Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Stanslaus Shing'oma Mabula
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyamagana
Primary Question
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza: - Je, Serikali ina mkakati gani wa kutimiza masharti ya ajira kwa watumishi ikiwa ni pamoja na kuwapandisha madaraja na stahiki nyingine?
Supplementary Question 1
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nitumie nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuliangalia suala hili kwa kipekee na kulipa uzito na kuwapa matumaini wafanyakazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nafahamu ya kwamba taasisi nyingi za Serikali zimekuwa na utaratibu wa kuchukua wafanyakazi kwa muda, kwa maana ya vibarua na wengine wanakuwepo kwa mikataba ya muda mfupi. Inapotokea suala la ajira, mara nyingi sana watu hawa wamekuwa wanasahaulika na kuchukuliwa watu kutoka nje. Kwa mtindo ule ule wa Serikali kuamua kuboresha maslahi ya wafanyakazi, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha vibarua na wale ambao wana ajira za muda, zinapopatikana fursa wanaajiriwa kwanza wao kama kipaumbele na wengine ndio wanafuata?
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Name
Deogratius John Ndejembi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chamwino
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Sera ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambayo ilipitishwa mwaka 2008 inaeleza wazi namna ya kupata Watumishi wa Umma kwa njia ya ushindani. Sasa nafahamu kuna maeneo mengi hata majimboni kwa Wabunge wengi kuna watu wengi wanajitolea katika taasisi za Umma.
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Ummy Mwalimu alieleza mbele ya Bunge lako hili kwamba kuna database ambayo inaanzishwa kukusanya majina ya wale wote ambao wanajitolea maeneo mbalimbali nchini ambapo watapewa kipaumbele pale ambapo ajira zitajitokeza. Sasa nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wote wale ambao wanajitolea kuwasilisha majina yao Ofisi ya Rais, TAMISEMI kama ambavyo alikuwa ametoa maelekezo Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI.
Mheshimiwa Spika, kwa wale ambao hawapo katika ajira za Serikali za Mitaa, wao pia waorodheshe majina yao na kuyafikisha Ofisi ya Rais, Utumishi ili tuweze kuwa na database ya pamoja na pale ajira zinapotoka, basi tutaangalia. Kwa sababu kumekuwa kuna scenario ambazo watu wanajitolea pale tu wanaposikia ajira zinatoka ili waweze kupata favour ya kuweza kuingia kazini. Ili kudhibiti hilo na kuhakikisha ushindani upo katika kuajiri watu katika Utumishi wa Umma, ndiyo maana ajira zile zinatangazwa.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo hao wanaojitolea, naamini watakuwa na added advantage kwa sababu wameshaifanya ile kazi kwa vitendo na hivyo wanapoenda kwenye usaili watakuwa wako vizuri zaidi katika kuweza kupata ajira hiyo.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved