndani ya Wizara labda tuangalie hawa ambao wamemaliza siku nyingi wanajitolea na hawajapata ajira kwa sababu muda wao wa kuajiriwa pia unapungua kwa sababu lazima waajiriwe kabla ya miaka 45. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana uiamini Serikali suala hili ni tete, walioomba wenye vigezo ni wengi, nafasi ni chache lakini tutatenda haki kama ulivyoelekeza bila kubagua dini, kabila, jinsia wala upendeleo wa nafasi yoyote. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
Name
Aida Joseph Khenani
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Nkasi Kaskazini
Primary Question
MHE. CECIL D. MWAMBE K.n.y. MHE. MWANTUM M. ZODO aliuliza:- Kada ya Elimu inakadiriwa kuwa na upungufu wa walimu takribani 60,000. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka kukabiliana na changamoto hiyo?
Supplementary Question 3
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, pamoja na jitihada ambazo Serikali inafanya juu ya kuajiri walimu lakini kuna changamoto kubwa kwenye maeneo ya vijijini kukosa walimu wa kike.
Ningependa kujua mkakati wa ziada wa Serikali inafikiri nini juu kuondoa hizo changamoto ambazo watoto wa kike wanakutana nazo shuleni.
Name
Ummy Ally Mwalimu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Tanga Mjini
Answer
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni swali zuri na mimi kama mama tunahitaji pia kuwa na walimu wanawake katika shule zetu za msingi na sekondari ni moja ya kigezo tutaki- take into consideration katika kutoa ajira mpya lakini pia kufanya reallocation ya walimu katika shule zetu za msingi na sekondari hususani za vijijini.