Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Primary Question

MHE. DENNIS L. LONDO aliuliza:- Je, ni lini upanuzi wa Kiwanda cha Sukari cha Ilovo utakamilika, na kwa kiasi gani upanuzi huo utaenda sambamba na kuondoa kero ya Mizani na Vipimo vya Sucrose kwa wakulima wa Miwa?

Supplementary Question 1

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri ambayo yanaonyesha jitihada ya wazi ya Serikali kutatua kero ya miwa kwa kulima miwa katika Bonde la Kilombero. Lakini pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri huduma zinaendelea. Kwa mfano, hivi tunavyozungumza, Vyama vya Ushirika vya RCG AMCOS ambavyo vilikuwa na DRD7 mwaka jana, wamepunguziwa kwenda 3. Chama cha Kitete AMCOS ambacho kilikuwa na DRD5 mwaka jana, mwaka huu imepewa 3. Chama cha KIDODI AMCOS ambacho kilikuwa na DRD4 mwaka huu kimepewa 2. Chama cha Mbwade, Msindazi na MIWA AMCOS vyote vimepunguziwa DRD, ambayo inapelekea kupunguza kiasi cha miwa ambacho kinapeleka Kiwandani.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana, tulilaza miwa tani 400,000. Mwaka huu wametupunguzia uwezo maana yake nini, maana yake wanajiandaa kuhujumu wakulima wa miwa kwa zaidi ya tani 400,000 ambazo tumelaza mwaka jana. Je, nini tamko la Serikali kwa vitendo hivi ambavyo vinafanywa na Kiwanda hiki? Lakini nini tamko la Serikali kwa makaburu hawa weusi ambao ni watanzania wenzetu wanaowasaidia wawekezaji kuumiza wakulima wetu? Naomba tamko la Serikali. (Makofi)

Name

Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Answer

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwanza, Serikali inataka wawekezaji wote nchini, kufanya uwekezaji na shughuli zao zote kwa kuzingatia sheria. Na kama kuna hujuma kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge, ni kinyume cha sheria na tutafuatilia.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili, suluhu ya kudumu ya miwa ya wakulima wa Kilombero ni upanuzi wa Kiwanda hiki ambao nimeeleza. Kwa sababu, tukishapanua wakulima watauza zaidi miwa yao kwa sababu, kiwanda kitakuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya mara tatu ya miwa ambayo wanachukua sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho, kama nilivyoeleza wakati wa bajeti yangu, mwaka huu wenzetu wa SIDO tumewaelekeza na wameshakubali kufanyia kazi. Tutakuwa na mitambo midogo ya kuchakata miwa ya wakulima katika ngazi ya chini.

Kwa hiyo, kutakuwa na wajasiriamali ambao wanaweza wakauza miwa kwa wajasiriamali wadogo wa kuchakata miwa hiyo. Kwa sasa hivi tuna viwanda vikubwa peke yake, sasa tumeona kwamba kuna haja ya kuwa na wajasiamali wadogo wadogo, watasaidia sana kuchukua miwa hii ya wakulima wetu.