Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: - Serikali imewekeza kiasi cha Shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya kutengeneza miundombinu ya ukaguzi wa magari nchini (Destination Inspection). Je, ni sababu zipi zilisababisha Serikali kubadilisha mfumo huo?

Supplementary Question 1

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri, Tanzania Bureau of Standards na Bureau of Standards zote ulimwenguni kazi yake ni kulinda na kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingia nchini na zinazozalishwa ndani ya nchi.

Je, utakubaliana nami kwamba, TBS haipimwi kwa kiasi cha pesa inazoingiza nchini, kutokana na jibu lako ulilonijibu katika swali langu la msingi?

Swali la pili; kuna wale ambao wanashindwa kulipia yale magari, kwa kushindwa huko kulipia yale magari inabidi yale magari mtueleze mnapeleka wapi yale magari? Hamuoni kwamba, Tanzania mnataka kuigeuza kuwa dumping area? (Makofi)

Name

Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Mgaya, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Neema kwa ufuatiliaji wa siku nyingi kuhusiana na ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini. Ni kweli, kazi ya msingi ya TBS ni kuhakikisha na kudhibiti ubora wa bidhaa zote zinazoingizwa nchini ndiyo maana tumeamua sasa ili kuwa na ufanisi katika hilo kukagua sisi wenyewe kwa sababu kama nilivyosema katika jibu la msingi, baadhi ya mawakala huko nje walikuwa hawafanyi kazi ipasavyo na malalamiko bado yalikuwa mengi sana kwamba kuna baadhi walikuwa wanaletewa bidhaa ambazo hazina ubora lakini kwa sababu tayari mawakala walikuwa wamethibitisha kwa hiyo maana yake TBS ilikuwa haina namna ya kufanya.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa sababu sasahivi tunathibitisha wenyewe, pia tumeshawaambia makampuni yanayoleta bidhaa nchini kuhakikisha wanaleta bidhaa ambazo zina ubora. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Neema kwamba kazi hiyo inafanyika na ndiyo maana tunaamua kujiimarisha sasa ili TBS waweze kufanya kazi hiyo kwa uthabiti.

Mheshimiwa Spika, pili, kuhusu ubovu wa bidhaa au magari yaliyotumika yanayoingizwa nchini, kama nilivyosema mpaka sasa zaidi ya wateja hao 13,968 ambao wameingiza magari nchini hakuna hata mteja mmoja ambaye amelalamika kuhusiana na ubovu wa magari au bidhaa zinazoingizwa. Kwa hiyo, tunaamini sasa mfumo huo utaenda kuboreshwa zaidi kwa maana ya kukagua kwa ubora zaidi na tunawaelekeza wateja wetu kuhakikisha wanaingiza bidhaa kupitia makampuni ambayo tumekubaliana ambayo yanatoa bidhaa hizo kutoka nje. Ninakushukuru.