Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kurasimisha vitambulisho vya wajasiriamali?

Supplementary Question 1

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wapo wafanyabiashara ambao hawalipi ushuru, wamejitoa kwenye kodi na leseni kwa kisingizio cha kukosekana kanuni za vitambulisho vya mjasiriamali.

Ni nini kauli ya Serikali juu ya upotevu wa mapato unaosababishwa na wafanyabiashara hawa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa namna hali ilivyo huko site, vitambulisho hivi inaonekana kama ni hiyari, zoezi lake ni gumu na kwa wale wanaovikataa hakuna hatua yoyote ya kuwachukulia kikanuni.

Sasa ni lini Serikali itatoa kanuni hizo za vitambulisho vya mjasiriamali ili kuondoa mkanganyiko huo na kuweka bayana masharti na utaratibu wa vitambulisho hivyo? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niseme kimsingi vitambulisho hivi vilitolewa kwa nia njema ya kuhakikisha wajasiriamali na
wafanyabiashara wadogo wanafanyabiashara kwa utulivu kwa kuwa na kitambulisho kinachowawezesha kutoa huduma zao za biashara bila kulipa gharama nyingine kama ilivyokuwa siku za kule nyuma.

Kwa hiyo, kanuni zimetolewa wazi kwamba kwanza ni mfanyabiashara mdogo, mwenye mzunguko wa biashara usiozidi shilingi milioni nne kwa mwaka lakini mfanyabiashara ambaye kimsingi anapatikana katika eneo husika linalofanyabiashara, lakini anaweza kufanya biashara sehemu nyingine; lakini kanuni nyingine ni kwamba kinatumika kwa miezi 12 tangu tarehe ile ya kukatwa kitambulisho kile.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa wafanyabiashara wadogo ambao hawalipii vitambulisho hivi, maana yake watakuwa tayari kulipa gharama zilizopo kisheria za kufanya biashara kwa maana ya ushuru mbalimbali na gharama zingine. Kwa hiyo, tunaendelea kuwaelimisha na walio wengi kwa kweli wanaona hii ni njia bora zaidi kwa sababu wanapata nafuu ya kulipa ushuru kila siku kwa kulipa kitambulisho kwa mwaka mmoja.

Mheshimiwa Spika, pili, vitambulisho hivi ni vya hiyari, lakini elimu inaendelea kutolewa ili walio wengi waweze kuona umuhimu wake na kuvitumia, ahsante.