Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Primary Question

MHE. FESTO R. SANGA aliuza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutekeleza Mradi wa REA katika Wilaya ya Makete ili kuhakikisha umeme unafika kila Kijiji?

Supplementary Question 1

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza niishukuru Wizara ya Nishati hasa Mheshimiwa Rais, Makete tulikuwa na vijiji 37 havina umeme, lakini mkandarasi amekuja na anaendelea kazi vizuri, lakini changamoto ambayo tuko nayo, swali la kwanza, ni kwa mkandarasi wa REA phase III round one ambaye hadi sasa hajakamilisha kazi ya kusambaza umeme kwenye vijiji baadhi ya Makete. Je, ipi kauli ya Serikali kwa mkandarasi huyo ambaye hadi dakika hii amefelisha zoezi la kusambaza umeme kwenye vijiji kadhaa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Makete tulipewa bwawa la umeme la Lumakalia sisi tunaita bwawa la Luvaninya, hili bwawa kwa muda mrefu limekuwa likitamkwa wananchi wangu hawajajua hadi sasa hivi ni lini linaanza kujengwa. Sasa naomba kauli ya Serikali, ni lini Serikali itaanza kujenga bwawa hili ambalo linaenda kutatua kero ya umeme kule Makete na mikoa ya karibu kama Mbeya?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Festo Sanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza, nipende kupokea shukrani alizozitoa kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha kwamba umeme unafika katika vijiji vyote na sisi kama Serikali tunaendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza majukumu ambayo ametupatia.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba REA III round ya kwanza kuna maeneo hayajakamilika. Zilikuwepo lots 29 na zilizokamilika kabisa ni lots 21, lots nane bado hazijakamilika na eneo la Makete likiwemo. Kauli ya Serikali ni kwamba tumeingia mkataba wa nyongeza ya muda kidogo na wakandarasi na tumekubaliana nao ifikapo Machi mwaka huu, kazi zote zimekamilika.

Mheshimiwa Spika, niseme moja wapo ya sababu kubwa ambayo ilichelewesha miradi hii ni UVIKO ambao ulichelewesha vifaa kupatikana, lakini sababu nyingine kubwa ambayo ilikuwa inatokea ambayo maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tumeyatekeleza na kubadilisha utaratibu REA III round one ilikuwa inaenda kwa utaratibu unaoitwa goods na siyo works, yaani wakandarasi walikuwa wanapewa pesa, wanunua vifaa ,wakishafikisha vifaa ndiyo sasa tunaanza kuwapa utekelezaji wa kazi. Hii imepelekea sasa wakandarasi wengine washindwe kufanya kazi na mikataba yao ikabidi tuivunje ili kupata wengine, kwa hiyo muda ukapotea.

Mheshimiwa Spika, kwenye REA III round II maelekezo tuliyoyapata na tutayatekeleza ni kwamba, mradi unatekelezwa kwenye utaratibu wa works, mkandarasi analipwa kwa kile kiwango cha kazi aliyofanya na tunaamini hiyo itatusaidia kukamilisha kazi zetu zote tulizonazo kwa wakati kwa sababu usipokamilisha kazi inabakia kazi sawa na pesa ambayo haujaifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la pili, ni kweli kwamba kule Makete na maeneo mengine ya Njombe kuna Mradi unaitwa Rumakali ambao Serikali inatarajia kuutekeleza na pale tutapata Megawatts 222. Feasibility ya pale ilifanyika mwaka 1998 na kwa kuwa tumeona uwezo wa kupata fedha wenzetu wa TANESCO wamemweka Consultant mpya wa kufanya update ya ile feasibility study ili tuendane na hali ya sasa. Kwa hiyo, kinachofanyika sasa, mkandarasi wa feasibility study ameanza kazi yake Januari, tunatarajia atamaliza mwezi wa Tano na kuanzia mwezi wa Tano itaanza kufanyika evaluation kwa ajili ya compensate wale watu walioko maeneo yale.

Mheshimiwa Spika, tunatarajia mwishoni mwa mwaka huu mambo yote yatakuwa yamekamilika, hivyo mwaka ujao pesa ya kujenga mradi itakuwa imepatikana na tunaweza kuanza kutekeleza mradi huo kwa ajili ya kuongeza umeme unaozalishwa kwenye maji katika Gridi ya Taifa.

Name

Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FESTO R. SANGA aliuza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutekeleza Mradi wa REA katika Wilaya ya Makete ili kuhakikisha umeme unafika kila Kijiji?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Napenda kuuliza na kujua tatizo lililopo hasa TANESCO kwa upande wa Morogoro Mjini; baadhi ya wananchi wamelipia umeme kuwekewa kwenye nyumba zao lakini imechukua muda mrefu hawajawekewa mpaka sasa hivi. Kwa mfano, Kata ya Kasanga kuna wananchi wamelipia lakini mpaka hivi sasa hawajawekewa: -

Je, kuna tatizo gani?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Christine Ishengoma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wapo wateja ambao wamelipia huduma ya TANESCO lakini walikuwa hawajaipata na hii ni kutokana na kwamba kulikuwa kuna mwamko mkubwa sana kwa wananchi wanaohitaji umeme na uwezo wetu TANESCO kidogo ulikuwa umepungua kwa sababu ya kutokuwepo na vifaa vya kutosha kukamilisha kazi hizi.

Mheshimiwa Spika, tayari Mheshimiwa Rais ameshaelekeza, Wizara yetu inasimamia TANESCO kuhakikisha kwamba vile viporo ambavyo ni vya nyuma angalau visiwepo zaidi ya miezi mitatu iliyopita. Yaani mtu akilipa Februari hii, angalau mwezi Machi au Aprili awe ameunganishiwa umeme. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Ishengoma pamoja na Wabunge wengine wote kwamba Serikali inajitahidi kuhakikisha kwamba vile viporo vya kuunganisha umeme vinaunganishwa na kukamilika ndani ya muda mfupi ili kila mtu aweze kunufaika na umeme ambao unazalishwa.

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Primary Question

MHE. FESTO R. SANGA aliuza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutekeleza Mradi wa REA katika Wilaya ya Makete ili kuhakikisha umeme unafika kila Kijiji?

Supplementary Question 3

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na jitihada kubwa ambayo imefanywa na Mheshimiwa Rais kupitia Wizara ya Nishati kusambaza umeme kwa kiwango kikubwa, lakini changamoto kubwa ni kwamba inaonekana fedha hazitoshi kwa ajili ya usambazaji wa umeme kwa line ndogo ndogo.

Mheshimiwa Spika, Wizara ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inapata fedha ili wananchi hawa sasa wafaidi umeme kupitia line ambazo zimeshajengwa nchini Tanzania?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Engineer Manyanya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mahitaji ni makubwa lakini pesa haitoshi. Hata hivyo, Serikali ya Awamu ya Sita tayari imetoa shilingi 1,250,000,000,000 kwa ajili ya upelekaji wa umeme katika vijiji. Hivyo, tunaamini pesa angalau ipo ya kutosheleza mahitaji kadhaa tuliyokuwa nayo.

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema juzi Mheshimiwa Waziri wa Nishati, kwamba sisi Wizara ya Nishati tunao mkakati mkubwa ambao baadaye utakuja kuwasilishwa kwa Mheshimiwa Rais na kwenu, kwamba tunatafuta fedha kwa ajili ya kupeleka umeme katika vitongoji vyote nchini na makadirio yetu yanaonesha ni kama shilingi trilioni saba na nusu. Tunaamini kwa sababu tunakopesheka, tunaaminika kwa Mataifa mengine na tunahitaji kupeleka umeme kwa wananchi wetu, fedha hiyo tutaitafuta na tutaipata kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kila mwananchi anayehitaji umeme anaupata.

Mheshimwia Spika, Mheshimiwa Waziri alisema, angalau ifikapo 2025 jambo hilo liwe limekamilika, Mheshimiwa Rais akisimama basi kura zimwagike kwa ajili ya kushinda vizuri.

Name

Benaya Liuka Kapinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Vijijini

Primary Question

MHE. FESTO R. SANGA aliuza: - Je, Serikali ina mpango gani wa kutekeleza Mradi wa REA katika Wilaya ya Makete ili kuhakikisha umeme unafika kila Kijiji?

Supplementary Question 4

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona. Utekelezaji wa REA III, round ya pili Jimbo la Mbinga unakwenda kwa kusuasua sana. Mpaka nakuja hapa Mkandarasi alikuwa bado hajafanya chochote.

Nini kauli ya Serikali juu ya Mkandarasi huyu?

Name

Stephen Lujwahuka Byabato

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kapinga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wakandarasi wa REA wanazo hatua kadhaa za utekelezaji wa miradi. Wanafanya survey, wanafanya uhakiki, wananunua vifaa na baadaye wanaanza kujenga. Hizi hatua tatu za mwanzo mara nyingi hawaonekani site, wanapoanza kujenga ndiyo wanaonekana. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Mkandarasi atakuwa kwenye mojawapo ya hatua hizo na kabla ya mwezi Machi ataonekana site kwa ajili ya kuendelea na kazi ambayo tayari amepewa kwa sababu deadline yake ni mwezi wa Desemba, 2022 na tunaamini ataikamilisha.