Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Halima James Mdee
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: - (a) Je, tangu janga la Corona lianze ni Watanzania wangapi wamepata maambukizi; wangapi wamekufa; na wangapi wamepona? (b) Je, ni fedha kiasi gani zimetengwa na Serikali na zimefanya nini na wapi katika kukabiliana na janga hili? (c) Je, nini kinapelekea gharama za kupima Covid- 19 kuwa kubwa na ni dawa gani zilizofanyiwa uchunguzi na kuthibitishwa kuwa zina uwezo wa kuzuia au kutibu Covid-19?
Supplementary Question 1
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza maswali yangu ya nyongeza, siafiki takwimu za Serikali kwa sababu Covid ilisambaa nchi nzima na kwa watu 725 ukigawanya tu kwa mikoa 31 maana yake kila mkoa wamekufa watu 23 ambayo haina mantiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kama nchi tulisimamisha mwaka mzima, Machi, 2020 mpaka Machi, 2021 kutoa takwimu. Kwa hiyo, hizi taarifa za takwimu siyo za ukweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maswali yangu ya nyongeza mawili; la kwanza, moja kati ya changamoto kubwa ilikuwa ni upimaji, kwa sababu ilikuwa lazima upime ndiyo ujue huyu mtu amekufa na Covid ama hajafa na Covid; sasa Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri sana juu ya mkopo wa shilingi bilioni 466 toka IMF, lakini hivi vitu alivyoviainisha hapa hakuna hata sentensi moja inayozungumzia ujenzi wa maabara ama uwepo wa maabara kwa ajili ya kupima Covid ama virusi vingine vinavyoashiria ama vinavyofanania na hivyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka aniambie, kwa sababu tunaishi na Covid-19 na virusi vinavyofanania na hivyo vitakuja, ni fedha kiasi gani katika mkopo huu wa shilingi bilioni 466 tutapeleka kwenye eneo la maabara specifically; na siyo hizi maabara sijui X-Ray, hizo zinatoa viashiria tu, kwamba kuna homa ya mapafu? Hilo ni la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusiana na dawa, nili-intend hapa kuuliza, tiba za asili za Tanzania kwa kiwango kikubwa sana zimechangia kutibu madhara yanayotokana na Covid. Imesaidia sana; na hizi ni fursa kwa watu wa tiba za asili kwa nchi, kwa ukanda na dunia: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka Serikali iniambie, mpaka sasa, kwa sababu kila siku mnajibu mnafanya tafiti, mmeshagundua ni tiba gani za asili ambazo ni sahihi kwa Watanzania watakaopata maradhi ama Virusi vya Covid ili wakiugua tujue protocol ya matibabu ni hii; na siyo sasa hivi kila mtu anakunywa kivyake mpaka tunakunywa sumu? Ni lini? (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimwambie tu rafiki yangu kwamba hii ni sayansi. Kama ni sayansi, inahitaji akili kubwa kuweza kuyaona hayo na siyo hisia za kwenye ma-corridor. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu kwamba Bugando, Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia amepeleka vifaa vya maabara vya kupima Corona vyenye thamani ya shilingi bilioni nne na mlinisikia nikisema. Kibong’oto ambayo ndiyo taasisi yetu ya magonjwa ambukizi, imepelekewa vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni sita na maabara inajengwa kwa thamani ya shilingi bilioni 14. Maabara yetu ya Taifa nayo inayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujue virus siyo mdudu mpya. Ni mdudu mpya kwenye genetic makeup lakini sayansi ni ile ile. Kwa hiyo, maabara ni zile zile, mashine ndiyo zimetofautiana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ni kuhusu tiba ya asili. Kwanza hatujaacha tiba ya asili. Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 1.2 imeenda NIMR kwa ajili ya kuchakata dawa zetu zilizoonekana kwamba zinatusaidia na kuziweka vizuri. Vilevile kwenye fedha hizi ambazo nilikuwa nazitaja, shilingi bilioni 466, imetengwa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya utafiti ule mkubwa na mgumu kwa ajili ya kuja na chanjo yetu ya Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa ninachoweza kumwambia Mheshimiwa, haya ya kisayansi huwa ni magumu, nawaachia wanasayansi. Unahitaji super computing system kubwa kuziona; hii siyo ngwini yaani, unajua. Kwa hiyo tulia. (Makofi)
Name
Rashid Abdallah Shangazi
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mlalo
Primary Question
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: - (a) Je, tangu janga la Corona lianze ni Watanzania wangapi wamepata maambukizi; wangapi wamekufa; na wangapi wamepona? (b) Je, ni fedha kiasi gani zimetengwa na Serikali na zimefanya nini na wapi katika kukabiliana na janga hili? (c) Je, nini kinapelekea gharama za kupima Covid- 19 kuwa kubwa na ni dawa gani zilizofanyiwa uchunguzi na kuthibitishwa kuwa zina uwezo wa kuzuia au kutibu Covid-19?
Supplementary Question 2
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami pamoja na majibu mazuri kabisa ya Daktari msomi, mwanasayansi Mheshimiwa Mollel, nina swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tulikuwa tunaona Serikali ikishiriki katika kampeni mbalimbali tunapokuwa na magonjwa haya ya mlipuko na magonjwa mengine. Kwa mfano tuliwahi kuwa na kampeni ya kutokomeza Malaria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufahamu, ni upi mpango wa Serikali kutumia wasanii wetu katika kuhamasisha, lakini pia kutoa elimu zaidi kwa wananchi hasa makundi ya vijana katika kupambana na Ugonjwa huu wa Uviko-19? Kwa sababu tunaona katika awamu hii kama wasanii hawajatumika sana katika eneo hili? Ni upi mpango wa Serikali?
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Mbunge ni muhimu sana; na kweli kwa kutumia wasanii wanaweza wakatufikishia vizuri sana ujumbe, lakini kikubwa ambacho kinaendelea sasa hivi ni kuhakikisha kwamba badala ya kutumia wasanii kutoka juu, tunapeleka kabisa huduma iende ikafanyike na jamii yenyewe kule chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imeonekana kwamba, ukiangalia fedha tulizonazo, ukitumia sana wasanii hawa wakubwa, ambao bado tunaendelea kuwatumia na tutawatumia jinsi watakapohitajika, lakini kwa kupeleka kule chini huduma inafika kwa urahisi zaidi kwa lugha inayoeleweka na watu wa jamii iliyoko eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tumesema tutakwenda kule na tukifika kule Umasaini tutawatumia wasanii walioko kule, lakini tutatumia redio na lugha zilizoko kule ili waweze kupata kirahisi na ili ujumbe ufike. Ila hatuna lengo la kuwaacha wasanii, isipokuwa tunatafuta namna ya kutumia hela kidogo kwa kufanya kazi kubwa zaidi. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Ester Amos Bulaya
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: - (a) Je, tangu janga la Corona lianze ni Watanzania wangapi wamepata maambukizi; wangapi wamekufa; na wangapi wamepona? (b) Je, ni fedha kiasi gani zimetengwa na Serikali na zimefanya nini na wapi katika kukabiliana na janga hili? (c) Je, nini kinapelekea gharama za kupima Covid- 19 kuwa kubwa na ni dawa gani zilizofanyiwa uchunguzi na kuthibitishwa kuwa zina uwezo wa kuzuia au kutibu Covid-19?
Supplementary Question 3
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Wakati Mheshimiwa Waziri anajibu maswali ya nyongeza, alisema wamefanikiwa kupeleka vifaa vya maabara kwenye maeneo mawili. Nchi yetu ukichanganya na Zanzibar ina mikoa 31, kwa Bara ni 26: Je, hamwoni kwamba hiki ni kikazi kiduchu kwa tatizo kubwa ambalo limetukumba la Covid? Ni lini mtahakikisha hizo maabara zinakuwepo nchi nzima na siyo hizi mbili ambazo zimetokana na pesa ya mkopo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Name
Dr. Godwin Oloyce Mollel
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Answer
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo niliyoyasema ni mifano tu. Nataka nimweleweshe Mheshimiwa Mbunge kwamba toka Uhuru tumekuwa na CT- Scan mbili tu kwenye nchi hii, kwenye hospitali za mikoa mbili tu, lakini amekuja leo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, tunakwenda kupata 29 ambazo zina gharama kubwa kuliko mashine za kupima Corona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka tu kumhakikishia ni kwamba tuna uwezo huo, mpaka leo tunapoongea hivi Mount Meru Hospital wanapima, Mbeya wanapima, kila mahali tutafikiwa. Kwa hiyo, usiogope, kazi inapigwa. Sisi tuendelee kusherehekea, karibuni upande huu kumenoga. (Kicheko/Makofi)