Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Stanslaus Haroon Nyongo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Maswa Mashariki
Primary Question
MHE. STANSLAUS H. NYONGO K.n.y. MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake na vijana katika Halmashauri wanapewa mikopo ya asilimia tano?
Supplementary Question 1
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza fedha hizi zimekuwa zikitolewa na Halmashauri, lakini hatuoni ni namna gani zinavyorudishwa ili kuweza kukopeshwa watu wengine; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaweka mkakati thabiti wa kuhakikisha kwamba hizo fedha zinavyorudi basi wapewe na watu wengine ili waweze kupatiwa mikopo hiyo na kuweza kujiendeleza katika biashara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kutoka kwenye asilimia nne kwa wanawake, nne kwa vijana na mbili kwa walemavu kuongeza asilimia walau ziwe 15 ili kila kundi lipate asilimia tano tano? Ahsante sana.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba fedha hizi asilimia kumi ambazo zimekuwa zinatolewa kwa vikundi vya wajasiriamali katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa zimewekwa kwa mujibu wa sheria na kKanuni ili ziwe ni fedha ambazo zinazunguka kwa maana ya revolving fund. Kwa maana kila vikundi ambavyo vinakopeshwa vinapaswa kutekeleza shughuli hizo za ujasiriamali na kurejesha fedha zile ambazo zilikopwa bila riba yoyote ili ziweze kutumika pia kuwakopesha vikundi vingine na hatimaye kuendelea kuwajengea uchumi mzuri wana vikundi katika vikundi hivi vya ujasiriamali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto ya urejeshaji wa fedha hizi kwenye baadhi ya vikundi vya ujasiriamali vinavyokopeshwa. Na sheria ya sasa imeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba tunakwenda kufungua akaunti maalum kwa ajili ya fedha hizi za mikopo ya asilimia kumi na kuhakikisha kila kikundi cha ujasiriamali kitarejesha fedha hizo na zionekane zinarejeshwa na kukopeshwa kwenye vikundi vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwaelekeza Wakurugenzi wote wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha wanalisimamia kwa karibu sana suala la mikopo na marejesho na sisi kama Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Serikali kwa ujumla tutakwenda kufanya kaguzi kuona fedha zilizokopeshwa zinarejeshwa na zinaendelea kukopeshwa katika vikundi vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; tumeweka asilimia kumi kutokana na mazingira ya fedha za mapato ya ndani kuwa yana majukumu mengi sana; sote tunafahamu asilimia 40 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, asilimia 60 kwa Halmashauri za Mijini kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini pia kuna shughuli zingine nyingi. Wazo hili ni zuri la kufikiria kuongeza asilimia 15 lakini tutakwenda kulifanyia tathmini na kuona kama linawezekana kutekelezwa lakini kwa sasa tunaendelea na asilimia kumi kwa sababu tumeangalia vigezo mbalimbali ili kuziwezesha Halmashauri kuendelea na shughuli zake. Nakushukuru sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved