Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Issa Jumanne Mtemvu
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibamba
Primary Question
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: - Je, Serikali ina mpango wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara za Mbezi Shule – Mpiji Magohe – Bunju kupitia Mabwe Pande na Kibamba Njia Panda – Mpiji Magohe kama zilivyoainishwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020 - 2025?
Supplementary Question 1
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
(a) Kwa kuwa majibu mazuri yametolewa na Serikali, kwa umuhimu barabara hizi pamoja na kuondoa msongamano sehemu ya pembezoni mwa Mkoa wa Dar es Salaam lakini pia zinasaidia kufungua uchumi wa wananchi wa pembezoni. Aidha, barabara hizi zilipata baraka za Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na kuzitamani zijengwe kwa haraka na udharura. (Makofi)
Je, Serikali sasa haioni inayo kila sababu kukamilisha barabara hizi katika mwaka wa fedha 2022/2023? (Makofi)
(b) Kwa kuwa kilomita zilizotajwa 33.7 ina sehemu ya kilometa 1 ya barabara ya njiapanda ya shule na wanahitaji fidia. Je, Serikali imejipanga vipi kulipa fidia wananchi hawa? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
MHE. NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Jumanne Mtemvu Mbunge wa Kibamba kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika ni kweli kwamba Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyekuwa Rais aliahidi kwamba, barabara za Jimbo la Kibamba angetamani zijengwe zote kwa kiwango cha lami. Nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi za viongozi wa Kitaifa, zote tunazichukulia kwa umuhimu mkubwa sana na ndio maana hata akienda kwenye kitabu chetu cha bajeti, tumetenga tayari fedha, kwa ajili ya kuanza upembuzi kwa sababu, barabara zote zilizotajwa katika Jimbo lake ni za vumbi. Kwa hiyo, lazima hatuwezi tukaruka hatua ni lazima tutafanya upembuzi yakinifu na usanifu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge awe na uhakika kwamba tunatambua pia tutafungua uchumi wa Jimbo lakini pia kurahisisha mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa kawaida barabara zote zinapojengwa tutahakikisha kwamba hiyo fidia aliyoitaja, tunailipa kabla ya ujenzi na kama kuna changamoto zaidi ya hii ambayo tunafahamu ya kuilipa kwa kawaida, basi nimuombe Mheshimiwa Mbunge tuweze kuonana naye kwa ajili ya kupata maelezo zaidi. Ahsante. (Makofi)
Name
Anatropia Lwehikila Theonest
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: - Je, Serikali ina mpango wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara za Mbezi Shule – Mpiji Magohe – Bunju kupitia Mabwe Pande na Kibamba Njia Panda – Mpiji Magohe kama zilivyoainishwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020 - 2025?
Supplementary Question 2
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Barabara ya Murongo kuja Kibale kuja Bugara halafu mpaka Mgakorongo ni barabara ya hadhi ya Mkoa. Ikiunganisha Uganda na Tanzania na mchakato wake umechukua muda mrefu. Nataka kujua ni lini hiyo barabara itaanza kujengwa kwa sababu, imekuwepo mchakato wake muda mrefu. Nataka kujua Serikali imejipangaje? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
MHE. NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI – (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anatropia Lwehikila kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara iliyotajwa ni barabara kuu na ni barabara ambayo ni kweli inaunganisha Tanzania na Uganda katika lile eneo linaloitwa Murongo. Nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge barabara ile nimeitembelea na barabara hiyo kwa mwaka huu, imetengewa fedha kwa ajili ya kuanza kwa kiwango cha lami ujenzi huo. Kwa hiyo, nimuhakikishie kwamba ipo kwenye mchakato na barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
Name
Shamsia Aziz Mtamba
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Mtwara Vijijini
Primary Question
MHE. ISSA J. MTEMVU aliuliza: - Je, Serikali ina mpango wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara za Mbezi Shule – Mpiji Magohe – Bunju kupitia Mabwe Pande na Kibamba Njia Panda – Mpiji Magohe kama zilivyoainishwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2020 - 2025?
Supplementary Question 3
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante, kutokana na umuhimu wa barabara inayotoka Mtwara mjini kuelekea Msimbati, ambako kuna visima na mitambo ya gesi. Je, ni lini sasa Serikali itaona umuhimu wa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Name
Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ileje
Answer
MHE. NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara aliyotaja ni barabara muhimu kwa sababu inaenda kwenye maeneo ya kimkakati. Naomba nimuhakikishie kwamba kadri fedha itakavyopatikana katika bajeti zinapokuja, barabara hii tutaijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, tunaifahamu ni barabara muhimu kutegemea na upatikanaji wa fedha na hasa kwa bajeti ambayo tutaanza kuitengeneza mwezi wa tatu mwakani. Ahsante. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved