Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Martha Festo Mariki
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha zoezi la utoaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi kwa kuwa kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa vitambulisho hivyo?
Supplementary Question 1
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa vigezo vinavyowakwamisha vijana wetu wa Kitanzania hususan waliopo katika mikoa inayopakana na nchi jirani ikiwemo Mikoa ya Katavi, Kigoma na mingineyo ni pamoja na ucheleweshwaji na upatikanaji wa namba za NIDA.
Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kutokutumia kigezo hiki wakati vijana wanapokuwa wanatumia ajira ili kuwawezesha vijana wetu waweze kupata ajira kwa kuwa mchakato huo bado haujakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili; ni kwanini sasa mfumo wa NIDA usiunganishwe na mfumo wa RITA wa vyeti vya kuzaliwa ili kuwawezesha Watanzania pale tu mtoto anapozaliwa aweze kupata cheti kimoja kinachounganisha kuonyesha kwamba huyu ni raia kwa kuzaliwa? Ahsante sana.
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martha Festo Mariki, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nichukue fursa hii nimpongeze sana Mheshimiwa kwa kuwa umefika wakati ameona umuhimu wa wananchi hasa wa mkoa wake kufanyiwa haraka katika kupata vitambulisho huku akiwa anajua kwamba vitambulisho kwa sasa NIDA ndiyo kila kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba sasa nianze kujibu swali la kwanza, kwamba, je, Serikali sasa haioni haja ya kuondosha hiki kigezo cha NIDA ili sasa mambo mengine yaweze kuenda yakiwemo ya vijana kuweza kupata ajira?
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba tumeamua kuweka kigezo hiki ili kuweza kuwajua ni nani wenye sifa na nani wasiokuwa na sifa; na tumeamua kukiweka kigezo hiki ili kuona kwamba nani ambao wana Utanzania na nani ambao hawana Utanzania. Sasa kwa kusema moja kwa moja kigezo hiki kukitoa basi ni jambo ambalo linahitaji procedure, twende tukakae na watu wa utumishi na taasisi nyingine. Nimwambie tu Mheshimiwa kwamba jambo hili tunalichukua na tutakwenda kuona namna ya kulifikiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kikubwa kingine ninachotaka niseme ni kwamba, na hapa nataka nitoe agizo lakini pia nitoe wito kwa mamlaka hii inayosimamia; kwamba kwa sasa tuone namna ya kuwapa zaidi kipaumbele vijana ambao wanakwenda kutafuta ajira ili waweze kupatiwa hivi vitambulisho kwasababu tumeona na tumegundua kwamba kweli hii imekuwa ni changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na yote hayo nichukue fursa hii niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba bado kuna wilaya vitambulisho vipo wenyewe hawajaenda kuvichukua, sasa matokeo yake tunaendelea kupata lawama. Tunataka tutoe wito tuwaambie Waheshimiwa Wabunge kwa kushirikiana na viongozi wengine huko wa Chama na Serikali muwaambie watu waende wakachukue vitambulisho vyao. Yapo maeneo vitambulisho vipo lakini hawajaenda kuvichukua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba, kwanini sasa tusiunganishe RITA na NIDA. Lengo na azma ya Serikali siku zote ni kuhakikisha kwamba wanatengeneza muunganiko wa mfumo ili wananchi waweze kupata huduma kwa urahisi zaidi. Sasa kuunganisha RITA na NIDA si tatizo, Serikali ipo tayari kuunganisha mifumo lakini kuziunganisha taasisi nadhani ni jambo ambalo tunahitaji tukae sasa tufikirie tuone namna bora ya kuziunganisha hizi. Ni kweli zote ni taasisi za Serikali lakini zinao utofauti katika muundo na katika majukumu yake. Kwa hiyo nalo hili pia tutalichukua tuone namna ambavyo tunaweza tukaenda tukasaidia wananchi. Nakushukuru.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved