Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza: - Je, Serikali imesaidia mikopo kwa vikundi vingapi vya wavuvi Wilaya ya Nkasi?

Supplementary Question 1

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuuliza maswali, naomba niishukuru Serikali kwa kunipatia injini siku ya leo Kata ya Kabwe, ninawashukuru sana. Nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: - (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri amenukuu Ilani ya Chama Cha Mapinduzi Ibara ya 43(h), natambua kwamba Ilani hiyo haijasema tukawatie umasikini Watanzania/wavuvi, imeelekeza mkawapatie mitaji na mikopo. Watu wa Nkasi shida yetu sio Ilani ila Ilani isipotekelezwa hapo ndipo maswali yanakuja. Ni lini Ilani Ibara ya 43 itatekelezwa Wilaya ya Nkasi kwa kuwapatia mikopo wavuvi wa Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kupitia Ilani hiyohiyo, nimesoma mwanzo mpaka mwisho hakuna sehemu Ilani imesema tukawape umasikini Watanzania. Kwa kuwa baada ya operesheni ya uvuvi haramu, Watanzania hasa wavuvi wa Nkasi wamekuwa maskini. Ningependa kujua, nini mkakati wa Serikali kwa kuwapatia vifaa vya kisasa ili kuwaondoa wavuvi hawa katika umasikini. (Makofi)

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Aida Khenani kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, la kwanza; ninapokea shukrani kwa niaba ya Serikali na Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi uliyoitoa Mheshimiwa Aida Khenani kwa kuwawezesha wavuvi wa Kikundi cha Ushirika cha Kabwe.

Mheshimiwa Spika, lini tutatoa mitaji? Naomba Mheshimiwa Mbunge yeye na wataalam wetu waliopo kule Halmshauri ya Nkasi kwa pamoja tushirikiane katika kuhakikisha kwamba tunaandaa sasa utaratibu wa vikundi hivi kuweza kupata fomu, kuzijaza, waainishe, wapewe elimu kwa kusudio la kuweza kuwaunganisha na Benki ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Aida Khenani, nipo tayari kabisa kuhakikisha kwamba tunasimamia jambo hili katika kutekeleza Ilani makini kabisa ya Chama Cha Mapinduzi ili kusudi wananchi hawa waweze kupata mikopo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili; ni kwa namna gani tutawasaidia mara baada ya kufanya operesheni ambayo yeye Mheshimiwa Mbunge anaitamka kwamba imewatia umasikini. Nataka nikuhakikishie kwamba kwanza operesheni ile ilikuwa ni kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi na matokeo ya operesheni ile wengi wameyavutika kwa sababu tulipata samaki wengi, wakubwa na wazuri.

Mheshimiwa Spika, na sasa namna ya mpango tulionao wa namna ya kuwasaidia, moja ni hili tulilolifanya leo kwa kukukabidhi mashine itakayokwenda kuwasaidia watu wa kule Kabwe. Na ninakupa hamasa wewe na Wabunge wengine wanaotoka katika kanda ya uvuvi watuletee maombi zaidi ili kusudi Serikali tuweze kusaidiana nao. Na dirisha la Benki ya Kilimo liko wazi, sisi tunacho kitengo maalum cha kuweza kusaidiana na wavuvi kuandika programu zile na kwenda kuomba zile pesa ili waweze kununua zana bora na waweze kufika mahala mbali kunapoweza kuwasaidia kupata mavuno toshelevu na biashara nzuri, ahsante sana.