Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Abubakar Damian Asenga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilombero
Primary Question
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: - Je, Serikali ina mikakati gani ya kuanza uzalishaji katika Kiwanda cha Chuma Mang’ula?
Supplementary Question 1
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, japokuwa majibu ya Serikali zijaridhika nayo sana, lakini kwa kuzingatia kuwa Kassim Faya Nakapala Mwenyekiti wa Halmashauri na Ebeneza Emmanuel Katibu wa CCM wa Wilaya wako hapa kufuatilia miongoni mwa mambo mengine jambo hili na Diwani wa Kata husika Fatma Mahigi wa Mang’ula “B” kwamba eneo hili sasa limekuwa hatarishi sana ni eneo ambalo lina ekari takribani 250 na akina mama wameshaanza kubakwa. Naomba kuiuliza Serikali maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza Serikali ipo tayari kuweka ulinzi wakati huu inatafuta mwekezaji wa kuwekeza katika Kiwanda hiki cha Machine Tools?
Lakini pili naomba kuiuliza Serikali sasa hivi tunajenga reli ya kisasa ya SGR na hii reli ya kisasa itahitaji mataruma na kadhalika, kwa nini wasikabidhi eneo hili na kiwanda hiki kwa SGR ili iendelee kutumia kuzalisha vifaa vya reli? Ahsante. (Makofi)
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana ndugu yangu Asenga kwa ufuatiliaji kwa ajili ya maendeleo ya Jimbo lake na hasa katika sekta ya viwanda na kwa ajili ya ufufuaji wa kiwanda hiki cha Mang’ula Machine Tools.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli eneo hili limekuwa kwa muda mrefu halitumiki kama nilivyosema kwa sababu mwekezaji aliyepewa eneo hili kuliendeleza hajaliendeleza kwa muda mrefu, nichukue nafasi hii kumuahidi kwamba tutashirikiana na Halmashauri kuona namna bora ya kuweka ulinzi ili eneo hili lisiwe hatarishi kwa sasa ambapo bado hatujapata mwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili kama nilivyosema tunaangalia matumizi bora ikiwa ni pamoja na kutafuta wawekezaji ambao wataweza kutumia eneo hili kwa ajili ya kuwekeza viwanda, tuchukue pia hoja ya Mheshimiwa Mbunge kwamba kama wenzetu wa reli ya kisasa watataka kutumia eneo hili kwa ajili ya kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa ajili ya kutumika katika SGR basi nao tutawakaribisha, ahsante sana.
Name
Dennis Lazaro Londo
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mikumi
Primary Question
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza: - Je, Serikali ina mikakati gani ya kuanza uzalishaji katika Kiwanda cha Chuma Mang’ula?
Supplementary Question 2
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniruhusu kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa kiwanda hiki kipo katika eneo la kimkakati kwa sababu kimezungukwa na mashamba ya miwa ama eneo ambalo linalima miwa kwa wingi, na kwa kuwa kulikuwa na mpango wa ku-transform kiwanda hiki kwenda kuzalisha sukari.
Je, Serikali inatoa tamko gani ikizingatiwa kwamba sasa hivi kuna mpango wa kuboresha viwanda vidogo vidogo vya kuzalisha sukari?
Name
Exaud Silaoneka Kigahe
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Answer
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Dennis Londo, Mbunge wa Jimbo la Mikumi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ukanda huu wa Kilombero ni ukanda ambao tunaweza tukasema ni wa kimkakati kwa uzalishaji wa miwa na sukari kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya hapa nchini. Ni kweli ni moja ya azma ya Serikali kuhamasisha au kuvutia wawekezaji wengi katika kuchakata miwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi tunatafuta wawekezaji mahiri ambao watajitokeza kuwekeza katika eneo hili ikiwemo wale ambao watataka kuchakata miwa basi na sisi tutawakaribisha ili kutumia nafasi hiyo katika eneo hili la Machine Tools kama sehemu ya kuwekeza viwanda vya kuchakata miwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tupo tayari na tusaidiane na Wabunge ili tuweze kuwekeza katika maeneo haya kwa umahiri zaidi, ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved