Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hassan Selemani Kaunje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lindi Mjini

Primary Question

MHE. HASSAN S. KAUNJE aliuliza:- Jimbo la Lindi Mjini lina eneo la Bahari ya Hindi lenye urefu wa kilometa 112, lakini eneo hilo halina mchango wowote wa maana kwenye pato la Taifa na Manispaa ya Lindi:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza eneo la bahari katika Manispaa ya Lindi?

Supplementary Question 1

MHE. HASSAN S. KAUNJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wa eneo hili la bahari unaendana na shughuli za wavuvi na Lindi kuna wavuvi. Nilipenda niulize nini msimamo wa Serikali kuwasaidia wavuvi wa Lindi kuhusiana na kodi mbalimbali ambazo ni kero kwao? Vilevile wana mpango gani wa kuwasaidia zana za uvuvi ili waweze kuleza pato katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kaunje, Mbunge wa Lindi Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli watu wa Lindi shughuli zao kubwa sana hasa wale wa ukanda ni uvuvi na siyo watu wa Lindi peke yake isipokuwa hata Kanda ya Ziwa na maeneo mbalimbali ambao wanaguswa na vyanzo vya maji. Wengi wao wana tatizo kubwa za tozo za kodi za aina mbalimbali ambazo zinawakabili kiasi kwamba shughuli zao zinakwama. Ndiyo maana katika nyakati mbalimbali hapa nimekuwa niki-refer aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Kilimo aliyezungumzia suala la kupitia hizi kodi mbalimbali, lengo kubwa ni kupunguza hizi tozo mwisho wa siku wananchi wa kawaida ambao wavuvi wa Lindi waweze kupata fursa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Mbunge tuwe na subira, Serikali inafanya mchakato huu mpana katika suala zima la kilimo, mifugo na uvuvi ambapo inaonekana kwamba mvuvi mwingine akitoka halmashauri moja kwenda halmashauri nyingine anatakiwa alipe kodi. Kwa hiyo, Serikali inaangalia haya yote kwa kina lengo kubwa ni kuliboresha eneo hili mwisho wa siku wananchi wa eneo lako la Lindi wataweza kupata fursa sana katika suala zima la shughuli zao za uvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo la pili la jinsi gani ya kuboresha suala zima la uvuvi, niki-refer tena katika Wizara ya Kilimo na Mifugo, wakati waki-submit hapa bajeti yao mwaka huu, walizungumzia wazi mkakati wao mpana wa kuwasaidia wavuvi hasa wale wa kandokando ya bahari na katika maziwa kwa kuangalia jinsi gani watapewa nyenzo ambazo zitasaidia katika suala zima la uvuvi. Hata hivyo, tulipopitisha bajeti ya TAMISEMI tulisema kuna zile asilimia tano za vijana na akina mama, katika maeneo mengine hasa ya uvuvi, halmashauri katika mipango yao iweze kuona jinsi gani ya kutumia five percent ya vijana na akina mama kuwasaidia wavuvi wa maeneo hayo ili waweze kushiriki katika shughuli za kujenga uchumi wa nchi yao.