Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuingiza lugha ya alama kwenye mitaala ya elimu nchini?

Supplementary Question 1

MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kuipongeza na kuishukuru sana Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo inazishughulikia changamoto mbalimbali za watu wenye ulemavu ikiwemo changamoto hii ya lugha ya alama; na ikikumbukwa kwamba changamoto hii niliweza kuizungumzia sana katika Bunge la Kumi na Moja, lakini hatimaye leo hii Serikali ya Awamu ya Sita imeanza kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia jamii yetu, yaani tunandaa kizazi ambacho kitaweza kuwasiliana na viziwi kwa maana ya Polisi, Walimu, Madaktari hata kwenye familia zetu. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali. Sina uwezo wa kupiga magoti, ningepiga magoti kuishukuru Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza la nyongeza ni kwamba, ni lini sasa mchakato huu utakamilika na hatimaye mitaala hii kuanza kutumika ndani ya nchi yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wakati tunasubiri ukamilishwaji wa mchakato huu, Serikali ina njia gani mbadala ya kuinua kiwango cha elimu kwa wenzetu viziwi? (Makofi)

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza naomba tupokee hizo pongezi za Mheshimiwa Rais kwa niaba yake, lakini tunaamini pongezi hizi zimemfikia na hiyo ndiyo Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan na huo ndiyo wajibu wetu kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba mchakato huu wa maboresho ya mitaala yetu ni agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alioutoa tarehe 22 Aprili, 2021. Mara tu baada ya maagizo yale, sisi kama Wizara tulikaa na kuanza kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato huu huwa unachukua muda mrefu, ni kati ya miaka mitatu mpaka mitano. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutajitahidi kuhakikisha kwamba katika kipindi kifupi kisichozidi miaka mitatu na miezi tisa mitaala yetu hii mipya iweze kuwa tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilihakikishie Bunge lako Tukufu, ifikapo mwaka 2025 Januari, mitaala yetu mipya itakuwa tayari kuanza kutumika katika maeneo yote kama tulivyokusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili amezungumzia juu ya namna gani watoto wetu tunawachukuwa kwa sasa hivi? Nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ipo mbioni na inaendelea kuwahudumia wanafunzi hawa au watoto wetu hawa. Kwanza tuna shule ya msingi ambazo tumejenga kule Mtwara inayoitwa Lukuledi kwa ajili ya kuwachukua wanafunzi hawa wenye matatizo ya uziwi kwa upande wa Shule za Msingi. Vilevile kule Patandi Arusha, tuna Shule ya Sekondari kwa ajili ya wanafunzi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, katika kipindi hiki tumeweza kutoa mafunzo kwa Walimu kwenye shule ambazo zinachukua wanafunzi wenye uziwi katika shule zetu zote za Sekondari katika kipindi kilichopita; na pia mwezi Machi mwaka huu Walimu wetu wa Shule za Msingi kwa shule zinazochukua wanafunzi hawa, nao vilevile tutawapa mafunzo ya lugha ya alama na kuwapa mbinu za namna ya kuwafundisha wanafunzi hawa. Ahsante. (Makofi)

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuingiza lugha ya alama kwenye mitaala ya elimu nchini?

Supplementary Question 2

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa kuna uhaba mkubwa sana wa Walimu wa Elimu Maalum nchini Tanzania na hasa katika Mkoa wangu wa Songwe; na sasa hivi Serikali ina-practice inclusive education kwa maana ya elimu jumuishi: -

Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka iwe ni compulsory kwa kila Mwalimu ambaye anasomea masuala ya elimu, kusomea elimu maalum kwa ajili ya watoto wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Shonza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika majibu yangu ya msingi, amezungumzia suala la inclusive education na nimeeleza, katika kipindi kilichopita tumeweza kutoa mafunzo kwa Walimu wote wa Shule za Sekondari katika shule zile ambazo zinachukua wanafunzi hawa wenye uziwi. Katika mwaka huu tunatarajia mwezi Machi tutafanya mafunzo kwa Walimu wote wa shule za msingi zile ambazo zinachukua wanafunzi hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa vile lengo lake ni kuhakikisha kwamba mitaala yetu inakwenda kuboreshwa ili somo hili liwe compulsory, hili ni eneo ambalo tutakwenda kulifanyia kazi katika uboreshaji wa mitaala hii ili wakati tunapoandaa mitaala, masomo ya lugha ya alama na mbinu za kufundishia wanafunzi wenye uziwi yaweze kuingia kwenye mitaala yetu. Ahsante sana.

Name

Zaytun Seif Swai

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuingiza lugha ya alama kwenye mitaala ya elimu nchini?

Supplementary Question 3

MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niulize swali dogo la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuwawezesha vijana wetu waweze kupambana na changamoto za uchumi wa kidigitali. Je, Serikali ina mpango gani wa kuingiza rasmi somo la TEHAMA, hususan kwa vitendo, katika mitaala yetu ya elimu ya msingi? Ahsante.

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Zaytun Swai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi. Kwa vile tunaenda kuboresha mitaala yetu na anazungumzia suala la TEHAMA kuweza kuingia katika mitaala yetu ili liweze kuwa compulsory, huu ndio wakati muafaka. Tunaomba tuyabebe mawazo haya na kwa vile tunaenda kuboresha tunaamini kabisa mtaala tutakaokuja nao ni ule ambao utakwenda kukidhi mahitaji ya Waheshimiwa Wabunge, lakini na Waheshimiwa wananchi wa Tanzania. Nakushukuru sana.

Name

Issaay Zacharia Paulo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Mjini

Primary Question

MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kuingiza lugha ya alama kwenye mitaala ya elimu nchini?

Supplementary Question 4

MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, Shule ya Msingi ya Endakoti katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu ina wanafunzi 40 wa elimu maalum. Shule hiyo iliyojengwa mwaka 1929 inakabiliwa na changamoto ya miundombinu. Je, ni lini Serikali itatekeleza azma yake ya kuteua shule mojawapo kila halmashauri itakayochukua wanafunzi wa elimu maalum ili vitengo hivyo viboreshwe kupata miundombinu na huduma nyingine?

Name

Omary Juma Kipanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Zacharia, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Zacharia kwa kuona umuhimu wa watoto wetu hawa kuweza kupata mazingira wezeshi na miundombinu wezeshi ili kuweza kufikia ndoto zao. Suala la uboreshaji wa mazingira ni suala endelevu na nadhani tumeona kwenye Serikali yetu kwenye kipindi hiki kifupi kilichopita zaidi ya trilioni 1.3 tulizozipata zimeweza kwenda kwenye eneo kubwa sana la miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika kipindi kijacho, kwa vile sasa tunaandaa bajeti, tutahakikisha kwamba, maeneo haya ambayo yanachukua wanafunzi wetu wenye mahitaji maalum tutakwenda kuyafanyia kazi na kuyapa kipaumbele kuhakikisha kwamba, yanapata miundombinu wezeshi, lakini vilevile na Walimu wa kutosha kwa ajili ya kuwafundisha watoto wetu. Ahsante sana.