Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Innocent Sebba Bilakwate
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyerwa
Primary Question
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza agizo la Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutaka mwananchi aliyevamia ardhi ya Kijiji cha Nyarututu/Kabanga kurejesha ardhi hiyo kwa Serikali ya Kijiji ili itumike kwa faida ya wananchi?
Supplementary Question 1
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, maeneo mengi yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za Serikali ikiwemo afya pamoja na shule, yamekuwa yakivamiwa na watu ambao hawana nia njema: -
Serikali ina mpango gani maeneo haya yote ili yaweze kupimwa kuondoa hii adha ambayo imekuwa ikijitokeza? (Makofi)
Swali la pili; tunayo miji midogo kama Nkwenda, Nsingiro, Mrongo na Mabira. Maeneo haya yanakua kwa kasi: Serikali ina mpango gani wa kupima haya maeneo ili baadaye wasije wakaanza kuwavunjia wananchi nyumba zao? (Makofi)
Name
William Vangimembe Lukuvi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ismani
Answer
WAZIRI WA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, Naomba nijibu mawali mawili ya Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli uvamizi ni mkubwa sana katika maeneo mbalimbali, lakini nilitaka niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji, Mamlaka ya Upangaji wa Ardhi ni Halmashauri za Wilaya. Maana yake ni kwamba ukipanga unapaswa kusimamia, wanaopanga master plan. Wanaopanga mipango flani flani ya utekeleaji wa master plan ndani ya sheria za nchi hii ni Halmashauri ndiyo wanaohitaji na ndiyo wanaojua kwamba ardhi yao itumike namna gani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natoa wito kwa Halmashauri zote, zisimamie na zilinde maeneo kama yalivyopangwa na mamlaka zao. Maeneo yote ya wazi hayapaswi kutumika kwa shughuli nyingine na nimeelekeza wenzangu kwamba maeneo yote ya Umma kama yanaangukia kwenye sekta fulani, basi sekta hiyo iyalinde, ichukue hati na iweke mipaka inayoonekana/alama zinazoonekana, kama ni maeneo ya shule wayalinde wachukue hati, nasi tulisema hatutawadai kodi ya ardhi ya kila mwaka. Kama ni maeneo ya afya, basi yalindwe, yapimwe yachukuliwe hati na yawekewe alama zinazonekana ili wananchi waweze kujua. Kwa hiyo, ni jukumu letu kuyalinda.
Mheshimiwa Spika, la pili, ni kweli kutokana na ustaarabu na utekelezaji ulio mzuri wa sera za CCM na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, leo tuna umeme kila kijiji. Umeme unaleta ustaarabu na unabadilisha maisha. Kwa hiyo, imetokea kwamba baadhi ya vijiji vingi sasa vimeanza tabia ya kimji. Sheria inaelekeza kwamba maeneo hayo, Halmashauri myawahi mapema. Maeneo ambayo mnajua yameanza kuchipukia na maisha yanakuwa ya kimji, pelekeni na mjadili kwanza muainishe maeneo hayo hata kama ni ya vijiji, mpelekeeni Waziri wa Ardhi ayatangaze kama town planning areas ili maeneo hayo ya vijiji yanayochipukia kuwa na maisha ya kimji, Waziri ayatangaze ili yapangwe kimji na Halmashauri zipime na watu wapewe viwanja na hati kama za mjini. Kwa namna hiyo tunaweza tukalinda, baadaye kukawa hakuna squatter katika mji yetu. Kwa hiyo, ni jukumu letu Mheshimiwa Mbunge Halmashauri na sisi kama Wajumbe tusimamie katika kupanga na kusimamia ardhi yetu.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved