Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:- Halmasauri ya Wilaya ya Lushoto ina upungufu wa walimu wa shule za msingi takribani 1,270 kwa mujibu wa ikama: - Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka walimu katika Halmashauri hiyo?
Supplementary Question 1
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa sasa Serikali ipo katika mchakato wa ajira hizi mpya ambazo amezitaja 6,979 hivi na sisi upungufu wetu ni walimu 1,270.
Je, haoni sasa kuna umuhimu angalau Halmashauri kama ya Lushoto ikapewa kipaumbele angalau kwa kusogeza hata kupata walimu japo 200?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa wapo walimu ambao asili yao ni Lushoto na Tanga kwa ujumla na wapo katika maeneo mbalimbali ya nchi hii na hawa wapo tayari kurudi Lushoto kuungana na wananchi wa Lushoto katika kutoa huduma hii ya elimu lakini changamoto za uhamisho ndio zinazowakwamisha.
Je, Serikali iko tayari kushirikiana na mimi kuwabaini wale wote ambao wapo tayari kurudi Lushoto ili kwenda kusaidia jukumu hili na kuondoa huu uhaba mkubwa wa walimu katika Halmashauri yetu?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS . TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi ni kweli kwamba katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, lakini pia katika Jimbo la Mlalo kuna upungufu wa watumishi kwa maana ya walimu na Serikali kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi imeendelea kuwaajiri kwa awamu walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto. Naomba nimhakikishie kwamba katika ajira hizi 6,900 ambazo zinakwenda kutolewa hivi sasa ambapo tayari taratibu za kuwa-shortlist na kuwapata walimu hao zinaendelea, tutakwenda kuhakikisha tunampa kipaumbele cha hali ya juu sana Mheshimiwa Shangazi na Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto kwa ujumla wake. Kimsingi namhakikishia kwamba tutaendelea kulifanyia kazi kwa karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; walimu wenye asili ya Lushoto ambao wanapenda kurudi kufanya kazi katika Halmashauri hiyo, utaratibu wa Serikali uko wazi na walimu na watumishi wote kote nchini wanaruhusiwa kufanya kazi sehemu yoyote, lakini wale ambao wana sababu za msingi za kuomba kurudi katika Halmashauri yoyote ile ikiwemo Lushoto bila kujali wanatokea ama hawatokei Lushoto wanaruhusiwa kufuata taratibu za Serikali za kuomba uhamisho na sisi kama Serikali tuna vigezo ambavyo tutavitazama na kuona walimu wale wanapata vibali vya kuhama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie kwamba kama wapo wanaohitaji tunawakaribisha, lakini kwa kufuata vigezo na taratibu zile za Serikali, nakushukuru. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved