Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Selemani Jumanne Zedi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Primary Question
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga Jengo la Wodi za kulaza Wagonjwa pamoja na kupeleka mashine ya X-ray katika Kituo cha Afya Itobo kilichopo Jimbo la Bukene?
Supplementary Question 1
MHE. SELEMAN J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze Serikali kwa kupeleka milioni 250 katika Kituo cha Afya cha Itobo ili kuboresha miundombinu ya pale, lakini nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vituo vya afya vya zamani kama Kituo cha Afya cha Itobo na Kituo cha Afya cha Bukene vinaitwa vituo vya afya, lakini kimsingi havina ile miundombinu mizuri ambayo inafaa kuitwa kituo cha afya. Unakuta kinaitwa kituo cha afya, lakini hakina maabara, hakina wodi, hakina theater, hakina X-ray. Kwa hiyo, swali langu ni kwamba je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari baada ya Bunge hili na kabla ya Bunge la Februari kwenda Jimboni Bukene atembelee hivi vituo vya afya vya zamani ambavyo ni tofauti kabisa na vituo vya afya vya sasa, japo tunahesabiwa kwamba tuna vituo vya afya, lakini kimsingi haviendani kabisa na hali halisi inayopaswa kuwepo kama kituo cha afya? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Suleiman Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipokee pongezi zake kwa kazi hii kubwa ambayo imeendelea kufanywa na Serikali Awamu ya Sita, chini ya Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha tunajenga vituo vya afya ikiwemo katika Kata ya Itobo. Hata hivyo, nimhakikishie kwamba Serikali tunatambua vyema kwamba ni kweli vituo vyetu hivi bado vina upungufu wa miundombinu na ujenzi huu kama ambavyo nimejibu kwenye swali la msingi ni wa awamu. Kwa hiyo, tuko awamu hii ya kwanza ya ujenzi wa majengo ya kuanzia, lakini awamu ya pili tutakwenda kujenga majengo mengine yakiwemo wodi, lakini na majengo mengine ya vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwahidi Mheshimiwa Zedi kwamba niko tayari, tutakubaliana baada ya Bunge hili, tupange ratiba ya kwenda kule Bukene, tupitie Vituo vya Afya vya Itobo na Bukene, tuweze kufanya tathmini na kuona mpango wa kuendeleza ili viweze kuwa na hadhi ya vituo vya afya. Ahsante.
Name
Festo Richard Sanga
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Primary Question
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga Jengo la Wodi za kulaza Wagonjwa pamoja na kupeleka mashine ya X-ray katika Kituo cha Afya Itobo kilichopo Jimbo la Bukene?
Supplementary Question 2
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Changamoto iliyopo Bukene ni sawasawa na changamoto iliyopo Makete katika Kituo cha Afya cha Matamba ambacho kinahudumia zaidi watu 25,000, lakini hakina jengo la mama na mtoto, hakina X-ray. Kwa hiyo, naomba Serikali iniambie ni lini italeta fedha pale Matamba ili wananchi wangu waweze kupata huduma? Ahsante.
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Richard Sanga, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Kituo cha Afya cha Matamba Makete ni kituo ambacho kinategemewa na wananchi wengi zaidi ya 25,000, lakini ni kweli kwamba kina upungufu wa miundombinu ya majengo likiwemo jengo la mama na mtoto.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imechukua changamoto hiyo tunatafuta fedha ili twende kujenga majengo hayo mengine kuhakikisha wananchi wa Matamba wanapata huduma za kituo cha afya kilichokamilika. Ahsante.
Name
Yahaya Omary Massare
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Primary Question
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga Jengo la Wodi za kulaza Wagonjwa pamoja na kupeleka mashine ya X-ray katika Kituo cha Afya Itobo kilichopo Jimbo la Bukene?
Supplementary Question 3
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Kituo cha Afya cha Itigi ambacho kinahudumia watu wengi katika Mji wa Itigi kama hospitali, je, Serikali ni lini itapeleka X-ray katika kituo hiki?
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa vituo hivi vya afya unaendana na uwekaji wa vifaa tiba zikiwemo mashine hizi za X-ray na ununuzi wa mashine hizi unakwenda kwa awamu kwa kadri ya bajeti zetu. kwa hivyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua kwamba Kituo cha Afya cha Itigi kina uhitaji mkubwa wa X-ray na kinahudumia wananchi wengi, hivyo tutaendelea kutafuta fedha ili tupate mashine ya X-ray kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Kituo cha Afya cha Itigi. Ahsante. (Makofi)
Name
Simon Songe Lusengekile
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Primary Question
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: - Je, ni lini Serikali itajenga Jengo la Wodi za kulaza Wagonjwa pamoja na kupeleka mashine ya X-ray katika Kituo cha Afya Itobo kilichopo Jimbo la Bukene?
Supplementary Question 4
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Hospitali ya Halmashauri ya Busega inahudumia takribani wakazi 300,000 na hatuna kabisa X-ray inabidi wananchi wale kwenda kutafuta huduma za X-ray kwenye wilaya nyingine kama Bariadi, Bunda na Magu. Je, ni lini Serikali itaipatia X-ray Hospitali ya Halmashauri ya Busega ili iweze kuhudumia wananchi wake? (Makofi)
Name
Dr. Festo John Dugange
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Wanging'ombe
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Simon Songe Lusengekile, Mbunge wa Jimbo la Busega, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Hospitali hii ya Wilaya ya Busega haina mashine ya X-ray na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika vipaumbele vya kupeleka mashine za X-ray, kipaumbele cha kwanza ni kupeleka katika hospitali za halmashauri.
Kwa hiyo, kadri ambavyo tunaendelea kuweka mipango yetu tutahakikisha hospitali zote za halmashauri zinakwenda kupata X-ray na ushahidi tumeona katika fedha hizi za UVIKO tunakwenda kununua digital X-ray zaidi ya 75 kwa ajili ya hospitali zetu za wilaya ambazo hazina, lakini pia vituo vya afya ambavyo vina idadi kubwa ya wananchi. Kwa hiyo nimhakikishie kwamba tutaipa kipaumbele Hospitali ya Wilaya ya Busega. Ahsante sana. (Makofi)