Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. ESTER A. BULAYA K.n.y. MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza ajira kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu hasa katika sekta ya kilimo kwa kuwa mikopo ya elimu ya juu imewezesha wanafunzi wengi kuhitimu?
Supplementary Question 1
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Utakubaliana na mimi kwamba tatizo la ajira kwa vijana kwa nchi hii limekuwa kubwa na la muda mrefu na Serikali ilishaji-commit, wakati nikiwa Mbunge wa Vijana kipindi kile wakati tunapitisha hapa Sheria ya Baraza la Vijana. Kwamba, kila Halmashauri itatenga maeneo ya kilimo kwa ajili ya vijana hasa ambao ni graduate waweze kwenda kujiajiri wenyewe. Lakini ardhi yenye rutuba ya daraja la kwanza, daraja la pili wamekuwa wakipewa wawekezaji. Hii ardhi ambayo vijana wanaitumia unakuta wamepewa na Mjomba, Shangazi na Bibi.
Je, lini Serikali mtatimiza ahadi ambayo mmeweka kutenga ardhi kwa vijana na kuwawezesha ili asilimia kubwa ya vijana waweze kujiajiri wenyewe? (Makofi)
Swali la pili; Serikali tulishatunga Sheria ya Baraza la Vijana na Vijana wanakosa chombo chao cha kujadili Kitaifa bila kujali itikadi zetu na Rais alishasaini. Je, ni nini kigugumizi cha kushindwa kutenga bajeti ya uanzishaji wa Baraza la Vijana kuanzia Taifa mpaka Kata? Tunahitaji commitment ya Serikali hatutaki ahadi. (Makofi)
Name
Paschal Katambi Patrobas
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Shinyanga Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Spika, tayari Serikali kwa agizo hilo la Serikali lililotolewa kupitia Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, tayari imekwisha kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana katika Halmashauri 84 zimekwisha tenga maeneo kwa ajili ya shughuli hiyo na eneo ambalo ni la mfano katika uzinduzi wa programu hii ya kutengewa maeneo kama agizo la kwenye Halmashauri nchini, lilifanyika hivi karibuni pale Kahama – Zongomela, kuna eneo kubwa ambalo vijana wanafanya shughuli mbalimbali pale zikiwemo pia za kilimo lakini pia biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anauliza ni lini Serikali sasa itaenda katika kukamilisha mchakato wa kupata Baraza la Vijana ikiwa sheria tayari. Tayari eneo hili ni agizo la Mheshimiwa Rais ambaye alizungumza alipokutana na vijana pale Mwanza, alitoa maelekezo na maelekezo hayo yanafanyiwa kazi na kwa kipindi chote tayari tumekwishaanza na mabadiliko kwa sasa. Tumeshafanya mabadiliko ya sera ya vijana ya mwaka 2007 na hatua ya pili itakuwa kwenda katika kuangalia uhitaji wa sasa katika sheria kama italazimika kuweza kufanya mabadiliko.
Mheshimiwa Spika, hatua ya tatu itakuwa sasa kuangalia kulingana na mazingira yaliyopo kama kutakuwa na ulazima kwa wakati wa sasa kuendana na situation iliyopo katika mahitaji ya vyombo vingi pia vya Kimataifa kama tutaweza tukaandaa Baraza la Vijana kwa kipindi hiki, lakini tayari michakato hii tayari tumekwisha kuianza kwa upande wa Serikali. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved