Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa shule za sekondari utaanza katika kata zisizo na shule za sekondari nchini ili kuendana na mpango wa Serikali wa kuhakikisha kila kata inakuwa na shule ya sekondari?

Supplementary Question 1

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ambayo yanaonesha kwamba kazi inaendelea. Lakini niiombe Serikali, pamoja na kazi, kasi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mtwara una Kata 191 na kati ya Kata hizo, 137 zina shule za sekondari na Kata 57 hazina shule za sekondari. Na jambo hili linasababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu sana kufuata shule za sekondari, na matokeo yake ni upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa katika Mkoa wa Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, je, katika shule hizi 310 Mkoa wa Mtwara umetengewa shule ngapi katika kipindi hiki? Hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba shule ni walimu pamoja na mambo mengine yote. Sasa Mkoa wa Mtwara una upungufu wa walimu wa sayansi wa asilimia 41. Sasa nina wasiwasi kwamba kama hakutakuwa na maandalizi ya kutosha, kukamilika kwa madarasa au kwa shule hizi zitakazojengwa kutaongeza tena upungufu wa walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba baada tu ya kukamilika kwa shule kunakuwepo na walimu wa sayansi wa kutosha ili kupunguza tatizo la uhaba wa walimu wa sayansi? Ahsante. (Makofi)

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari umeshanipa mwongozo kuhusu takwimu sahihi na mimi nitampatia takwimu sahihi katika mwaka huu wa fedha tutajenga shule ngapi. Lakini niwahakikishie wananchi wa Mtwara kwamba Kata zote zilizobaki 57 zitajengwa sekondari za Kata kwa sababu zipo katika mpango wetu kwa sababu idadi ya shule tulizonazo zinatosheleza Kata zote nchini ambazo hazina shule hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, anasema Mkoa wa Mtwara una upungufu wa walimu, hususan wa sayansi, na alitaka kujua mpango wa Serikali ni upi kuongeza. Ni kwamba Serikali itaendelea kuajiri kama ambavyo tulitangaza hizi ajira ambazo muda mfupi, ndani ya wiki mbili hizi tutakuwa tumeshatoa hayo majina. Lakini vilevile Serikali itaendelea kuajiri walimu wengi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu kwamba tutaendelea kuangalia hivyo vigezo ambavyo amevitaja, wakiwemo walimu wa sayansi, na masomo mengine hatutayaacha kwa sababu yote yanahitajika katika elimu yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri, wakati unajibu hapo umesema fedha zinatosheleza kwenda kwenye kata zote ambazo hazina shule, na Mtwara wanazo 57. Hizo sule zote zitajengwa mwaka huu wa fedha?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ambacho nilikuwa nakieleza kwa kifupi ni kwamba Mradi wetu wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari Nchini ni ujenzi wa shule za sekondari 1,000. Na awamu ya kwanza Mwaka huu wa Fedha ambao tunakwenda, 2021/ 22, tunaanza kujenga shule 310.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika hizi 310 ni kwa mwaka huu. Halafu mwakani tutakuwa na idadi nyingine ya shule kwa Mwaka mwingine wa Fedha kwa maana ya 2022/2023, tutaleta fedha nyingine. Lakini mradi wetu unatosheleza kujenga shule zote kwa sababu tuna upungufu katika Kata kama 780 ambazo hazina sekondari za Kata hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo bado tutajenga na bado zile kata ambazo zina idadi kubwa ya wanafunzi tutapeleka vilevile sekondari nyingine, yaani kutakuwa na sekondari mbili katika Kata moja ili tuweze ku-accommodate idadi kubwa ya wanafunzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilichomwambia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba awe na uhakika kwamba Kata zote za Mtwara zitafikiwa. Lakini kwa mwaka huu nitampa idadi kamili ya shule ngapi tunajenga na mwakani tutajenga shule ngapi na mara ya mwisho tutamaliza kwa ngapi. Ahsante.