Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Flatei Gregory Massay
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbulu Vijijini
Primary Question
MHE. FLATEI G. MASSAY Aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupeleka umeme katika Vijiji na Vitongoji vya Jimbo la Mbulu Vijijini?
Supplementary Question 1
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, amekuja kuzindua umeme katika Jimbo la Mbulu Vijijini. Lakini nataka nimtaarifu kwamba pamoja na kuja kuzindua ule umeme baada ya kuondoka hakuna kilichoendelea, maana yake mkandarasi hayuko site.
Je, atafanya nini ili walau mkandarasi yule arudi site aweze kuendelea kuunganisha vile vijiji ambavyo mkandarasi amesaini kama mkataba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ziko kata ambazo kwa kweli zina hali mbaya na uliahidi kwamba umeme utafika; ni lini hasa zile kata ambazo wewe mwenyewe alitamka wakati anazindua umeme Mbulu Vijijini zitapata umeme? Maana sasa hivi kama nilivyosema, wakandarasi hawako site. Ahsante.
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nimpongeze Mheshimiwa Massay kwa sababu kweli tulikwenda kuzindua umeme katika jimbo lake na tulizindua umeme katika Kijiji kinachoitwa Munguhai, ni eneo zuri sana, na uwepo wa Mungu ulionekana kweli katika kijiji hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba mkandarasi anapopewa kazi ya REA kuna awamu kama nne za kufanya. Baada ya kusaini mkataba mkandarasi anakwenda site kufanya survey ili kubaini kama ile kazi iliyoandikwa kwenye karatasi ndiyo hasa ile ya kufanyika kazini. Na hiyo mara nyingi inachukua miezi mitatu mpaka mitano kulingana na hali ya hewa, eneo linavyofanana na wigo wa upana wa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linafanyika baada ya hapo, wanakwenda kufanya uhakiki watu wa TANESCO, REA pamoja na mkandarasi mwenyewe, wanashirikiana kuona kama kilichoonekana site ndicho hicho hasa ambacho kinatakiwa kifanyike na wanakubaliana. Baada ya hatua hiyo, inakwenda sasa kwenye ununuzi wa vifaa. Baada ya vifaa kupatikana ndiyo sasa tunakwenda kwenye utekelezaji wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi hatua tatu nilizozitaja za kwanza za survey, kwenda kwenye kufanya uhakiki na ununuzi wa vifaa unachukua miezi nane mpaka kumi kukamilika. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, najua kwenye maeneo mengi hatua hizi ndiyo sasa zinaelekea kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengi sana ambapo wakandarasi watakuwa hawaonekani site, siyo kwamba wame-abandon site, hapana, watakuwa kwenye moja wapo ya hizo hatua ambapo pengine hawaonekani kuwepo sana katika maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niwahakikishie kwa maelekezo yaliyokuwepo mikataba yote inatakiwa ikamilike Desemba mwaka huu na tunatarajia kuanzia mwezi Machi mwanzoni wakandarasi wengi watakuwa wamemaliza zile hatua za manunuzi na survey na watakuwa wamefikisha vifaa site wataanza kuonekana wakifanya kazi kwa miezi nane mfululizo ili kazi hizo ziweze kukamilika kwa wakati. Kwa hiyo na ndugu yangu, Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu Vijijini atakuwa kwenye category hiyohiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye eneo la pili kama nilivyosema tangu mwanzo, vijiji vyote ambavyo havina umeme vitapatiwa umeme kabla ya Desemba na vijiji vingine vilivyopo kwenye kata alizozitaja vikiwemo. Nashukuru.
Name
George Ranwell Mwenisongole
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mbozi
Primary Question
MHE. FLATEI G. MASSAY Aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupeleka umeme katika Vijiji na Vitongoji vya Jimbo la Mbulu Vijijini?
Supplementary Question 2
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa hii nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kuna mkanganyiko mkubwa kuhusu bei ya umeme vijijini; kwa nini Serikali isitoe tamko hapa Bungeni ili wananchi wote wanaoishi vijijini waelewe bei ya umeme vijijini ni shingapi, ni shilingi 27,000 au ni hiyo 300,000? Ili kuondokana na sintofahamu inayowapata wananchi wa vijijiji.
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Mwenisongole kwa swali lake zuri na kwa ufuatiliaji wa mambo yanayowahusu wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshatoa tamko na mimi nilirudie; umeme vijijini ni shilingi 27,000 kwa njia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie tena; kwa single phase vijijini umeme ni shilingi 27,000. Ilikuwa jana na itakuwa leo na kwa hali ilivyo sasa na maelekezo tuliyonayo itakuwa hivyo kesho, shilingi 27,000. (Makofi)
Name
Sophia Hebron Mwakagenda
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. FLATEI G. MASSAY Aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupeleka umeme katika Vijiji na Vitongoji vya Jimbo la Mbulu Vijijini?
Supplementary Question 3
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama ilivyo shida ya vitongoji vya Mbulu, katika Wilaya ya Rungwe Kitongoji cha Ngana kina wakazi wapatao 600, lakini waliounganishiwa umeme wa REA ni familia 36 tu peke yake; ni nini Serikali inajipanga kwenda kuhakikisha vitongoji vile na familia zingine zinapata umeme kama wanavyopata wananchi wengine?
Name
January Yusuf Makamba
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bumbuli
Answer
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Stephen Byabato, Naibu Waziri wa Nishati, kwa majibu mazuri ambayo aliyatoa awali katika maswali yaliyopita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nizungumzie hili suala la vitongoji kwa sababu hii changamoto ipo karibu katika kila jimbo, kwamba Serikali imefanya kazi kubwa sana ya kupeleka umeme katika vijiji karibu vyote, na tunavyo vijiji 12,345 hapa nchini na takribani vijiji vyote tutavimaliza itakapofika Desemba mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika vijiji hivyo tuna vitongoji 64,760, na katika vitongoji 64,000 vitongoji 37,610 havina umeme. Kwa hiyo, vitongoji zaidi ya asilimia 58 havijafikiwa na umeme wakati vijiji zaidi ya asilimia 80 vimepata umeme. Na tunafahamu kwamba manufaa ya umeme siyo unapofika kijijini, ni pale unapowafikia watu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetazama mahitaji ya kupeleka umeme katika vitongoji vyote, ni karibu shilingi trilioni 7.4, na tumeangalia mahitaji ya urefu wa nyaya, idadi ya transfoma na kila kitu ili tuweze kufanya kazi hii ya kupeleka umeme katika vitongoji vyote kwa muda mfupi. Ndiyo kazi ambayo nilikuwa nimefanya tangu niingie katika nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida kubwa ni fedha. Kwa utaratibu wa tunavyopata fedha za REA sasa hivi itachukua miaka 23 kumaliza vitongoji vyote. Sasa ndani ya Serikali tumetafakari na tumekuja na options tatu na hapo mbele tutaamua ni ipi twende nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, option ya kwanza ni hii ya sasa hivi tunayoendelea nayo ambayo itachukua muda mrefu, kama miaka 23. Option ya pili ili tufanye ndani ya miaka minne lazima tutenge bajeti karibu shilingi trilioni 1.8 kila mwaka kwa kazi hiyo. Option ya tatu ni kutoa hati fungani ya nishati vijijini (energy bond) ambayo mapato ya mafuta, ile petroleum levy ya shilingi 100, tunai-ringfence kwa miaka 20 ambayo itatupa karibu dola bilioni 3.1 na hiyo bond tunaipeleka sokoni, hizi fedha zote tunazipata sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lazima tukubaliane kwamba charge ya mafuta tutai-peg kwenye dola, hiyo shilingi 100 kwa miaka 20. Na matumizi ya sasa hivi ya mafuta ni lita milioni 10 kwa siku, kwa hiyo kwa miaka 20 – na tunaamini matumizi yataongezeka – kwa miaka 20 kwa hakika kabisa tutapata pesa za kulipa hiyo hati fungani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, option ya tatu ni kitu wanaita EPC plus F, Engineering, Procurement, Construction plus Financing, kwamba kampuni kubwa zinazoweza kupeleka umeme vijijini kwa mkupuo kwenye vitongoji zinakuja na proposal lakini na financing ambayo ni concessional; asilimia moja kwa miaka 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini kwamba katika kutafakari hizo options tunaweza tukapata ambayo itakuwa ni nafuu kwa maana ya interest, lakini itatuwezesha kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote kwa kipindi cha miaka minne. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutakapokamilisha kufanyia kazi hilo jambo tutakuja Bungeni na kuwaeleza ni option ipi ambayo tumekwenda nayo. Na tutakapoamua kwa hakika kabisa dhamira yetu sisi ni kwamba Wabunge hapa watakapokuwa wanaelekea kwenye uchaguzi basi umeme lisiwe jambo ambalo litawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na maelekezo hayo tumepewa na Mheshimiwa Rais, na katika kipindi hiki kifupi tutakuja na plan ya financing ya kupeleka umeme kwenye vitongoji 37,000 katika kipindi cha miaka minne ili tusisubiri miaka 20. Kwa hiyo, naamini kabisa maswali yote ya umeme vitongojini yatakuwa yameisha mara tutakapokuja na hiyo plan. Ahsante sana. (Makofi)
Name
Yahaya Omary Massare
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Primary Question
MHE. FLATEI G. MASSAY Aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupeleka umeme katika Vijiji na Vitongoji vya Jimbo la Mbulu Vijijini?
Supplementary Question 4
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii nami niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itupe ufafanuzi kidogo; pamoja na ufafanuzi uliotolewa wa shilingi 27,000 katika vijiji lakini kabla ya hapo kulikuwa na bei tatu; kulikuwa na 320,000; 177,000 kwenye vimiji vidogo kama Itigi na 27,000 kwa vijiji. Sasa wametoa wale wa 177,000 wamewapeleka kwa 320,000; vijiji ambavyo vimeungana vijiji vitatu vinne kwa kuwa tu vina kasoko basi vinaonekana ni mji vilipe 320,000/-. Je, Serikali iko tayari sasa kukubaliana na bei zilizokuwa kabla ya kurudi 27,000 na kuwa 177,000 kwa miji midogo? (Makofi)
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali zuri kutoka kwa Mheshimiwa Massare. Ni kweli hata kabla ya hapa tayari sisi kama Wizara kwa niaba ya Serikali tumeshapata mapendekezo na maoni na maombi mbalimbali ya ku-vary hizi gharama ambazo tuko nazo sasa. Na wengine wakaenda kwenye kupendekeza kwamba hata mtumishi wa Umma anavyolipwa posho anapoenda kwenye jiji, manispaa au wilaya, zile posho anazopewa zinatofautiana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Serikali niseme tumelipokea na tutakwenda kulifanyia kazi ili kuangalia uhalisia wa maisha tunayoishi sasa na gharama ambazo Serikali inaweza ikazitoza ili wananchi waweze kupata huduma hii ya umeme kwa gharama nafuu ambayo inamfikia kila mtu. (Makofi)
Name
Innocent Sebba Bilakwate
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyerwa
Primary Question
MHE. FLATEI G. MASSAY Aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kupeleka umeme katika Vijiji na Vitongoji vya Jimbo la Mbulu Vijijini?
Supplementary Question 5
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ambapo REA wamepeleka umeme wamepitisha laini kuu na pale chini kwa wananchi wa kawaida hakuna umeme. Kwa mfano nimueleze Mheshimiwa Waziri, nina vitongoji 610, vitongoji ambavyo havijafikiwa ni 503 na ukija kuangalia wanasema vijiji karibu asilimia zaidi ya 75 vimeshapata umeme, lakini ukiangalia wananchi wengi hawana umeme na mahitaji ni makubwa. Ni lini hivi vitongoji vitapelekewa umeme? (Makofi)
Name
Stephen Lujwahuka Byabato
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukoba Mjini
Answer
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, na ninamshukuru kaka yangu, Mheshimiwa Bilakwate, kwa swali zuri kabisa, na mimi Kyerwa ninapafahamu. Lakini ninaomba Mheshimiwa Bilakwate achukue tu na kuamini maelezo aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri, kwamba tunafahamu kwamba vitongoji vingi sana havina umeme na plan na mkakati mkubwa sana wa Serikali wa kufikisha umeme katika vitongoji hivyo vyote ndani ya miaka minne upo na unaendelea na utakapokuwa tayari vitongoji vyote 37,000 nchini ambavyo havina umeme vitapatiwa umeme.