Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Name
Bernadeta Kasabago Mushashu
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Primary Question
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: - Je, ni lini wananchi waliokuwa wameweka fedha zao katika Benki ya Wakulima wa Kagera ya KFCB iliyofungwa na Benki Kuu Mwaka 2018 watarejeshewa fedha zao?
Supplementary Question 1
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza. Ufungaji wa Benki ya Wakulima ya Kagera iliyopo pale Manispaa ya Bukoba, iliwaumiza watu wengi ambao hawakuwa na hatia wakiwepo vikundi vya akinamama, SACCOS za akinamama, wakulima, wajasiriamali na hata wale wastaafu waliokuwa wameweka akiba zao. Serikali iliwalipa Sh.1,500,000/= pekee hata kama mtu alikuwa na akiba ya shilingi milioni 40. Sasa hivi anatuambia kwamba Serikali imekuwa ikikusanya madeni, pamoja na kuuza mali za Benki hiyo tangu mwaka 2018. Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha hilo zoezi la kuwalipa hiyo Sh.1,500,000/= pamoja na akiba zote walizokuwa wameweka kwenye hiyo benki? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa nini Serikali isione umuhimu sasa badala ya kuzifunga, ikaziunganisha hizi Benki ndogo ndogo, kama ilivyofanya ikaunganisha Benki ya Wanawake, Benki ya Posta, Benki ya Twiga, TIB wakatengeneza Tanzania Commercial Bank kwa hiyo, mtaji ukawa umeongezeka kuliko kungoja sasa hizi Benki wakazifilisi na wakawaumiza wananchi ambao wanakuwa wameweka akiba zao kwenye hizo Benki? (Makofi)
Name
Hamad Hassan Chande
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Answer
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu awali ya yote napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Mushashu, kwa juhudi yake ya kuwatetea wananchi hao ambao walipata hasara hiyo katika benki iliyohusika, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini ndugu yangu Byabato, kwa kuwa wanafuatilia kwa karibu suala hili lililojitokeza katika Benki hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la ulipaji wa fidia ya amana linaendelea mpaka hivi sasa tunavyozungumza. Wale wote ambao hawajajitokeza kwenda kuchukua amana hiyo, basi tunamwomba Mheshimiwa Mbunge, awashajihishe watu hao waende kupata fidia hiyo isiyozidi Sh.1,500,000/=. Wale ambao amana yao ni zaidi ya Sh.1,500,000/= waendelee kuwa na subira, mpaka zoezi la ufilisi wa benki hiyo utakapokamilika na watalipwa kwa mujibu wa taratibu za ufilisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili. Serikali tayari imeshaanza zoezi kwa upande wake kuziunganisha Benki, ambazo zilipata changamoto mbalimbali zikiwemo mitaji. Tayari Serikali yetu imeshaziunganisha Benki ya Posta, Benki ya Wanawake, Benki ya TWIGA na Benki ya TIB na kuunda Benki inayojulikana kwa jina la Benki ya Biashara Tanzania (TCB). Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved