Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Bonnah Ladislaus Kamoli
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Segerea
Primary Question
MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje kutoa elimu ya utunzaji mazingira kwa wakulima wa mbogamboga ikiwemo pamoja na hatua za kuchukua ili kulinda mazingira katika Bonde la Mto Msimbazi?
Supplementary Question 1
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza tunaunga mkono jitihada za Serikali. Hata hivyo, kuna wananchi ambao wanafanya shughuli zao za kilimo cha mbogamboga ambazo zinawaingizia kipato, wako ndani ya mita 60; na shughuli zao hizo haziathiri mazingira.
Je, Serikali iko tayari kuwasaidia wananchi hao au kuwalinda ili wazidi kujiongezea kipato?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa eneo hili linaweza likageuzwa kuwa vivutio au sehemu ambazo ni center ambazo wananchi wanaweza wakatengeneza, kama vile Coco Beach au sehemu nyingine, wakaweza kupata shughuli za kujiendeshea maisha yao.
Je, Serikali iko tayari kuwasiliana na Halmashauri zetu ili wananchi wetu ambao wanaweza kufanya shughuli hizi waweze kupewa maeneo haya?
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Segerea kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la mita 60 ni jambo la kikanuni kabisa. Lakini kingine tunaweza tukawaruhusu wakaendelea ndani ya mita 60; lakini changamoto iliyopo, athari za kimazingira si athari za kuonekana leo na kesho. Huwezi ukachimba mgodi leo, ukawa unachimba dhahabu au chochote ukaziona athari leo. Huwezi kukata miti ukaona athari leo, huwezi ukaendesha viwanda ukaona athari leo. Kwa hiyo ni jambo ambalo ni la muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo na kesho inawezekana wananchi wa Segerea wanaweza wasione athari za kimazingira, lakini baada ya muda watakuja kuona athari za kimazingira. Hicho ndicho kitu ambacho sisi Serikali tunakihofia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni vipi tutawasaidia, tuko tayari kuwasaidia kwa kuendelea kuwapa taaluma ili sasa waweze kufahamu mambo haya ili wajue athari za kimazingira. Kwa sababu tusipoyalinda mazingira hayataweza kutulinda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali lingine kwamba je, Serikali iko tayari kuwatengenezea creation centers kwa ajli ya angala ya kuweza kujiendesha. Hilo jambo wala hatuna tatizo nalo kwa sababu lengo letu ni kwasaidia wananchi; lakini nadhani watupe muda kwanza ili tutafute fedha kwa sababu hili jambo linahitaji fedha. Kupageuza pale ili tutengeneze sehemu ya kivutio yenye garden nzuri tunahitaji tupate fedha za kutosha. Lakini pia watupe muda ili tuweze kufanya ushauriano na baadhi ya wadau wengine maana pale Wizara za Maji, Maliasili na Ardhi, pamoja na sisi na Halmashauri zinahusika. Kwa hiyo jambo hilo linawezekana, lakini watupe muda kidogo ili tujue namna ambavyo tunafanya. Nakushukuru.
Name
Neema Kichiki Lugangira
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje kutoa elimu ya utunzaji mazingira kwa wakulima wa mbogamboga ikiwemo pamoja na hatua za kuchukua ili kulinda mazingira katika Bonde la Mto Msimbazi?
Supplementary Question 2
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru; kwa kuwa leo ni Siku ya Saratani Duniani, ningependa kuiuliza Serikali, ina mkakati gani wa kuzuia wenye viwanda ambao wanachepusha machi yenye kemikali ambazo si salama? Maji haya yanakwenda kwenye Mto Msimbazi na ndiyo maji hayo hayo ambayo hawa wakulima wa mbogamboga wanatumia katika kuzalisha na kumwagilia mbogamboga hizi, hivyo kuhatarisha usalama wa chakula (food safety) na hatimaye usalama wa hali ya afya ya wananchi na hivyo uwezekano wa kuchangia katika saratani ni mkubwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majibu.
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena kujibu swali la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumebaini kuwa kuna baadhi ya shughuli nyingine za kibinadamu zinasababisha uchafuzi wa mazingira, zikiwemo hizo ambazo amezitaja, za viwanda na nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali kupitia Ofisi ya Makamu Rais, Muungano na Mazingira tunazo jitihada Madhubuti ambazo huwa tunazichukua katika kuhakikisha kwamba tunazuia mambo haya ili kuweza kuzuia athari kwa wananchi, ikiwemo hiyo milipuko ya maradhi, yakiwemo ya kansa na mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, tunaendelea kutoa taaluma kwa hawa wanaofanya shughuli hizi za kibinadamu, lakini la pili kuna wakati tunatoa hata faini ili waweze kuacha na iwe funzo kwa wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile huwa tunafanya operations za mara kwa mara kwenye haya maeneo ya uzalishaji, lengo na madhumuni ni kwamba wanaozalisha wajue kwamba wanazalisha lakini wananchi nao wanaathirika. Lakini zaidi tunafika hatua mpaka tunazuia. Inafika wakati kuna kiwanda kinafanya visivyo, kuna shell inafanya isivyo, kuna migodi inafanya visivyo. Kisheria, kwa mujibu wa utaratibu tunazuia uzalishaji ili sasa shughuli nyingine au taratibu nyingine za uhifadhi wa mazingira ziweze kuendelea. Nakushukuru.
Name
Asya Mwadini Mohammed
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BONNAH L. KAMOLI aliuliza: - Je, Serikali imejipangaje kutoa elimu ya utunzaji mazingira kwa wakulima wa mbogamboga ikiwemo pamoja na hatua za kuchukua ili kulinda mazingira katika Bonde la Mto Msimbazi?
Supplementary Question 3
MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ukosefu wa taaluma za kimazingira katika Bonde la Mto Msimbazi ambayo husababisha uchafuzi wa kimazingira kutokea, hali kadhalika ukosefu huu wa elimu unawahusu hasa wavuvi ambapo bahari yetu imechafuka sana na tunakosa samaki wenye afya kutokana na wavuvi kwenda na plastics na vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusikia Serikali ina mkakati gani, kwanza kuisimamia rasilimali hii muhimu ya bahari, lakini la pili, kutoa taaluma kwa wavuvi wetu ili rasilimali yetu iwe salama?
Name
Khamis Hamza Khamis
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Uzini
Answer
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kujibu swali lingine la Mheshimiwa Asya, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kazi kubwa tunayofanya kama Serikali na kama Wizara hii ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira ni kuwapa wananchi elimu; na ni kwa sababu tumefika wakati tumegundua kwamba elimu pekee ndiyo itakayotuokoa sisi kutokana na mazingira machafu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wavuvi tumefanya jitihada kubwa. Kaskazini Unguja, kwa sababu kuna bahari tumewapa elimu, Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na maeneo yote ya Tanzania yenye visiwa, mito, maziwa pamoja na bahari ambamo shughuli za uvuvi zinafanyika tumejitahidi sana tumewapa taaluma na taaluma inafanya kazi, na tutandelea kufanya hivyo. Nakushukuru.