Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Cecilia Daniel Paresso
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: - Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na baadhi ya askari wa TANAPA wanaolinda Hifadhi ya Msitu wa Marang inayopakana na Kata ya Buger Wilayani Karatu kujichukulia sheria mkononi na kuwaua wananchi wanaoingia kwenye hifadhi?
Supplementary Question 1
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwanza nisikitike kwa majibu yasiyoridhisha au niseme labda ya sitaki kutumia kauli kama ya uongo dhidi ya matukio haya ambayo yametolewa na Serikali, na imekuwa ni rahisi sana askari wa TANAPA kujichukulia sheria mkononi kuliko majeshi mengine yoyote, na hii inafanyika maeneo mbalimbali nchini.
Sasa swali langu la kwanza; tarehe 29 Desemba, 2020 wananchi saba waliingia hifadhilini ikisadikika wanakwenda kuchimba madini, wananchi wanne mpaka leo hawajulikani walipo na inasemekana wamechomwa moto hadi kufa na askari wa TANAPA.
Je, hao nao waliamua wenyewe kujichoma au askari wa TANAPA waliwachoma wananchi hao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; tarehe 22 Oktoba, 2020 siku ya kupiga kura askari wa TANAPA waliwapiga risasi ng’ombe kumi wa mama mjane kwenye eneo hili mpaka leo mama huyu hajafidiwa wale ng’ombe sasa hawa ng’ombe nao walijipiga risasi wenyewe au askari wa TANAPA waliwapiga risasi?
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecilia Paresso, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba maelezo yote niliyosema hapa ni kweli na akihitaji ushahidi tutautoa kama Serikali. Askari wetu ni wengi sana wanauawa na tumekuwa tukishambulia zaidi askari, lakini haya matukio yanatokea pande zote mbili kwamba askari wanakuwa kwenye sheria na kukabiliana na maeneo yao ya hifadhi kwa maana ya kuyalinda yale maeneo lakini inapotokea sasa wananchi kutotii sheria basi huu mtafaruku unatokea.
Mheshimiwas Spika, lakini kwenye hili analoliongelea kwamba waliingia na kuchomwa moto, mimi hilo siwezi kuliongelea hapa kwa sababu taarifa zake tulishawahi kuziongelea hapa kwamba ziko kwenye uchunguzi na DNA ilishapelekwa kwenye maeneo yetu ya uchunguzi na taarifa hizi ni za kiusalama zaidi, kwa hiyo, tamko la Serikal litakuja kutolewa baada ya uchunguzi kufanyika.
Mheshimiwa Spika, na hili la risasi kwamba kuna ng’ombe walipigwa risasi pengine labda nimuombe Mheshimiwa atuletee uthibitisho kwamba wakati ng’ombe hawa wanauawa kama alikuwepo basi tuweze kulishughulikia, lakini vinginevyo ninaomba sana na nimuombe kama anavithibitisho vyovyote ambavyo askari walienda kupiga hao ng’ombe atuletee na Serikali itachukua hatua, ahsante. (Makofi)
Name
Christopher Olonyokie Ole-Sendeka
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Simanjiro
Primary Question
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: - Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na baadhi ya askari wa TANAPA wanaolinda Hifadhi ya Msitu wa Marang inayopakana na Kata ya Buger Wilayani Karatu kujichukulia sheria mkononi na kuwaua wananchi wanaoingia kwenye hifadhi?
Supplementary Question 2
MHE. CHRISTOPHER O. OLE-SENDEKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniona.
Kwa kuwa mgogoro unaoendelea kati ya askari wetu wa uhifadhi na wananchi wanaozunguka katika msitu wa Marang unafanana kabisa na mgogoro unaoendelea hivi sasa kati ya wananchi wa vijiji vya Kimotorok kwa upande wa Simanjiro na Kijiji cha Kiushiuborko kwa upande wa Kiteto dhidi ya pori la Mkungunero Game Reserve askari wanaoishi Mkungunero Game Reserve na kwa kuwa mgogoro huu ni wa muda mrefu na ulifikia Serikali kukubali kurudisha eneo ambalo walipima kwa makosa kinyume na GN iliyotakiwa Mkungunero Game Reserve imebaki Kondoa sasa imevuka mipaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itaamua sasa kuja kukaa na wananchi wa vijiji vinavyozunguka Mkungunero Game Reserve kumaliza mgogoro huu ili kuepusha maisha wa watu na vitendo vinavyofanana na hivi ambavyo Waziri akihitaji, hata hapa ndani nitoe ushahidi wa vitendo vya kinyama walivyofanyiwa wananchi wa Kimotorok na wahifadhi, nitakupa kwenye simu yangu hii? Nitakupa nashukuru sana naomba swali langu lijibiwe. (Makofi)
Name
Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Songea Mjini
Answer
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ufafanuzi ambao aliutoa awali, lakini pia niweze kumjibu Mheshimiwa Ole-Sendeka kwamba tunapotaka kutatua tatizo lazima twende kwenye kiini cha tatizo. Wote tunajadili hapa na hakuna siri ni kweli yanatokea mapigano kati ya askari wa Maliasili pamoja na wananchi, lakini mapigano haya yanatokea ndani ya maeneo ya hifadhi.
Kwa hiyo kwanza Mheshimiwa Ole-Sendeka na Waheshimiwa Wabunge wote tusaidiane kuelimisha wananchi wetu kwanza tusiingie, na endapo wananchi wanaingia kwa bahati mbaya na akatendewa visivyo tutoe taarifa, tupate huo ushahidi, tuwawajibishe askari hawa ambao hawafanyi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeshawawajibisha askari kadhaa, nilitoa takwimu hapa, askari 61 tumewafukuza kazi kwa sababu ushahidi umeletwa. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge pale wananchi wetu ambapo wanafanyiwa ndivyo sivyo tuletewe ushahidi ili tuwashughulikie askari hawa, lakini na sisi tuna wajibu wa kuwashauri na kuwaelekeza wananchi wetu tusiingie kwenye maeneo haya yaliyohifadhiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pili ameongelea suala la Mkungunero, tulifanya kikao mimi Mheshimiwa Lukuvi pamoja na Mheshimiwa Olelekaita kuhusiana na Mkungunero kuhusiana na dispute ya mpaka wa Mkungunero na tukakubaliana tunapeleka wataalam kwenda kuhakiki mpaka huo kwa mujibu wa coordinates ambazo zimewekwa kwenye GN. Niseme hapa kuna tatizo moja, katika maandishi katika maneno imesema ni Wilaya ya Kondoa lakini coordinates zimefika Wilaya ya Kiteto, sasa kitaalam zile coordinates zina prevail, kwa hiyo, wataalam waende wakatuoneshe coordinates hizi zinatakiwa kuvuka au zisivuke ili tutatue mgogoro huo.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Name
Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kondoa
Primary Question
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: - Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na baadhi ya askari wa TANAPA wanaolinda Hifadhi ya Msitu wa Marang inayopakana na Kata ya Buger Wilayani Karatu kujichukulia sheria mkononi na kuwaua wananchi wanaoingia kwenye hifadhi?
Supplementary Question 3
MHE. DKT. ASHATU K. KIJAJI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, tatizo la Pori la Hifadhi la Akiba la Mkungunero ni tatizo kubwa ambalo limegharimu maisha wa wananchi wetu limegharimu maisha hata ya wanyama pori wenyewe.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kondoa wangependa kujua ni lini ripoti ya Mawaziri ambayo ilikuwa ni taarifa ni timu iliyoundwa na Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ikaenda timu ya Mawaziri nane kwenda kufanya kazi na kuzunguka kwenye mapori yote likiwepo Pori la Hifadhi ya Mkungunero. Sasa ni lini ripoti ile itatolewa kwa wananchi na mipaka ikajulikana ili matatizo ambayo wananchi wameyaishi kwa miaka 50 na zaidi yaweze kufika mwisho sasa? Ahsante sana. (Makofi)
Name
William Vangimembe Lukuvi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Answer
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, wakati wa bajeti ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili nilisaidia kuchangia na nikasema kwamba tumekubaliana tutapita kwenye maeneo haya yote ya migogoro ili kuhakiki kwa pamoja kwa kutumia idara inayohusika na upimaji wa ramani ambayo ipo chini ya Wizara yangu, kwenda kuhakiki maeneo yote haya yenye migogoro ili tuweze kuchukua hatua. (Makofi)
Lakini nataka kumpa taarifa katika eneo hilo la Mkungunero timu ya Wizara yangu ipo huko wiki hii, kwa maombi ya Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto, lengo ni kwenda kuhakiki mipaka ya Mkungunero kulinganisha na GN iliyoanzisha pori na ndicho kilichoombwa na Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto, kwamba yeye hapingi pori, lakini anataka kujua ana mashaka pori lina mipaka tofauti na ile ya GN kwa hiyo timu ya wataalam wa Wizara yangu na Wizara ya Maliasili wako Mkungunero hivi sasa kwenye pori hilo hilo wanafanya hiyo kazi ya uhakiki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini juu ya matokeo ya ile timu ambayo iliagizwa na Serikali tulikuwa tumeshasema hapa kwamba tuliomba fedha mwaka huu na tumepewa kwenye bajeti hii, tunakwenda sasa kuwajulisha na Wakuu wa Mikoa wanajua.
Mheshimiwa Spika, lakini tunakwenda kutelekeza sasa uamuzi wa Baraza la Mawaziri yale maeneo ambayo wananchi wameachiwa tutakwenda kuwaonesha na yale maeneo ambayo yanaondoshwa ndani ya hifadhi tutakwenda kuwaonesha na yale maeneo ambayo yanakaa ndani ya hifadhi tutawaonesha na tutaweka mipaka inayoonekana.
Kwa hiyo shughuli hiyo hatujaifanya katika maeneo yale lakini mwaka huu Wizara ya Maliasili na ya kwangu tumepewa fedha tunakwenda kufanya kazi hiyo rasmi baada ya bajeti hii. (Makofi)
Name
Salma Rashid Kikwete
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mchinga
Primary Question
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza: - Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na baadhi ya askari wa TANAPA wanaolinda Hifadhi ya Msitu wa Marang inayopakana na Kata ya Buger Wilayani Karatu kujichukulia sheria mkononi na kuwaua wananchi wanaoingia kwenye hifadhi?
Supplementary Question 4
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; swali langu linahusiana na suala la maaskari.
Mheshimiwa Spika, nini kauli ya Serikali juu ya kutuletea kituo katika Tarafa ya Milola, sababu ya msingi ni kwamba ndani ya tarafa ile kila usiku uchao, kila asubuhi kuna taarifa ambayo ninaipata juu ya wanyama hasa tembo kuja kuzunguka katika maeneo yale ambayo watu wanaishi na matokeo yake watu wanapoteza maisha yao na nilishasema watu wamepoteza maisha, mazao yanaharibika kila siku na tunaambiwa tulime, sasa hata kama watu watalima nini matokeo yake.
Naiomba Serikali inipe tamko au inihakikishie juu ya kuleta kituo katika eneo letu lile ili askari wale waweze kushughulika na wale wanyama, ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Mama Salma ni askari anakuwa wa Halmashauri au unataka wa Wizara?
MHE. SALMA R. KIKWETE: Ikiwa wa Halmashauri sawa, ikiwa ni wa Wizara sawa, lengo ni kuhakikisha kwamba askari wanakuwepo na maisha ya wananchi yanakuwa salama. (Makofi)
Name
Mary Francis Masanja
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Answer
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa
Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na utalii naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, niwape pole kwanza wananchi wa eneo lile kwa kuendelea kuvamiwa na tembo, lakini Serikali itapeleka askari pale ambao wataenda kulinda ili kupunguza kadhia hii ya wanyama wakali na waharibifu kama tembo.