Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Benaya Liuka Kapinga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbinga Vijijini
Primary Question
MHE. BENAYA L. KAPINGA aliuliza: - Je, ni lini Vituo vya Afya vya Mapera na Muungano vitaanza kutoa huduma ya upasuaji ambao haufanyiki kutokana na kukosekana kwa baadhi ya vifaa ikiwemo sterilizer?
Supplementary Question 1
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nishukuru kwa majibu yanayoridhisha ya Serikali. Ni kweli kituo hiki cha Mapera kuanzia mwezi Julai kimeanza kutoa huduma. Kituo cha Muungano, wananchi hawa kituo hiki wamekijenga wenyewe kwa asilimia 100 kwa kusaidiwa na mapato ya ndani kidogo sana, hiyo shilingi milioni 60, lakini sasa wanahangaika kujenga jengo la wazazi. Je, Serikali ina mpango gani kuunga jitihada hizi mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kata ya Kipololo imejenga Zahanati ya Kipololo, Kata ya Mbuji imejenga Zahanati ya Mnyao, Kata ya Litembo imejenga Zahanati Lituru lakini pia Kata ya Mkako Kiukuru wamejenga zahanati. Zahanati hizi zimekamilika, zingine sasa zina miaka mitatu, miwili mpaka leo hazijaanza kazi. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka watumishi katika zahanati hizi ili ziweze kuanza kufanya kazi? (Makofi)
Name
David Ernest Silinde
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tunduma
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Benaya Kapinga, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameomba tu Kituo cha Afya Muungano ambacho kimejengwa na wananchi kwa asilimia 100 na sasa hivi kuna jitihada za kujenga jengo la wazazi, anataka commitment ya Serikali. Niseme tumelipokea na tutaliweka katika mipango inayofuata ili kuhakikisha tunaingiza katika bajeti zetu hiki Kituo cha Afya cha Muungano ili kiweze kukamilika.
Mheshimiwa Spika, la pili kuhusu kata alizozitaja katika vijiji alivyoviainisha kama Kata ya Kipololo, Mbuji, Litembo na Likako ambazo zimejenga zahanati na mpaka sasa hivi bado hazijafunguliwa. Niseme tunalipokea na naamini watendaji wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambao wanasimamia Idara ya Afya wamelisikia hili, hivyo sasa tutajua namna ya kupanga watumishi waliopo na vile vile kama Serikali itaajiri hapo mbele kidogo tutapeleka watumishi ili vituo hivi vianze kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved