Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Primary Question

MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga daraja linalounganisha Wilaya ya Kilindi na Kiteto kupitia Kijiji cha Sambu?

Supplementary Question 1

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu haya ya kusema kwamba huu wa fedha unaoanza keshokutwa hapo tumetengewa shilingi milioni 182 kwa ajili ya kutengeneza kalavati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la msingi lilikuwa linazungumzia kwamba ni lini Serikali itatengeneza daraja, kama katika maelezo yake alivyosema kwamba eneo hili lina kilometa 38 zinazounganisha Wilaya ya Kiteto na Wilaya ya Kilindi. Eneo hili lina changamoto kubwa kwa sababu daraja ni kubwa sana, kiasi hiki kilichotengwa hakitoshi hata kidogo kwa ajili ya kujenga daraja.

Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakwenda yeye au wataalam wake kwenda kuangalia upana wa daraja hili ili Serikali iweze kutenga fedha za kutosha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; miaka ya nyuma Serikali ilishatenga pesa kwa ajili ya daraja hili, lakini nina uhakika thamani ya fedha kwenye daraja hili haikufanyika.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kutuma timu kuona kama fedha hizi zilitumika ipasavyo? Ahsante. (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua Mbunge wa Kilindi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa anachokieleza Mheshimiwa Mbunge, kwamba daraja lile ni kubwa na Bonde la Mto Sambu kama alivyokuwa amelianisha hapa ni bonde ambalo limeongezeka na linakadiriwa kuwa urefu wa mita 75. Na kwa tathmini ya awali ambayo ilikuwa imefanyika kwenda kufanya matengenezo katika eneo hilo ambalo linahusu hilo daraja, kuna makaravati kama 18, pamoja na drift yaani vile vivuko mfuto vidogo zaidi ya 30 na kitu. Na ilivyofanywa tathmini ya fedha ya awali ni kwamba eneo hilo linahitaji zaidi ya bilioni 2.9 ili kuhakikisha hiyo barabara iwe inapitika muda wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi tu niseme kabisa kwamba Mheshimiwa Mbunge kama alivyosema mimi mwenyewe nitafika eneo hilo ili niweze kushuhudia, na vilevile nitaituma timu kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenda katika eneo husika. Lakini kikubwa ni kwamba kwa sasa tuna ufinyu wa bajeti ndio maana umeona tumetenge hizi fedha chache. Lakini Bajeti Kuu ya Serikali ikipita, na kile chanzo kipya ambacho tunapelekea fedha kuongezea TARURA ninaamini tutazingatia hili ili barabara hii iweze kupitika kwa wakati wote.

Mheshimiwa Naibu Splika, kwa hiyo tunaomba Waheshimiwa Wabunge mpitishe Bajeti Kuu ya Serikali ili tupate kile chanzo cha uhakika na ninaamini katika mwaka ujao wa fedha hili swali halitaulizwa tena, tutakuwa tumeshalifanyia kazi. Ahsante sana.