Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JULIANA D. SHONZA aliuliza: - Je, ni lini jengo jipya la hospitali lililojengwa Tunduma litafunguliwa na kuanza kutoa huduma kwa wananchi?

Supplementary Question 1

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. Sote tunafahamu kwamba ni adhma kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita kumaliza changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi. Pia tunafahamu kwamba kwenye mwaka huu wa fedha Serikali imetenga zaidi ya bilioni 1.5. Lengo ni kuhakikisha kwamba baadhi ya majengo katika Hospitali hii ya Tunduma yanakamilika. Hata hivyo changamoto kubwa ni kwamba mpaka sasa hivi hakuna jengo la wazazi. Kwa hiyo mimi nilitaka nitoe ombi kwa Serikali, kwamba iangalie sasa namna, kwamba kwenye mwaka huu wa fedha iharakishe kupeleka fedha hizo kwa haraka ili majengo hayo yatakapokamilika yasaidie pia kutoa huduma za uzazi kwa wanawake wa Mji wa Tunduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu; kwa kutambua jitihada kubwa ambazo zinafanywa na Mbunge wa Jimbo la Tunduma na Naibu Waziri Mheshimiwa David Silinde katika kuhakikisha kwamba hospitali hii inakamilika kwa wakati; nilitaka tu niweze kufahamu na wananchi wa Tunduma, Maporomoko, wa Muungano wa Kaloleni wanataka kumsikia Mbunge wao kwamba anasemaje, kwamba ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi wa hii hospitali kwa maana ya majengo, vifaa Pamoja na watumishi? Ahsante.

Name

David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza kwa kazi nzuri sana anayoifanya kwa wanawake wa Mkoa wa Mkoa wa Songwe, hususan kwenye kupigania masuala yao ya afya, anafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hili swali nasema nina interest nalo kidogo kwa sababu ni jimbo langu, na bahati nzuri leo nalijibu mimi mwenyewe. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya mama yetu Samia Hassan Suluhu ina dhamira ya dhati kabisa ya kusaidia sekta ya afya nchini. Ndiyo maana katika bajeti ya mwaka wa fedha huu 2021/2022 katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma imetengewa bilioni 1.5.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nimhakikishie tu kama Mbunge wa Jimbo husika fedha hiyo itafika na tutahakikisha kwamba inajenga kama amabvyo imekusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili ni kwamba anauliza ni lini hospitali ile itakamilika. Ni kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais imeshatoa fedha awamu ya kwanza imepeleka bilioni nne ambazo zimeshajenga jengo la kwanza na ambalo linatumika sasa hivi. Awamu ya pili tunapeleka bilioni 1.5, kwa hiyo itakuwa imebaki bilioni kama nne ya mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini Serikali ya Awamu ya Sita ina dhamira ya dhati kwenye hilo na ile hospitali itapelekewa fedha zote, kwa sababu muda bado upo na itajengwa na itakamilika kama ambavyo imekusudiwa. Ahsante sana.