Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Kilumbe Shabani Ng'enda
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Mjini
Primary Question
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA K.n.y. MHE. ASSA N. MAKANIKA aliuliza:- Je, ni lini Serikali itawasaidia wananchi wa Kigoma ambao wamekuwa wakikamatwa mara kwa mara kwa kuitwa wakimbizi nchini mwao?
Supplementary Question 1
MHE. KILUMBE S. NG’ENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na nitaomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwanza ni ukweli kwamba tunajua umuhimu wa kazi ya Idara ya Uhamiaji katika kusimamia masuala aliyoyasema Mheshimiwa Waziri ya ungiaji wa wageni ukaaji wao. Hata hivyo, kiwango cha usumbufu wa wananchi unaotokana na doria za uhamiaji kimepita kiasi ambacho sisi tunakifahamu katika historia ya Mkoa wetu wa Kigoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka Mheshimiwa Waziri aniambie kuna jambo lipi jipya ambalo limejitokeza linalosababisha kwa sasa kuwe na misako inayosumbua hata raia halali waliokaa katika mkoa wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili; msingi wa kukua kwa tatizo hili ni kuchelewa kwa Wizara yake kutoa vitambulisho vya NIDA kwa wananchi halali wa Mkoa wa Kigoma, jambo ambalo lingekuwa limekamilishwa, haya yote yasingekuwepo. Anieleze ni lini Serikali itakamilisha kazi hii ya kutoa vitambulisho vya NIDA ili kuondokana na usumbufu huu; na kama inawezekana misako hiyo isimame mpaka hapo mtakapokamilisha vitambulisho vya NIDA? (Makofi)
Name
George Boniface Simbachawene
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibakwe
Answer
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kiwango cha usumbufu katika kusimamia Sheria ya Uhamiaji, Kifungu cha 12 kama ilivyorejewa mwaka 2016 ambapo Jeshi la Uhamiaji limepewa jukumu la kufanya misako, doria na hata ikibidi kufanya upekuzi ili kubaini nani ni raia na nani sio raia; zoezi hili kama tulivyojibu katika jibu letu la msingi, linafanyika kwa nchi nzima. Usumbufu huu unatokana na mkoa ulivyo na mipaka na majirani zetu ambapo mara nyingi kumekuwa kuna shida katika nchi zao na kwa hiyo wana msukumo mkubwa sana wa kuja katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kusema kweli kwa muda wa miezi mitatu tumekamata wahamiaji haramu zaidi ya 1,000. Kiwango hiki ni kikubwa na siyo rahisi tusifanye doria, lakini tunafanya hivyo kwa mikoa yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anauliza vitambulisho vya NIDA vingetotewa basi usumbufu usingekuwepo. Ni kweli, lakini nataka niseme, kupewa kitambulisho cha NIDA cha uraia wa Tanzania siyo mwarobaini kwamba wewe sasa huwezi ukaulizwa kuhusu uhalisia na uhalali wa uraia wako. Sheria hizi ni mbili tofauti; kuna Sheria ya Uraia, Sheria ya Uingiaji Nchini na Sheria ya Vitambulisho vya Taifa na zote hizi zinashughulikia mambo mawili tofauti. Vitambulisho hivi hata wakazi wasio raia wanapewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna madaraja tofauti tofauti ya kutoa vitambulisho. Siyo kwamba ukipewa kitaambulisho hiki, basi wewe hutaulizwa tena. Tutaulizwa, hata mimi naweza nikaulizwa uraia wangu hata kama nina kitambulisho na hata kama natoka Dodoma; nitaulizwa uraia wangu na uhalisia endapo utajitokeza wasiwasi wowote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ndiyo majibu yetu ya Serikali na tunaomba Mkoa wa Kigoma watuelewe hatufanyi kwa Mkoa wa Kigoma peke yake, tunafanya kwa mikoa yote. Hivi sasa kuna oparesheni imeanza tarehe mosi itaisha tarehe 15 ya mwezi huu kwa mikoa yote ya Tanzania. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved