Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Oran Manase Njeza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbeya Vijijini

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kugharamia matengenezo ya Reli ya TAZARA ambayo miundombinu yake imechakaa na ni muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania na hata nchi jirani za SADC?

Supplementary Question 1

MHE. ORAN M. NJEZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hali ya madaraja ya TAZARA, hasa kwa upande wa mataruma ya mbao, yana hali mbaya sana kiasi cha kuhatarisha maisha ya wasafiri pamoja na usalama wa mizigo. Je, Serikali ina mkakati gani na mpango wa haraka kupeleka fedha ili hayo madaraja yaweze kukarabatiwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; TAZARA ni muhimu sana katika ushindani wa Bandari yetu ya Dar es Salaam, huu ushindani wa kikanda unaifanya bandari yetu kuwa katika pressure kubwa sana. Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga pesa ya kutosha kupitia TPA Shirika letu la Bandari ili liweze kushiriki katika kujenga na kuboresha miundombinu ya TAZARA? Nashukuru. (Makofi)

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, anatoa taarifa ya hali mbaya ya Reli yetu ya TAZARA. Ninaomba nimuelekeze Mtendaji wetu wa TAZARA atembelee maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja, afanye tathmini ya haraka ili tuone kama hali ni mbaya kiasi hicho Mheshimiwa alivyozungumza basi ufanyike utaratibu wa kawaida kufanya marekebisho ili kuepuka madhara kwa mizigo na abiria ambao wanatumia eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anauliza kama kuna uwezekano wa TPA kuwekeza katika eneo hili. Mheshimiwa Mbunge ni Mjumbe wa Kamati tumekutana kule TPA Dar es Salaam, wazo hili alilitoa ni wazo jema. Tumewapa maelekezo watu wa TPA waangalie uwezekano wa kuwekeza katika eneo hili kwa sababu wanaihitaji TAZARA katika kusafirisha mizigo, walifanyie kazi, wafanye tathmini, tukijiridhisha basi wazo la Mheshimiwa Mbunge tutalifanyia kazi. Lengo ni kuweza kutoa huduma kwa watu wetu, hasa upande wa Tanzania. Ahsante. (Makofi)

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kugharamia matengenezo ya Reli ya TAZARA ambayo miundombinu yake imechakaa na ni muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania na hata nchi jirani za SADC?

Supplementary Question 2

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa njia pekee ya kuisadia TAZARA ni kubadilisha hiyo sheria iliyoanzisha TAZARA, Serikali inatoa tamko gani la haraka kuhakikisha sheria hiyo inabadilishwa ili Tanzania iwekeze zaidi kuliko wenzetu wa Zambia wanaosuasua? (Makofi)

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spik, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba sheria hii imekuwa ni kikwazo kwa upande wa Tanzania kuwekeza katika reli hii kwa sababu kama nilivyosema, hisa ni asilimia 50 kwa 50. Kila ukiwekeza upande wa Tanzania haiongezi hisa katika upande wetu, lakini nia ya Serikali ni kwamba ingewezekana hata leo sheria hii ingeweza kubadilishwa tuwekeze katika upande wetu kuweza kutoa huduma kwa watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, ni kwamba sheria hii hatuwezi kuibadilisha upande wa Tanzania mpaka tukutane na watu wa Zambia. Wenzetu walikuwa na uchaguzi wameshamaliza, wamefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, tumeshawaandikia barua tunasubiri wakijibu tukikutana jambo hili nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge litafanyiwa kazi haraka sana. Ahsante sana. (Makofi)

Name

Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Primary Question

MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kugharamia matengenezo ya Reli ya TAZARA ambayo miundombinu yake imechakaa na ni muhimu sana kwa uchumi wa Tanzania na hata nchi jirani za SADC?

Supplementary Question 3

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuuliza kuhusu hii reli kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi na Arusha ilifufuliwa, sasa imekufa, ni kitu gani kimeiua? Naomba Waziri hebu tueleze. (Makofi/Kicheko)

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Kimei kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hii reli haijafa ila zipo changamoto ambazo tunaendelea kuzifanyia kazi, kuongeza vitendeakazi pamoja na wafanyakazi katika eneo hili. Mheshimiwa Mbunge avute subira tunalifanyia kazi, reli hii itaendelea kufanya kazi ambavyo imekusudia Serikali, ndiyo maana ikaanzishwa baada ya muda mrefu sana. Ahsante.