Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Sylivia Francis Sigula
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. SYLIVIA F. SIGULA aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wavuvi wa Ziwa Tanganyika wavue kisasa ili kupata kipato zaidi na kutoa ajira kwa vijana?
Supplementary Question 1
MHE. SYLIVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa majibu mazuri ya Wizara lakini nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali imerahisisha upatikanaji wa vifaa, lakini pia tumeona vijana wengi wamejitokeza na wamehamasika kuingia katika sekta ya uvuvi na wengi wameunda vikundi, lakini hawajapatiwa mafunzo, lakini pia hawana vifaa vya kisasa vya kuvulia.
Je, ni lini kauli ya Serikali kwa vijana ambao wamejiunga kwenye vikundi na wamekidhi vigezo lakini awajapatiwa vifaa vya kuvulia na mikopo?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili tunaona kabisa kwenye majibu ya msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri anasema kwamba mahitaji ya wavuvi wa Tanzania na yaliyopitishwa ikiwa ni 2.6 bilion lakini hela iliyotolewa ni milioni 500 plus ambayo hii ni chini ya asilimia 25.
Je, ni nini mpango wa Serikali katika kuhakikisha tunaongeza kipato hiki hili wavuvi wakaweze kupata tija na uvuvi uweze kuwa na tija kwa nchi hii kwa kuongeza ajira kwa vijana na kipato cha Taifa? (Makofi)
Name
Abdallah Hamis Ulega
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkuranga
Answer
NAIBU WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sylivia kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uniruhusu pia nimpongeze Mheshimiwa Sylivia kwa umahiri na uhodari wake wa kufuatilia masuala ya wavuvi hasa vijana wa Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya mafunzo na uwezeshaji wa makundi haya ya vijana yaliyokwisha kuanzishwa, tunacho chuo chetu cha uvuvi kilichopo pale Kigoma Mjini kwa maana ya Kibirizi, nataka nimhakikishe ya kwamba tutahakikisha chuo kile kinayafikia makundi yote haya, namuomba Mheshimiwa Mbunge aniwasilishie vikundi vile vya Ziwa Tanganyika kimoja baada ya kingine tutakifia kwa mafunzo na tutakifikia katika kukiwezesha hasa kupata mashine ya boti, hilo ni jambo la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni juu ya kuongeza mikopo kwa tasnia hii ya uvuvi. Serikali hususani Wizara ya Mifugo na Uvuvi tulifanya jitihada ya makusudi ya kuanzisha Dawati la Sekta Binafsi na sasa limefanya kazi kubwa kabla ya kuanzishwa kwa Dawati la Sekta Binafsi Idara ya Uvuvi ilipata mikopo sawa na sifuri kwa wavuvi wadogo na baada ya kuanzishwa tumeipandisha mpaka kufikia milioni 560.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wanawakilisha wavuvi katika Bunge hili Tukufu kwamba mkakati wetu ni kuimarisha zaidi Dawati la Sekta Binafsi kimkakati, kwa ajili ya kuweza kuiwezesha sekta hii iweze kupata pesa zaidi, maandiko ya vikundi hivi vya wavuvi tutayapitia na kuyawezesha yaweze kuweza kushawishi benki kuweka pesa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini na mkakati wetu wa pili ni bima ya wavuvu; pamekuwa na mgogoro wa muda mrefu juu ya kuweza kupata bima kwa ajili ya wavuvi na wafungaji. Dawati la Sekta Binafsi tumefika mahala kuzuri hivi sasa Shirika letu la Bima la Taifa linakwenda kutupelekea kupata bima ya wavuvi na bima ya mifugo ili sasa mabenki yaweze kuwa na appetite ya kutoa pesa zaidi, ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved