Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa barabara za kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mikoa ya jirani utaanza?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa maswali madogo mazuri ya nyongeza. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini mradi wa barabara inayounganisha Jimbo la Iringa Mjini, Jimbo la Kalenga na Jimbo la Kilolo utakamilika? Kwa sababu mradi huo ni wa siku nyingi sana na wakati wa mvua wananchi wanapata mateso makubwa na barabara hiyo ni ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ni lini mradi wa barabara ya Msembe inayokwenda Ruaha National Park utakamilika? Kwa sababu barabara hiyo pia ni ya kiuchumi na inakosesha mapato makubwa sana kwa Serikali kwa kuingiza mapato ya watalii wa ndani na wa nje. (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na jibu la barabara ya Ruaha National Park; barabara hii ipo kwenye bajeti na iko kwenye taratibu za manunuzi. Hali kadhalika barabara ya Iringa kwenda Kilolo inaendelea kujengwa na tuna hakika kadri fedha zitakavyopatikana barabara hii ni azma ya Serikali iweze kukamilika kwa kiwango cha lami. Ahsante.

Name

Jerry William Silaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ukonga

Primary Question

MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa barabara za kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mikoa ya jirani utaanza?

Supplementary Question 2

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza. Kwanza niipongeze Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa inayofanya kwenye miundombinu ya barabara. Tarehe 1 Februari Daraja la Tanzanite limeanza kutumika pale Dar es Salaam. Kwa niaba ya watu wa Dar es Salaam tushukuru sana na nikuombe Kamati za mwezi Machi zifanye ziara Dar es Salaam mpate kupiga picha pale kwenye daraja la kisasa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hali ya barabara kwenye Jimbo la Ukonga inaweza isitofautiane sana na kule Katavi kwa Mheshimiwa Martha aliyeuliza swali la msingi. Iko barabara ya Banana – Kitunda – Kivule – Msongola (kilometa 14.7) ambayo nishukuru sana Serikali imeshajengwa kwa kilometa 3.2 na kwenye Ilani ya Uchaguzi ukurasa wa 78 inaeleza wazi kukamilisha ujenzi wa barabara kwa kilometa 11.5 kutoka eneo la Kivule Mwembeni – Fremu Kumi –Msongola.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii inahudumia watu wengi na hali yake ni mbaya mpaka inasababisha…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jerry swali.

MHE. JERRY W. SILAA: …mpaka inasababisha Mbunge siwezi kufanya ziara Kivule bila kuwa na mabaunsa wa kunilinda kutokana na kero kubwa kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Serikali inieleze, haioni inahitajika jitihada ya dharura kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kwa kilometa hizi 11.5 kama inavyosema kwenye Ilani ya Uchaguzi?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipokee pongezi kwa niaba ya Serikali kutoka kwa Mbunge kwa kazi ambazo Serikali inaendelea kuzifanya, shughuli za miundombinu na ninaomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Ukonga kwamba barabara ya Banana – Kitunda –Msongola kama ilivyoainishwa kwenye Ilani, lakini pia iko kwenye mpango wa Wizara kujengwa kwa kiwango cha lami na Serikali ina mpango wa kukamilisha barabara hii na ndiyo tayari kwanza tumeshakamilisha kilimeta 3.2 na hizo kilometa zilizobaki tunahakikisha kwamba tutazikamilisha ili wananchi waweze kupata huduma sahihi. Ahsante.

Name

Dr. Josephat Mathias Gwajima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kawe

Primary Question

MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa barabara za kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mikoa ya jirani utaanza?

Supplementary Question 3

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya barabara za Katavi yanafanana sana na matatizo ya barabara ya Kawe. Nataka kuuliza swali dogo kwa Mheshimiwa Waziri; barabara ya Bagamoyo – Tegeta imejengwa hapo katikati haina mitaro kabisa na matokeo yake inasababisha mafuriko kwenye maeneo ya Basihaya, DAWASCO na Boko; ni lini sasa Mheshimiwa Waziri utakwenda pamoja na mimi uone jinsi ambavyo TANROADS wamejenga bila mtaro kabisa na inasababisha mafuriko ambayo yanahatarisha maisha ya wananchi? Ni lini Mheshimiwa Waziri?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Askofu Gwajima, Mbunge wa Kawe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie mara baada ya kumalizika kwa Bunge tutaambatana naye kwenda kutembelea barabara hii. Ahsante.

Name

Mariamu Nassoro Kisangi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa barabara za kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mikoa ya jirani utaanza?

Supplementary Question 4

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza, lakini pia niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuweka jiwe la msingi barabara ya mwendokasi ya Mbagala, kutoka Bendera Tatu kwenda Mbagala mambo ni mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la nyongeza; ni lini sasa Serikali itakamilisha barabara ya kutoka Mbagala Kokoto mpaka kwenda Kongowe kupunguza msongamano wa magari na kero kubwa ya kupoteza muda katika eneo la Mbagala Rangi Tatu? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitaja ni muhimu sana na imeainishwa kukamilishwa kwa kiwango cha lami, lakini itajengwa kulingana na upatikanaji wa fedha na kwa kuwa tuko kwenye kipindi cha bajeti basi tutaangalia ili iweze kupangiwa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha. Ahsante.

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa barabara za kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mikoa ya jirani utaanza?

Supplementary Question 5

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaomba kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Lupila kuelekea Kipengere ni barabara ambayo inaunganisha Wilaya za Ludewa, Makete na Wanging’ombe na tumeiombea kibali kwenye RCC cha kupandishwa hadhi ya TANROADS, hadi leo takribani miaka mitatu imepita.

Je, ni lini Wizara itatoa kibali barabara iwe chini ya TANROADS ili iweze kujengwa na kupitika kwa uhakika kwa sababu wananchi wangu wanateseka sana?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Festo Sanga, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zote ambazo zinahudumiwa na TAMISEMI kwa maana ya TARURA zina utaratibu wake. Naomba kama imefanyiwa tathmini inawezekana imeshindwa kukidhi viwango, lakini tunaomba Mheshimiwa Mbunge baada ya hapa tuonane ili tuweze kuona ni kitu gani kinakwamisha barabara hii kama inakidhi viwango isiweze kupandishwa hadhi na kuhudumiwa na TANROADS. Ahsante.

Name

Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa barabara za kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mikoa ya jirani utaanza?

Supplementary Question 6

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa Mbunge wa Kawe, mwaka 2015-2020 barabara ya Chuo cha Ardhi – Makongo Juu – Goba ilikuwa ina changamoto kubwa sana, tukafanikiwa kujenga kipande kutoka Goba mpaka Makongo Juu. Ilivyofika mwaka 2020 kipande cha Makongo Juu kwenda Chuo cha Ardhi akapatikana mkandarasi ambaye ikasemekana angejenga ndani ya mwaka mmoja. Sasa hivi ni mwaka wa tatu toka mwaka 2020 mpaka 2022 mkandarasi aliyeko anasuasua, sasa sijui tatizo ni mkandarasi ama tatizo ni ufuatiliaji.

MWENYEKITI: Uliza swali Mheshimiwa Halima Mdee.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Waziri wa Ujenzi aniambie ni lini kipande cha barabara cha Makongo Juu kwenda Chuo cha Ardhi kitakamilika na kwa viwango vyote? (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima Mdee, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Halima Mdee kwamba barabara hii ambayo inajengwa na anasema inachukua muda nimhakikishie kwamba kutoka hapa nitahakikisha nafuatilia nijue tatizo ni nini na nitatoa majibu kwa nini barabara hii imechukua muda mrefu. Ahsante.

Name

Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Primary Question

MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa barabara za kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mikoa ya jirani utaanza?

Supplementary Question 7

MHE KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. kama ilivyo kwa Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Tanga haujaunganishwa na Mikoa miwili; Morogoro na Manyara. Barabara ya Handeni – Mziha – Turiani na barabara ya Handeni – Kiberashi – Kiteto – Kondoa – Singida; ni lini Serikali itakamilisha taratibu za kuanza ujenzi wa barabara hizi mbili?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kwagilwa, Mbunge wa Handeni Mjini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayoanza Handeni kwenda Kiberashi hadi Kwamtoro taratibu zipo zinaendelea kwa kuanza na kilometa 50 na ziko kwenye hatua ya manunuzi; na barabara ya Handeni – Turiani upande wa kwenda Turiani barabara inaendelea kujengwa na bado hatujakamilisha kwa sababu ya upatikanaji wa fedha, lakini tayari nayo tumeshaanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, ni matumaini ya Serikali kwamba barabara zote ziko kwenye mpango na zitakamilishwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.

Name

Tarimba Gulam Abbas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Primary Question

MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa barabara za kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mikoa ya jirani utaanza?

