Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Shamsia Aziz Mtamba

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itawapatia wazee hasa wa vijijini bima ya afya ikiwemo ya CHF inayotolewa na Halmashauri?

Supplementary Question 1

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali inawaambia nini wananchi hasa wazee wenye kadi za Bima ya Afya pindi wanapokwenda kupata huduma na kujibiwa dawa wakanunue madukani; nini majibu ya Serikali juu ya hili?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kutokana na ongezeko kubwa la zahanati vijijini changamoto kubwa ni upatikanaji wa dawa, vifaa tiba kwa maana ya vipimo na waganga. Nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha vifaa hivi vinapatikana bila usumbufu?

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Spika, ni kweli concern ya Mbunge anayoisema ndiyo concern kubwa ambayo imeonekana kwenye eneo la CHF ambayo wananchi wengi wamekuwa wakienda na wakifika kwenye kituo wanakutana na tatizo hilo la upatikanaji wa dawa pamoja na daktari kumwandikia na CHF ni kwamba haiwezi kumsaidia mtu huyu kupata kwenye maduka mengine dawa zaidi ya kwenye kituo husika.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana sasa hivi Serikali umesikia moja; Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi bilioni 123 kwa ajili ya kuboresha eneo la dawa, maana yake sasa wakienda vituoni watakutana na dawa. Lakini umemsikia Waziri wetu kwa sababu suala la upatikanaji wa dawa vituoni ni zaidi tu ya fedha zenyewe kupatikana ndiyo maana umemsikia Waziri wetu wa Afya pamoja na Waziri wa TAMISEMI wameanza kufanya kazi kubwa sana kwenye eneo la uadilifu kuhakikisha kuna accountability kwenye eneo zima la dawa. Kwa hiyo hilo ndilo jibu la swali lako la kwanza.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili ni upatikanaji vilevile wa dawa na vifaa tiba vituoni; nalo linajibiwa na swali la kwanza kwa sababu tukishakuwa na shilingi bilioni 123 ambayo Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ameshazitoa kimsingi tutakuwa tumetatua hilo tatizo. Lakini vilevile sasa tunapokwenda kwenye Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote maana yake hata tukiingia watu wote wakapata bima ya afya inayofanana na hizi ambazo wafanyakazi wa Serikali wanazo hata kama watakosa dawa kwenye kituo chake, kuna maduka ya dawa ambayo yanatumia Bima ya Afya ambayo ni hii kubwa ya Taifa kwa hiyo tatizo hilo la dawa litaondoka.

Name

Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Primary Question

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itawapatia wazee hasa wa vijijini bima ya afya ikiwemo ya CHF inayotolewa na Halmashauri?

Supplementary Question 2

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mheshimiwa Waziri katika jibu lake amesema kwamba wanaruhusu kuwahakiki wazee na kwa sababu mfumo wa kuhakiki wazee haujawa rasmi, mmewaachia Halmashauri na ndiyo unakwamisha wazee wengi kutokupata huduma hii kwa kigezo cha kutokusajiliwa.

Ni nini hatua ya ziada ya Serikali kuhakikisha wazee wote wanasajiliwa katika muda ambao umepangwa ili wapate haki yao ya matibabu? (Makofi)

Name

Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL):
Mheshimiwa Spika, labda nijibu swali zuri la Mheshimiwa Mbunge, moja; nachukua concern yake kwa sababu ameonesha kuna tatizo kwenye eneo zima la utambuzi wa wazee. Kwa hiyo tutaenda kukaa kuona ni namna gani tunaweza kuboresha hilo eneo hasa la utambuzi wa kujua ni nani mzee na nani siyo mzee.

Lakini kwa sababu tunakwenda, suala hapa ni tiba ni ku-access tiba tunapokwenda kwenye Muswaada wa Bima ya Afya kwa Wote kimsingi hilo litakuwa lipo contained kwenye utaratibu mzima, kwa hiyo, halitakuwa tatizo.