Supplementary Question 8

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi, lakini la pili, nikupongeze wewe pamoja na Wabunge wote wapenzi wa Simba Sports Club kwa kuonja ushindi angalau jana; matarajio yetu mtaendelea na utaratibu huo ambao mmeuanzisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu; naomba nipate kauli ya Serikali juu ya matumizi ya barabara wanazozijenga Serikali, hasa barabara ya mwendokasi pale Dar es Salaam na hususan katika Jimbo langu la Kinondoni. Matumizi ya barabara zile yamekuwa mabaya sana, pikipiki zinapita, magari binafsi yanapita, magari ya Serikali yanapita, hali ambayo inasababisha ajali nyingi sana.

Ni nini kauli ya Serikali pamoja na vyombo vyake kuhakikisha kwamba tabia hii ya kutumia vibaya barabara zinazojengwa…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tarimba umeshaeleweka; Mheshimiwa Waziri.

MHE. TARIMBA G. ABBAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, lakini na la kwanza umenielewa Mheshimiwa, la pongezi. (Kicheko)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tarimba, Mbunge wa Kinondoni, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli alichokisema Mheshimiwa Mbunge kwamba kumekuwa na kutokutumia vizuri barabara hizi za mwendokasi na inawezekana ni kwa sababu tu hizi barabara kwetu ni mpya. Lakini naomba nitumie nafasi hii kuwajulisha wananchi wa Tanzania kwamba zile barabara zimewekewa alama na zina matumizi yake. Barabara ya mwendokasi ni ya mwendokasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nitumie nafasi hii kuhakikisha kwamba watumiaji wote wa barabara hizi za Dar es Salaam ambapo mwendokasi unapita basi wazingatie sheria ili tusisababishe ajali na matatizo mbalimbali kwa watumiaji wa barabara. Ahsante. (Makofi)

Name

George Ranwell Mwenisongole

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa barabara za kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mikoa ya jirani utaanza?

Supplementary Question 9

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa hii nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Barabara ya Mlowo – Utambalila – Kilyamatundu inaunganisha Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Katavi, na ni barabara ya pili kwa ukubwa ndani ya Mkoa wetu wa Songwe. Kwa sasa hii barabara maeneo ya Itewe pale Itaka pameharibika na imesababisha kero kubwa kwa wananchi wa Songwe, Mbozi na mikoa ya jirani. Ni nini kauli ya Serikali kuhusu matengenezo ya haraka yanayohitajika ili kuinusuru barabara hiyo na hizi mvua zinazoendelea?

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mlowo – Itaka – Kilyamatundu ni barabara muhimu sana kwa Mkoa wa Songwe ambayo inaunganisha na Mkoa wa Rukwa; na kwa kuwa hiki ni kipindi cha mvua, naomba pia nitumie nafasi hii kuwajulisha na kuwaelekeza Mameneja wote wa TANROADS kuhakikisha kwamba kila kunapotokea changamoto kwenye barabara ambazo tunazihudumia basi wazishughulikie mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na nitumie nafasi hii kumuagiza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe kesho afike eneo la Itaka, Kijiji cha Itewe kwenye changamoto ili aweze kutatua hiyo changamoto, na mimi mwenyewe binafsi na Mheshimiwa Mbunge tuweze kupata majawabu. Ahsante.

Name

Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Primary Question

MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. MARTHA F. MARIKI aliuliza: - Je, ni lini ujenzi wa barabara za kuunganisha Mkoa wa Katavi na Mikoa ya jirani utaanza?

Supplementary Question 10

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi Novemba nilikuwa kwenye kata yangu inaitwa Lugulu, Mheshimiwa Naibu Waziri akanifuata kule akaja akaniambia kwamba barabara yangu ya Mkomazi – Kisiwani Same yote inatangazwa kujengwa moja kwa moja.

Sasa ninapenda Mheshimiwa Waziri awatangazie wananchi wangu ndani ya Bunge kile alichoniambia kule Lugulu ili wananchi wangu wasikie. Nashukuru. (Makofi)

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anne Kilango, Mbunge wa Same Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru na nimpongeze Mheshimiwa Anne Kilango kwa kufuatilia maendeleo ya barabara za jimbo lake; na ni kweli nilikwenda kwenye jimbo lake na yalikuwa ni maagizo pia ya Kiti kwamba niende nikatembelee barabara za Same.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizi zote ambazo tumeziongelea sana ziko kwenye hatua mbalimbali za manunuzi ikiwepo na barabara aliyoitaja ya Kisiwani –Mkomazi. Ahsante.